2026.06.25 Wajumbe wa "Chama cha Vyuo na Vyuo Vikuu vya Kijesuit" 2026.06.25 Wajumbe wa "Chama cha Vyuo na Vyuo Vikuu vya Kijesuit"  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV:Vyuo vikuu vinaweza kushukulikia matokeo hasi na chanya ya AI

Papa Leo XIV akikutana na Marais wa vyuo na vyuo vikuu vya Kijesuit vya Amerika Kaskazini alisema,Vyuo Vikuu ni njia zenye nguvu za kukuza mshikamano na manufaa ya wote na kwamba vyuo vikuu vinaweza kuwa nafasi nzuri za kukabiliana na masuala yanayoikabili jamii,kama vile kushughulikia mahitaji ya watu waliotengwa na kutafakari athari za akili unde.“Taasisi za Kijesuit zinaitwa pia kutoa fursa kwa wahamiaji,wakimbizi na wenye uhitaji kijamii."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV akikutana mjini Vatican na marais na wawakilishi wa vyuo na vyuo vikuu vya Kijesuit huko Amerika Kaskazini Alhamisi, tarehe 25 Juni 2026 alisema kuwa "Kwa kuhamasisha utafutaji wa ukweli, kuwa karibu na wale waliotengwa na vijana, na kufanya kazi ya kulinda mazingira, vyuo vikuu vinakuwa nafasi muhimu za kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanadamu leo.  Papa Leo XIV alisema kwamba “Taasisi zenu hazijaitwa kuwafundisha wanafunzi wenu kuhusu dhuluma zinazowakabili wale walio pembezoni mwa jamii tu, bali pia kuwa njia zenye nguvu katika kukuza mabadiliko ya kimfumo kupitia kupendekeza mifumo mipya yenye mizizi katika mshikamano na manufaa ya wote."

Wakuu wa vyuo na vyuo vikuu vya kijesuit vya Amerika Kaskazini
Wakuu wa vyuo na vyuo vikuu vya kijesuit vya Amerika Kaskazini   (@Vatican Media)

Kuonesha Njia ya Mungu katika kutembea na waliotengwa

Katika hotuba yake, Papa Leo XIV alitoa ramani ya jinsi taasisi hizi zinavyoweza kuwasaidia wanachama wao kukabiliana na masuala muhimu zaidi ya jamii. Papa alipata msukumo kutoka kwa Mapendeleo manne ya Kitume ya Wajesuit: mada zilizoanzishwa mwaka 2019 na zinalenga kuongoza kazi ya Jumuiya ya Yesu kwa miaka 10 ijayo. Mapendeleo ni: kuonesha njia ya Mungu, kutembea na waliotengwa, kusafiri na vijana, na kutunza nyumba yetu ya pamoja. Papa Leo XIV alianza hotuba yake kwa kuakisi "changamoto nyingi zinazowakabili wanadamu leo" katika wakati ambao "umeitwa enzi ya mabadiliko ya kihistoria." Alisisitiza kwamba jamii zinazidi kuwa za kidunia, "huku wengi wakitafuta kusukuma kutajwa kwa Mungu katika umma na zaidi ya utamaduni maarufu," au jinsi mifumo ya kisiasa isivyoshughulikia "kilio cha maskini, wahamiaji, na wale ambao ulimwengu unawaona kuwa wametengwa."

Papa alisisitiza kwamba vijana mara nyingi hawana matumaini ya mustakabali bora na kwamba rasilimali za sayari zinatumika mara kwa mara kwa maslahi binafsi. Pia alibainisha athari inayoongezeka ya akili unde kwa binadamu. Katika suala hilo alibainisha kuwa Mapendeleo manne ya Utume wa Wajesuiti yanaweza kusaidia kushughulikia masuala haya. Kuhusu mada inayoendana na maskini, Papa alisisitiza jinsi hii ilivyo muhimu sana "katika wakati ambapo idadi kubwa ya kaka na dada zetu wanaishi katika umaskini." Alisema watu wengi wanalazimika kuondoka majumbani mwao kutokana na vita, mateso ya kidini au kisiasa, njaa, au mabadiliko ya tabianchi. Papa alisisitiza kwamba taasisi za elimu ya juu za Wajesuit hazijaitwa kukuza wema na mshikamano wa pamoja tu, bali pia "kutoa fursa kwa wahamiaji, wakimbizi, na wale walio na hali ya chini ya kiuchumi na kijamii ili kupata faida ya elimu ya juu."

Wajumbe kutoka vyuo na vyuo vikuu vya Kijesuit, Amerika Kusini
Wajumbe kutoka vyuo na vyuo vikuu vya Kijesuit, Amerika Kusini   (@VATICAN MEDIA)

Akili unde: Vyuo vichukue jukumu na kusindikiza vijana

"Kwa njia hiyo, Papa Leo XIV aliongeza kuwa, wataweza kujumuika kikamilifu zaidi katika jamii wanamoishi na pia kutajirisha mihimili mipana ya wanafunzi kwa uzoefu na mitazamo yao mbalimbali." Ingawa si mada maalum katika Mapendeleo ya Wajesuit, Papa Leo XIV pia alizungumzia kuhusu athari za akili Unde, akibainisha kuwa vyuo na vyuo vikuu vinaweza kuchukua jukumu maalum katika kushughulikia matokeo hasi na chanya ya maendeleo haya ya kiteknolojia. Taasisi hizi zinaweza hasa kutoa "msukumo mpya kwa kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa" kwa njia ambayo itakuwa muhimu na yenye ufanisi katika kushughulikia mapinduzi ya kidijitali.

Kuhusu mada ya kusindikiza vijana, Papa alisisitiza kwamba vyuo na vyuo vikuu ni sehemu za asili za kutoa matumaini katika mustakabali bora. Alisema wanafunzi, mara nyingi huanza kazi zao za kitaaluma zilizojaa mawazo na nguvu na, kupitia masomo yao na mahusiano, hupata hisia mpya ya matumaini katika kubadilisha ulimwengu kuwa bora. "Ninawaalika muendelee kukuza hisia hiyo ya matumaini miongoni mwa wale walio katika jamii zenu kupitia fursa za mazungumzo, huduma, na maombi, mkikumbuka kila wakati kwamba ufufuko wa Kristo ndio chanzo kikuu cha matumaini na kwamba pamoja naye mambo yote yanawezekana," Papa Leo XIV alisisitiza.

Wakuu wa vyuo vikuu vya Kijesuit
Wakuu wa vyuo vikuu vya Kijesuit   (@Vatican Media)

Wale wanaofanya utafiti hatimaye wanamtafuta Mungu

Akigeukia mada ya kutunza uumbaji, Papa Leo XIV aliwahimiza taasisi zinazoendeshwa naWajesuit "kufundisha kwa mfano, na si kwa nadharia tu," hasa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na "unyonyaji wa rasilimali na wachache kwa gharama ya manufaa ya wote." "Ninawahimiza mvumilie na juhudi zenu za kuwaelimisha wale walio katika vyuo vyenu kuhusu hatari hizi za sasa, lakini pia kuziacha jamii zenu ziwe mifano ya uendelevu wa ikolojia, urahisi, na shukrani kwa zawadi za Mungu," alisema. Kuhusu mada inayoonesha njia ya Mungu, Papa alibainisha kwamba "wale wanaofanya utafiti, wale wanaofuatilia masomo, na wale wanaotafuta ukweli hatimaye wanamtafuta Mungu, iwe wanatambua au la."

Kumjua aliye wa kweli

Papa alisisitiza umuhimu wa kuunda jumuiya za kitaaluma ambapo wanachama wanaweza kumjua "Yule aliye Kweli," na kujibu njaa inayoongezeka ya Mungu miongoni mwa vijana. Katika suala hilo Papa aliwasihi Wajesuit kuhimiza ushiriki mpana katika Mazoezi ya Kiroho, kwani yanaweza pia kusaidia kutoa utambuzi juu ya maamuzi muhimu. Papa alihitimisha hotuba yake kwa kuita Jumuiya ya Yesu kwa msaada wa mwanzilishi wao Mtakatifu Ignatius wa Loyola "kuendeleza utamaduni wa Wajesuit" wa kuwaunda wale waliokabidhiwa uangalizi wao "kuwa 'wanaume na wanawake kwa wengine.'

PAPA LEO: VYUO VIKUU KUSHUGHULIKIA AI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

25 Juni 2026, 16:31