Papa Leo XIV:Tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwa Mt.Franciska Cabrini!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kama Mama Franciska angekuwa hai leo hii, roho yake ya kimisionari ingemwambia nini? Au tuseme, Moyo wa Kristo ungemwambia nini kama mwanamke aliyewekwa wakfu Kwake na kwa utumishi wa Ufalme Wake? Na Papa kama Francisko, mwana wa wahamiaji wa Italia, angemwomba nini? Ni maswali yaliyomo ndani ya tafakari ya Papa Leo XIV wakati kuabudu na kuheshimu mabaki ya moyo wa Mtakatifu Franciska Xavier Cabrini katika Kanisa Kuu lililopewa jina lake huko Sant'Angelo Lodigiano, Jumamosi tarehe 20 Juni 2026 katika ziara ya Kichungaji huko Pavia na Sant'Angelo Lodigiano.
Papa Leo XIV alikazia kusema kuwa ujumbe unao faa wa Mtakatifu mlinzi wa wahamiaji, ulifika kila mahali, kuanzia makazi duni hadi magereza. Aliwahimiza vijana kujifunza kuhusu maadili ya mwanamke wa kwanza aliyetangazwa kuwa Mtakatifu nchini Marekani, akinukuu maandishi yake kuwa: "Hakuna nchi iliyo mbali sana, hakuna mtu aliyejeruhiwa sana kwa upendo wa Moyo wa Yesu."
Papa Leo XIV akianza tafakari yake alisema “Ninafurahi kuwasalimu nyote, raia wenzangu na wapenzi wa Mtakatifu Francisk Xavier Cabrini! Ninamshukuru Askofu Maurizio Malvestiti, Padre wa parokia, meya, na mamlaka nyingine za kiraia. Niko hapa kutoa heshima kwa Mama Cabrini, mlinzi wa wahamiaji, mtakatifu wa kwanza wa Marekani, aliyezaliwa hapa, huko San' Angelo Lodigiano, mwaka 1850, na akafa huko Chicago, mji wangu wa asili, mwaka 1917. Nilipogundua kwamba Sant' Angelo Lodigiano iko kilomita chache tu kutoka Pavia, mara moja nilifikiri ningetumia fursa hiyo... Nami niko hapa.” Watu walipiga makofi, na akawashukuru hata kwa makaribisho ya joto!
Mama Cabrini alitambua kutafsiri ishara za nyakati
Kwa hivyo Papa aliendelea kusema kuwa "Mnanionesha upendo wa Kanisa la Lodigiano na kwa Papa, upendo ambao Mama Cabrini aliukuza kwa kujitolea na utii wa pekee. Hakika, wakati ulipofika wa kufanya uamuzi muhimu kuhusu "njia" ya utume wa taasisi yake ya kitawa. Na Leo XIII alikuwa wazi: "Sio Mashariki, bali Magharibi," kuwahudumia maelfu ya wahamiaji wa Italia huko Amerika, kama Askofu wa Piacenza, Mtakatifu Yohane Mbatizaji Scalabrini, alivyokuwa tayari amemshauri. Kupitia sauti za wachungaji hawa wawili walioelimika, Mama Cabrini alitafsiri ishara za nyakati na kuelewa kwamba ndoto ya kwenda China, kuiga Mtakatifu Francis Xavier, ilibidi itimizwe ambapo, wakati huo, hitaji lilikuwa kubwa zaidi. “Lakini, tukiangalia ulimwengu wa leo, tuseme nini? "Ishara" hiyo, yaani, jambo la uhamiaji, imeingia katika awamu tofauti, hakika ni ngumu zaidi, lakini pia ina uwezo wa kulichangamotisha Kanisa.”
Tujiulize: kama Mama Franciska angekuwa hai leo hii, roho yake ya kimisionari ingemwambia nini? Au tuseme, Moyo wa Kristo ungemwambia nini kama mwanamke aliyewekwa wakfu Kwake na kwa utumishi wa Ufalme Wake? Na Papa kama Francisko, mwana wa wahamiaji wa Italia, angemwomba nini? Amefanya huduma kwa wahamiaji kuwa kipengele muhimu cha upapa wake.” Baba Mtakatifu Leo XIV akiendelea alisema kuwa , Papa Francisko alitaka Waraka wake wa Tatu, Dilexit nos, “Alitupenda” ambao ukawa wa mwisho kwake, utolewe kwa "upendo wa kibinadamu na wa kimungu wa Moyo wa Kristo," yaani, kwa fumbo hilo la upendo usio na kikomo ambalo ndilo "nguvu pekee ya kweli" ya maisha ya Mtakatifu Cabrini, ya yote aliyoyatimiza, na, zaidi ya hayo, jinsi alivyoyatimiza.
Katika Waraka wake huo Papa Francisko anaandika: "Inafaa kujitolea kwa Moyo wa Kristo ambako kunaonekana waziwazi katika kazi ya uinjilishaji na elimu ya shule za kitawa za wanaume na wanawake, ambazo zimeainishwa kutoka asili yake na uzoefu huu wa kiroho wa Kristo" (n. 150). Papa Leo XIV alikiri kwamba “Kwa upande wangu, nimerithi na kuendeleza Majisterio ya Papa Francisko pamoja na Waraka wa Kitume Dilexi te, yaani ‘Nilikupenda’ kuhusu upendo kwa maskini, na ambapo upendo unaozungumziwa katika mfumo wa "wahamiaji wanaosindikizwa na," sura ya Mtakatifu Franciska Xavier Cabrini inaonekana, pamoja na Mtakatifu Yohane Mbatizaji Scalabrini.”
Moyo wa kimama
"Moyo wake wa kimama, ambao haukuwa na amani kamwe, uliwafikia kila mahali—wahamiaji—katika makazi duni, magerezani, katika migodi" (n. 74). Yeye mwenyewe aliandika: "Hakuna kazi itakayokuwa ngumu sana, hakuna nchi iliyo mbali sana, hakuna mtu aliyejeruhiwa sana na upendo wa Moyo wa Yesu na wale wote walioalikwa kuwa wabebaji wa upendo wa Kristo duniani." Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa “Kaka na dada, ni nini kilicho cha wakati zaidi kuliko karama hii? Nasema hapa, mbele ya mabaki ya moyo wa Mama Cabrini, yaliyoletwa kutoka Nyumba Mama huko Codogno.” Papa alisema hayo, huku akiwasalimu na kuwashukuru binti zake wa kiroho kwa upendo, Masista Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. “Ni nini kilicho cha wakati zaidi kuliko karama ya kimisionari inayojiweka katika huduma ya wahamiaji?”
Kwa vijana mjueni Mtakatifu Franciska Cabrini
Papa Leo XIV aliendelea kwamba Mtakatifu huyo aliwahimiza vijana kujifunza kuhusu maadili ya mwanamke wa kwanza aliyetangazwa kuwa Mtakatifu nchini Marekani: “Kwa hivyo nachukua fursa hii kuwasihi, hasa vijana: mjueni Mtakatifu Franciska Cabrini! Someni maandishi yake, yakiwa yamejaa shauku kwa Yesu na kwa utume; barua zake, shajara zake za usafiri, maelezo yake ya mafungo. Mtu yeyote anayemjua Mama Cabrini anavutiwa naye. Nafsi yake ilikuwa ya kutafakari na yenye shughuli nyingi; alizama katika upendo wa Moyo wa Kristo, na hii ilimpatia uwezo wa ajabu wa kufanya kazi na nguvu ya roho, sambamba na kauli mbiu ya Paulo aliyoichagua kwa ajili ya Taasisi: "Naweza kufanya mambo yote katika Yeye anitiaye nguvu." (Fil 4,13).
Wito kwa Kanisa Sant'Angelo Lodigiano
Papa Leo XIV alihimiza tena kwamba “Ninatoa wito huu hasa kwa Kanisa la Lodi, ambalo limenikaribisha leo kwa upendo mkubwa! Na ningependa kuelezea kama ombi: Kanisa la San Bassiano liwe tofauti kila wakati na sifa zinazong'aa katika binti yake huyu mtukufu zaidi. Kwa mfano wake na maombezi, Mtakatifu Cabrini awasaidie kumpenda Kristo, mashahidi wa Injili yake kwa roho ya bidii na ukarimu, katika kuwahudumia maskini zaidi. Awasaidie kuishi sinodi yenye ufanisi, mkitembea pamoja na kujitahidi kwa utakatifu, katika aina mbalimbali za karama na huduma. Kwa hili ninawahakikishia maombi yangu.” Hatimaye, Papa alimwomba “Bwana kwa ajili ya Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, katika kila jumuiya yao: Mungu awabariki na kuwafanya upya katika uaminifu kwa karama ya Mama Cabrini. “ Na hatimaye alisema” Na Kanisa zima limtazame mmisionari huyu wa ajabu wa Upendo, kujifunza maana ya kutumikia Ufalme wa Mungu katikati ya historia. Kwa moyo mkunjufu Papa alitoa baraka zake za kitume kwao na wapendwa wao na kuwashukuru.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here
