Mkutano wa Kumi wa Wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa Kuhusu Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote wa Austria tarehe 16 Juni 2026 Mkutano wa Kumi wa Wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa Kuhusu Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote wa Austria tarehe 16 Juni 2026  (LISA LEUTNER)

Papa Leo XIV Utunzaji Bora wa Mazingira: Imani, Matumaini na Mapendo!

Papa Leo XIV katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa Mkutano wa Kumi wa Wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa Kuhusu Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote wa Austria amejikita katika nguzo kuu tatu ambazo kimsingi ni fadhila za Kikristo yaani: Imani, Matumaini na Mapendo, mambo msingi yanayoweza kusaidia majadiliano katika mkutano huu. Imani katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Kumi wa Wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa Kuhusu Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote wa Austria umefanyika tarehe 16 Juni 2026. Hii ni kati ya mikutano muhimu sana ya Kimataifa inayojadili kwa kina na mapana kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, uvumbuzi na suluhisho endelevu Mkutano huo umeandaliwa na Mpango wa Hali ya Hewa wa Schwarzenegger na umefanyika huko Vienna, Hofburg nchini Austria. Ni mkutano unaowajumuisha viongozi wakuu kutoka katika siasa, biashara, sayansi na kutoka katika mashirika ya kiraia na hukutana kila mwaka, ili kujadili mustakabali wa dunia mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mkutano wa Kumi wa Wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa Kuhusu Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote wa Austria ulianzishwa kunako mwaka 2017 na umekuwa ni jukwaa linalotambulika Kimataifa na sehemu muhimu sana ya majadiliano kuhusu: Ubunifu, ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mama Kanisa amekuwa daima makini ili kuhakikisha kwamba, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote unakuwa ni endelevu kwa kujikita katika ikolojia shirikishi na kwamba, hii ni sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwani suala zima la kiikolojia lina mwelekeo pia wa kanuni maadili na utu wema. Kwa hakika mgogoro wa kimazingira ni suala la kiikolojia linalogusa na kutikisa mgogoro mamboleo wa kijamii na kiuchumi. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano huu huko Austria amejikita katika nguzo kuu tatu ambazo kimsingi ni fadhila za Kikristo yaani: Imani, Matumaini na Mapendo, mambo msingi yanayoweza kusaidia majadiliano katika mkutano huu. Imani katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. 

Wajumbe wa mkutano wa kumi wa wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa
Wajumbe wa mkutano wa kumi wa wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa   (LISA LEUTNER)

Huu ni mwelekeo wa kidini kwa kuamini kwamba, Ulimwengu ni kazi ya Mwenyezi Mungu na mwanadamu amekabidhiwa kuulinda, kuutunza na kuudumisha. Kumbe mgogoro wa Kiikolojia ni wito wa toba na wongofu wa ndani na binadamu kuishi wito wao wa kuwa ni walinzi wa kazi ya uumbaji na kwamba, huu ni wajibu wa lazima katika maisha ya fadhila na kwamba, hili si suala la hiari katika mang’amuzi au maisha ya Kikristo. Rej. Laudato si, 217. Waamini kutoka mapokeo mengi wanaelewa kwamba, uumbaji ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya uhai na hivyo lazima uheshimiwe. Kumbe, imani ya kidini huimarisha hamu ya jumla ya kulinda uhai sanjari na kutunza asili. Baba Mtakatifu Leo XIV Katika Waraka wake wa Kwanza wa Kitume: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” anakazia kuhusu: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hatima ya uzalishaji, kanuni ya auni, mshikamano na haki jamii. Haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana na kwamba, ni chanzo cha mgogoro mkubwa wa kijamii na kiuchumi, changamoto ya kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote na kwamba, vipengele hivi ni muhimu wakati wa kufanya tathmini, kupanga na kutekeleza miradi ya utunzaji bora wa mazingira.

Jukwaa la majadiliano kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Jukwaa la majadiliano kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.   (AFP or licensors)

Jambo la pili anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV ni fadhila ya matumaini inayowaunganisha na kuwaambata watu wote na kwamba, watu wengi wanao ufahamu kuhusu amani inayotishiwa na ukosefu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, matumizi haramu ya rasilimali za dunia pamoja na kupungua kwa ubora wa maisha ya mwanadamu kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Changamoto hizi zinahitaji ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa, ili hatimaye kupata suluhu ya kudumu. Kumbe kuna haja ya kushinda woga na wasiwasi mintarafu woga wa kupoteza nguvu, wasiwasi wa mambo yajayo na hofu ya kufanya mabadiliko! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuvuka wasiwasi huu kwa kujikita Katika fadhila ya matumaini, ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mkutano wa thelathini wa Mkataba wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC COP30) ulifanyika jijini Bélem, nchini Brazil kuanzia Novemba 3 hadi Novemba 20, 2025. Lengo lake kuu lilikuwa kushughulikia ongezeko la gesi joto duniani na kuweka: sera na mikakati thabiti ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Utunzaji wa mazingira: Imani, matumaini na mapendo
Utunzaji wa mazingira: Imani, matumaini na mapendo   (LISA LEUTNER)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika mchakato wa mabadiliko yote haya kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kutafuta faida kubwa na kwamba, mifumo ya uchumi ikite mizizi yake katika mshikamano, utu na heshima ya binadamu pamoja na utekelezaji wa malengo ambayo yamewekwa na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuzisaidia nchi maskini duniani ziweze kusimama kidete kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, maendeleo fungamani ya binadamu yakite mizizi yake katika binadamu kwa kuthamini utu na heshima yao. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahimiza viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kukuza na kudumisha utamaduni wa upendo kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Papa Francisko anasema, huu ni upendo wa kiraia na kisiasa, kiini cha maendeleo ya kweli na kwamba, upendo huu unamwilishwa katika maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Upendo wa kijamii ni ufunguo wa kuyaelekea maendeleo ya kweli, kwa kukazia utu na heshima ya binadamu. Kumbe, upendo unaojali utasaidia kukoleza ustaarabu wa upendo. Kumbe, sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote haina budi kukita mizizi yake katika imani, matumaini na mapendo; kwa kuendeleza majadiliano, ili hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa iweze kupata suluhu ya kudumu, ili kutunza zawadi ya kazi ya uumbaji.

Papa Leo XIV Mazingira
16 Juni 2026, 15:55