Papa Leo XIV: Umuhimu wa Majadiliano ya Kidini: Huduma ya Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kwa takribani miaka 100, Shirikisho la Umoja wa Wayahudi kutoka New York “Delegation of the United Jewish Appeal, Federation of New York” Shirikisho la UJA limekuwa nguvu kuu ya mipango ya Jumuiya ya Wayahudi wa New York, nchini Marekani. Kupitia Shirikisho, la UJA karibu wafadhili 50,000 hukusanya rasilimali fedha, mali na vitu ili kuwasaidia watu wenye shida, kuhamasisha shauku ya maisha ya Kiyahudi, kujifunza, na kuimarisha jumuiya za Kiyahudi sehemu mbalimbali duniani. Shirikisho hili hushughulikia masuala mbalimbali ya waamini wa dini ya Kiyahudi na watu wanaoishi katika Jiji kubwa kama New York. Shirikisho hili linaunganisha Mashirika zaidi ya 100 na hivyo kuwafaidia: Watu, Masinagogi pamoja na mashirika mengine ya Kiyahudi kuanzia Jijini New York, pamoja na nchini nyingine 70 sehemu mbalimbali za dunia na hivyo kuwafikia watu zaidi ya milioni 4.5 kila mwaka, huu ndio uzuri wa kufanya kazi kwa ushirika na umoja. Shirikisho hili linawafaidisha maskini, wakimbizi na wahamiaji, wazee na walemavu. Huu ni utambuzi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu; mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, wito na mwaliko wa kuwajali na kuwapenda jirani.
Hija ya pamoja katika majadiliano ya kidini ni muhimu sana kwa ajili ya: Ustawi, maendeleo na mafao ya waamini wa dini hizi mbili, ili kufahamiana, kuheshimiana na kwa pamoja, kuweza kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu! Huu ni mchakato wa ujenzi wa fadhila ya upendo wa kidugu kati ya watu kwani Mungu ni asili na hitimisho la upendo. Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano na waamini wa dini mbalimbali duniani, “Nostra aetate” ni msingi wa mahusiano mema ambayo yameendelea kujengeka na kuimarika kama ndugu wamoja kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Urithi mkubwa ambao waamini wa dini mbalimbali wanaweza kuufanya katika maisha na utume wao ni kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya upendo kwa Mungu na jirani. Kizazi baada ya kizazi kinapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anapaswa kupendwa kwa moyo wote, kwa roho yote na kwa nguvu zote. Upendo huu kimsingi, unapaswa pia kuelekezwa kwa jirani ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Kanisa linakiri kwamba, kumekuwepo na mafanikio makubwa yanayofumbata amana na utajiri wa maisha ya kiroho; uelewa na udugu wa kibinadamu unaopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya chuki na uhasama kwa Wayahudi; kwa kujikita katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya amani, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatatu, tarehe 15 Juni 2026 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Umoja wa Wayahudi kutoka New York: “Delegation of the United Jewish Appeal, Federation of New York.” Wakristo na Wayahudi wanapaswa kutambuana kwamba, wao ni ndugu wamoja na kwamba, asili yao ni Mababu wa imani: Ibrahimu, Isaak na Yakobo na kwamba, mbegu ya ushirikiano na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini hizi mbili imeanza kuzaa matunda ya: Uelewano, urafiki, ushirikiano na amani. Dini zote mbili zinatambua na kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa likisukumwa na upendo wa Kiinjili linashutumu chuki, udhalimu na ukatili dhidi ya Wayahudi “Antisemitismus” wakati wowote na yeyote yule. Rej. NA 4-5.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika Ulimwengu ambao umegawanyika kutokana na vita, chuki na uhasama kuna haja ya kuchuchumilia ya mbeleni kwa kujenga na kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Sanjari na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waamini wa dini hizi mbili waendelee kujipambanua katika huduma kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii, kama njia na madaraja ya watu kukutana na hivyo kuendelea kung’ara katika huduma inayofunua mengi yaliyofichika katika sakafu ya moyo wa mwanadamu na hivyo kupyaisha tena jamii. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, mkutano huu utaendelea kumwilisha majadiliano, uelewano wa kina; haki na amani inayohitajika katika Ulimwengu mamboleo.
