Papa Leo XIV Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume: Umoja wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, katika Sherehe ya Watakatifu Petro aliyeteuliwa na Kristo Yesu kuwa Mchungaji mkuu wa Kondoo wake na Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa; wote wawili ni Miamba wa imani ya Kanisa, Jumatatu tarehe 29 Juni 2026, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, akabariki Pallio Takatifu na kuwavisha Maaskofu wakuu wapya 35 walioteuliwa katika kipindi cha Mwaka 2025-2026. Kati yao kuna Maaskofu wakuu wanne kutoka Barani Afrika nao ni: Askofu mkuu Sithembele SIPUKA: Jimbo kuu la Cape Town (Afrika ya Kusini); Askofu mkuu François SYLLA, Jimbo kuu la Conakry (Guinea); Askofu mkuu Isaac Jogues Kodjo Agbéménya GAGLO Jimbo kuu la Lomé (Togo) na hatimaye ni Askofu mkuu Dennis Kofi AGBENYADZI, S.M.A, Jimbo kuu la Berbérati (Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.)
Pallio takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa na manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa mabegani na Baba Mtakatifu, Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki wanapokuwa katika majimbo yao pamoja na Mapatriaki kutoka Kanisa la Mashariki. Na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na Shahidi, aliyeuwawa kunako karne ya tatu; akaonesha upendo wa pekee sana kwa Kristo Yesu mchumba wake wa daima, kiasi cha kuyasadaka maisha yake, ili asiuchafue ubikira wake. Yesu mwenyewe alitambulishwa na Yohane Mbatizaji kama Mwana Kondoo wa Mungu anayebeba na kuondoa dhambi za ulimwengu. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, katika Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu, wanazovishwa Maaskofu wakuu katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata Maaskofu wakuu wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; daima wakikumbuka kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mastahili na mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya kondoo wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa sasa katika nafsi ya Baba Mtakatifu Leo XIV. Baada ya mabadiliko yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015, tangu wakati huo, Maaskofu wakuu wapya wamekuwa wakivishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican majimboni mwao, ili kuwashirikisha watu wa Mungu kutoka katika majimbo yanayounda Jimbo kuu husika tukio hili adhimu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Lakini, Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Dominika tarehe 29 Juni 2025 alirejesha tena katika Mapokeo ya Mama Kanisa ya kuwavisha Pallio Takatifu Maaskofu wakuu na Mapatriaki wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake ametaja sifa kuu na udhaifu wa watakatifu Petro na Paulo katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto na mwaliko kwa wakristo kuwa ni wajenzi wa umoja wa Kanisa, huku upendo wa Mungu na jirani zao ukipewa kipaumbele cha kwanza, kama njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa Pallio Takatifu waamini pia wawe tayari kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu kuubeba Msalaba ambao mwili na ulimwengu “Caro et mundus” huwatwisha mebegani mwao wote watafutao haki na amani. Wanahimizwa na Mama Kanisa kusadaka nguvu, muda, mateso na hata maisha yao, ili Injili iweze kuwafikia watu wote na ndani mwake waweze kupata amani na utulivu. Ametambua uwepo wa ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ukiongozwa na Askofu mkuu Emmanuel Adamakis wa Jimbo kuu la Calcedonia.
Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Mtakatifu Petro katika Maandiko Matakatifu anajulikana kama mlinzi wa watu wa Mungu aliyepewa dhamana na wajibu wa kujenga na kuimarisha umoja; imani na matumaini hata pale kwa macho ya kibinadamu, mambo yalikuwa hayawezekani, lakini kwa Neno la Kristo Yesu aliweza kushuhusha nyavu zake na kupata samaki wengi. Rej. Lk 5:5. Hata pale Kristo Yesu katika mafundisho yake, kwamba Yeye ndiye chakula cha uzima kilichoshuka kutoka mbinguni, wengi wa wafuasi wake wakakwazika na kurejea nyuma kwa sababu hawakuamini, lakini Simoni Petro, akamwambia Kristo Yesu kwamba, Yeye anayo maneno ya uzima, wamesadiki na kujua ya kwamba Kristo Yesu ndiye Mtakatifu wa Mungu. Rej. Yn 6: 22-71. Ni Mtakatifu Petro ambaye kwa niaba ya Mitume wengine alimtambua Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu. Rej Mt 16:13-19. Hata baada ya mateso, kifo na ufufuko wake, alimtambua Kristo Mfufuka na kuonja upendo wake wa dhati uliomstahilisha kupewa Mamlaka katika maisha na utume wake. Hata pale kulipotokea malumbano ya kiimani, Mtakatifu Petro alibaki kuwa ni mwaminifu kwa kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hata Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake, alionesha udhaifu mkubwa, itakubukwa kwamba, wakati wa mateso ya Kristo Yesu, Petro alimkana mara tatu, akajuta kwa kilio kikuu na machozi mengi. Rej. Lk 22:54-62. Ni kiongozi aliyetambua na kukiri udhaifu wake wa kibinadamu, ili hatimaye aweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kuwakusanya kondoo wa Kristo Yesu, hata mauti ilipomfika, kwa kifo dini hapa Roma, akawa ni kielelezo cha umoja na maadili ya Kanisa, mahali ambapo ukweli unatangazwa na kushuhudiwa na hivyo unakuwa ni chombo na chachu ya ukuaji wa wengine. Huu ni mwaliko kwa waamini kumsikiliza Mtakatifu Petro, ili wote chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu, waweze kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa umoja wa Kanisa, changamoto na mwaliko kwa wakristo kuwa ni wajenzi wa umoja wa Kanisa, huku upendo wa Mungu na jirani zao ukipewa kipaumbele cha kwanza, kama njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Rej. 2Tim 4:17.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa, alikuwa ni mtangazaji mwaminifu na asiyechoka kwa Habari Njema ya Wokovu na kwamba, katika maisha na utume wake alibahatika kupewa alama mbili zinazounganika kati yao, yaani Kitabu na Upanga akisema “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.” Ebr 4:12-13. Mwenyezi Mungu katika upendo na huruma yake, alimwita Mtakatifu Paulo katika ujana wake, akamwongoa, akamtuma kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, na hatimaye, akayamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa kwa nguvu ya Neno la Mungu, aliweza kumwokoa kutoka katika kulidhulumu Kanisa hadi kumfikisha katika Njia ya upendo. Kwa hakika alilitesa na kulidhulumu Kanisa la Kristo Yesu. Lakini neema na huruma ya Mungu vikamwongoa na hivyo kuwa kweli mjumbe wa amani na mhudumu wa huruma na msamaha wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa wabatizwa wote kuwa kweli ni vyombo, wajenzi na mashuhuda wa umoja wa Kanisa na wahudumu wa ukweli unaofumbwa katika Injili ya upendo.
Na kwa alama ya Pallio takatifu ambacho ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa na manyoya ya kondoo wachanga, kama ilivyo kwa Maaskofu wakuu, hata waamini wanahimizwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, waamini pia wanakuwa tayari kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu kuubeba Msalaba ambao mwili na ulimwengu “Caro et mundus” huwatwisha mebegani mwao wote watafutao haki na amani. Wanahimizwa na Mama Kanisa kusadaka nguvu, muda, mateso na hata maisha yao, ili Injili iweze kuwafikia watu wote na ndani mwake waweze kupata amani na utulivu. Rej. Gaudium et spes, 38. Baba Mtakatifu Leo XIV ametambua uwepo wa ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ukiongozwa na Askofu mkuu Emmanuel Adamakis wa Jimbo kuu la Calcedonia.
Itakumbukwa kwamba, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo ni Siku maalum ambayo imetengwa na Mama Kanisa ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika nafsi ya Papa Leo XIV kwa kuchangia kwa hali na mali ili kusaidia utekelezaji wa Injili ya huduma ya upendo, huruma na ukarimu inayomwilishwa katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mchango huu unalenga kufanikisha jitihada za huruma ya Mungu ambazo kimsingi zinafumbatwa katika Sakramenti za Kanisa na kumwilishwa katika huduma ya ukarimu na upendo kwa watu wanaosiginwa, utu, heshima na haki zao msingi kutokana na umaskini, ujinga na maradhi; kwa wakimbizi na wahamiaji; kwa watu wanaokumbwa na majanga pamoja na maafa mbalimbali kwa sasa. Mchango huu unamwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kuwa ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kwa mwaka huu 2026 siku hii imeadhimishwa Dominika tarehe 28 Juni 2026. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika waamini kuwaomba watakatifu Petro na Paulo, waendelee kuwaimarisha katika hija ya ujenzi wa umoja kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu Mkombozi wa Dunia. Hii ndiyo njia ambayo Kristo Yesu amewafundisha waja wake katika ile Sala yake ya Kikuhani, ili wawe wamoja na watu wa matumaini. Rej. Yn 17: 21-23.
