Tarehe 30 Mei 2026 Njia ya Ukatekumeni Mpya imeadhimisha Kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwake. Tarehe 30 Mei 2026 Njia ya Ukatekumeni Mpya imeadhimisha Kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.   (© Tomasz Marynowski.)

Papa Leo XIV: Miaka 60 ya Jumuiya ya Ukatekumeni Mpya: Neno, Liturujia, Sala na Jumuiya

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anawakumbusha waamini kwamba, dhamana na utume wa Kanisa ni kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ni utume unaotekelezwa kwa furaha kubwa na kwa njia ya unyenyekevu; sanjari na kuendeleza ujenzi wa umoja wa Wakristo, daima wakiwa chini ya maongozi na usimamizi wa Roho Mtakatifu: Muhimu: Neno, Liturujia, Sala na ujenzi wa Jumuiya

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, Jumuiya inayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo thabiti inakuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu, ari na mwamko mpya wa ujenzi wa Kanisa la kimisionari na kisinodi. Hii inatokana na ukweli kwamba, neema ya utume huu inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowakirimia waamini ari na nguvu ya kuwa kweli ni wamisionari tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini walei wanahamasishwa kuwa ni wamisionari kwa watu wanaowazunguka kwa kuwasikiliza na kuwapatia huduma: kiroho na kimwili; kwani ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni chachu ya Uinjilishaji mpya inayokolezwa na Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ushuhuda wa Kanisa unafumbatwa katika huduma makini kwa maskini wa kiroho na kimwili. Mama Kanisa anawataka wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya, (Neocatecumenale) kuwasaidia na kuwaendeleza watoto wao katika maisha ya kiroho na utu wema, kwani wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa la Kristo! Wajitahidi kuwafunda ili hatimaye, waweze kuwa ni wakristo watakatifu na raia wema zaidi. Njia ya Ukatekumeni Mpya ilianzishwa kunako mwaka 1968 huko Madrid, nchini Hispania. Wanachama wake wa kwanza ni watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na umaskini pamoja na changamoto mbalimbali walizokumbana nazo katika maisha.

Kiko akajitosa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka
Kiko akajitosa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka   (@Vatican Media)

Bwana Francisco Josè Gomes Arguello Wirtz, maarufu kama “Kiko” akajitosa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka na kwa msaada wa Roho Mtakatifu akaanzisha Njia ya Ukatekumeni Mpya, mchakato wa maisha ya wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Bwana Francisco Josè Gomes Arguello katika safari ya maisha yake, alitikiswa sana, hatimaye, akagundua mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto iliyomfanya kuacha yote na kuanza kuandamana na maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Hayati Mama Carmen Hernàndez, mtaalam wa masuala ya kemikali kutoka Hispania, aligundua upya wa maisha uliokuwa unabubujika kutoka katika Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Umaskini, Taalimungu na Ushuhuda wa Kerigima ya Katekesi yakawa ni mambo msingi yaliyotoa dira na mwongozo wa maisha na utume wa Njia ya Ukatekumeni Mpya, ulioanza kuenea kwa kasi kubwa nchini Hispania na baadaye sehemu mbali mbali za dunia. Mama Carmen Hernàndez akafariki dunia tarehe 19 Julai 2016 baada ya juhudi kubwa ya kupandikiza Neno la Mungu katika nyoyo na akili za watu!

Njia ya Ukatekumeni Mpya: Neno la Mungu, Liturujia na Maisha ya Kijumuiya
Njia ya Ukatekumeni Mpya: Neno la Mungu, Liturujia na Maisha ya Kijumuiya   (@Vatican Media)

Njia ya Ukatekumeni Mpya ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto iliyotolewa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Paulo VI, akiwataka wanachama hawa kukita maisha yao katika ukweli wa maisha ya Kikristo, chemchemi ya furaha, matumaini na ushuhuda unaotolewa na wanachama hawa. Wakristo wanaofuata Njia ya Ukatekumeni Mpya wanapaswa kwa namna ya pekee kabisa anasema Mtakatifu Paulo VI kujikita katika ukweli, uhalisia na utimilifu wa maisha ya Kikristo, chimbuko la chemchemi ya ushuhuda wa furaha na matumaini kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha na utume wao. Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, akawatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu wa kimisionari, akiwataka pia kulea na kukuza miito ya kimisionari. Mtakatifu Yohane Paulo II akatambua na kuandika kwamba, asili ya chama hiki cha kitume cha Njia ya Ukatekumeni Mpya ni mwendelezo wa mchakato wa majiundo makini ya kikatoliki, muhimu sana kwa watu wa Mungu kwa nyakati hizi. Mtakatifu Yohane Paulo II akawataka Maaskofu kuthamini mchango na huduma iliyokuwa inatolewa na wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Njia ya Ukatekumeni Mpya ni chemchemi ya miito mitakatifu
Njia ya Ukatekumeni Mpya ni chemchemi ya miito mitakatifu   (© Tomasz Marynowski.)

Njia ya Ukatekumeni Mpya inapata chimbuko lake katika Neno la Mungu, Liturujia ya Kanisa na Maisha ya Kijumuiya yanayosaidia kurutubisha na kujenga udugu wa kibinadamu na ukomavu wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, imani ambayo inapaswa kumwilishwa katika Injili ya huduma ya upendo. Huu ni mchango wa tajiriba na mang’amuzi ya maisha na utume wa Kanisa, changamoto iliyoibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ikapokelewa kwa moyo wa shukrani na unyenyekevu mkuu na Askofu mkuu Casimiro Morcillo wa Jimbo kuu la Madrid kwa wakati ule na hatimaye, kama moshi wa ubani, Njia ya Ukatekumeni Mpya ikaenea pole pole na harufu yake kuijaza Hispania hadi kufikia “miisho ya dunia.” Mtakatifu Yohane Pualo wa Pili, kunako mwaka 1986 akabahatika kuona matunda ya kuanzishwa kwa Seminari ya kwanza ya “Redemptoris Mater” lakini kabla ya hapo, mwaka 1984 na mwaka 1986, bahari ya vijana kutoka katika Njia ya Ukatekumeni Mpya wakafurika mjini Vatican kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Vijana Duniani na Jubilei ya Vijana na huo ukawa ni moto wa kuotea mbali.

Katekesi endelevu ni muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa
Katekesi endelevu ni muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Njia ya Ukatekumeni Mpya ikawa ni chemchemi ya miito mitakatifu, vijana wengi wakaamua kufunga ndoa, ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; baadhi ya wao wakajiunga na wito wa kipadre na kitawa, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, watangazaji mahiri wa Neno la Mungu na wagawaji wa Mafumbo ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II akaanzisha mchakato wa kuandika Katiba ya Njia ya Ukatekumeni Mpya iliyopitishwa na kuridhiwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kunako mwaka 2008. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kunako mwaka 2010 likapitisha na kuidhinisha Mwongozo wa Katekesi ya Njia ya Ukatekumeni Mpya. Mwaka 2026 Njia ya Ukatekumeni Mpya imeenea katika nchi 138 Ulimwenguni kote, kuna Parokia 6,250 katika Majimbo 1,400 Tarehe 30 Mei 2026 Njia ya Ukatekumeni Mpya imeadhimisha Kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwake. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake ulioandikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kusomwa baada ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Madrid, Hispania na Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anawakumbusha waamini kwamba, dhamana na utume wa Kanisa ni kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ni utume unaotekelezwa kwa furaha kubwa na kwa njia ya unyenyekevu; sanjari na kuendeleza ujenzi wa umoja wa Wakristo, daima wakiwa chini ya maongozi na usimamizi wa Roho Mtakatifu, ili wokovu ambao ni zawadi ya Mungu, iweze kuwafikia watu wote, ni katika muktadha huu, anasema Baba Mtakatifu waamini wabatizwa wanapaswa kutekeleza wajibu huu kwa ari na moyo mkuu.

Njia ya Ukatekumeni mpya ni chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa
Njia ya Ukatekumeni mpya ni chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Maandalizi ya kupokea Sakramenti za Kanisa yanapaswa kueleweka katika mtazamo mpana zaidi, kwani ni katika “tumbo hili”, Jumuiya ya waamini inazaliwa katika imani na kuanza kutembea katika maisha na Fumbo la Pasaka, kwa kujenga na kudumisha ushirika na Kristo Yesu pamoja na Jumuiya ya waamini. Katika kipindi cha Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Njia ya Ukatekumeni Mpya, watu wa Mungu wamemtambua kuwa ni: Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo ambaye amejifunua kwa njia ya Sheria, kielelezo cha utambulisho, dira na mwongozo wa watu wa Mungu. Mwenyezi Mungu amejifunua kwa njia ya Manabii wake watakatifu, waliotumwa kutangaza na kushuhudia uwepo wake endelevu katika hija ya maisha ya waja wake. Hatimaye, Mwenyezi Mungu katika nyakati hizi amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma na upendo wa Baba wa milele. Huyu ndiye Neno aliyekuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu; ni Mungu mwaminifu na mwingi wa huruma anasema, Kardinali José Cobo Cano, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania, katika mahubiri yake, kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Njia ya Ukatekumeni Mpya.

Kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuanzishwa Njia ya Ukatekumeni Mpya
Kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuanzishwa Njia ya Ukatekumeni Mpya   (@Vatican Media)

Huu ni mwaliko kwa waamini kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Makanisa mahalia, kwa kujenga na kudumisha umoja wa Kikanisa sanjari na kukuza uhuru wa kila mwamini, chemchemi ya utakatifu wa maisha kama ilivyo kwa Hayati Mama Carmen Hernàndez, mtaalam wa masuala ya kemikali kutoka Hispania, ambaye mchakato wake wa kutangazwa kuwa Mwenyeheri umehitimishwa, Jumanne tarehe 2 Juni 2026. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kwa njia ya maisha na utume wa Kanisa la Kihispania, amewezesha watu wengi kufanya upyaisho wa maisha yao kwa njia ya watakatifu, mashuhuda na wafiadini. Hii ni historia inayobeba mchakato wa toba na wongofu wa ndani, chemchemi ya maisha na miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Hili ni jeshi kubwa linaloundwa na Makatekista, Mapadre na Majandokasisi walioenea sehemu mbalimbali za dunia. Muhimu ni kuendeleza majiundo makini mara baada ya kupokea Sakramenti za Kanisa, kwa kujikita katika Katekesi endelevu, maisha ya sala na hija mbalimbali ili waamini waendelee kukua na kukomaa katika maisha na utume wao!

Njia ya Ukatekumeni mpya 2026
02 Juni 2026, 17:33