Papa Leo XIV: Kumbukizi ya Miaka 50 ya Skauti Barani Ulaya: Utu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Italia ya Viongozi wa Kikatoliki na Skauti wa Ulaya (pia inajulikana kama FSE au Scouts of Europe, FSE) ilianzishwa rasmi tarehe 14 Aprili 1976, mjini Roma. Jumuiya hii ilianzishwa na kikundi cha viongozi, walezi na waelimishaji ambao waliamua kujitenga na harakati ili kudumisha mbinu ya asili ya Skauti, kufuatia kuunganishwa kwa ASCI na AGI na kuunda AGESCI. Kumbe kwa mwaka huu 2026 Jumuiya hii inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Se piace a Dio, per sempre!” Yaani: "Mungu akipenda, milele!” Jubilei hii inaadhimishwa muda mfupi tu baada ya Mama Kanisa kuadhimisha Sherehe ya Pentekoste, yaani ni Siku ya hamsini baada ya: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Ni Sherehe ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Kanisa kwa njia ya Roho Mtakatifu yaani kuumbwa upya kwa Taifa jipya la Mungu. Siku ya Pentekoste ni kilele cha Sherehe ya Pasaka, kwa sababu utajiri wote uliofunuliwa na Yesu mfufuka unaanza kuonekana katika mioyo na maisha ya Mitume wa Yesu, kielelezo cha utimilifu wa ukombozi wa mwanadamu na ishara ya umoja. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatatu tarehe 1 Juni 2026 alipokutana na kuzungumza na Jumuiya ya Italia ya viongozi wa Kikatoliki na Skauti ya Ulaya.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Roho Mtakatifu anapowashukia Mitume anawasha moto wa maisha, anawafungulia wafuasi wa Kristo Yesu utume na umoja, kiasi cha kuelewana licha ya tofauti zao za lugha. Zawadi ya Kristo Mfufuka kwa waja wake ni kuwawezesha kutangaza na kushuhudia uzuri wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chemchemi ya Injili ya matumaini, inayowatia shime waamini kutenda vyema katika medani mbalimbali za maisha na utume wao; tayari kutangaza na kushuhudia uzuri wa kazi ya uumbaji, historia ya mwanadamu pamoja na changamoto zake. Huu ni mwaliko kwa wanajumuiya hawa kuchota amana na utajiri wa Maandiko Matakatifu katika tajiriba zao za ukuaji kiutu, katika maisha ya kiroho mintarafu ukuaji wa mtu binafsi na ule wa kijumuiya. Injili ya Kristo Yesu iwe ni dira na mwongozo wa maisha, wanayopaswa kuisoma na kuitafakari kila siku ya maisha yao.
Hii ni kwa sababu, Injili, Neno la Mungu ni Kristo Yesu mwenyewe, Habari Njema ya Wokovu; Ni Neno anayezima kiu na njaa ya haki na ukweli na hivyo kuwakirimia waja wake ujasiri wa kuendelea kudumu katika wema, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Kwa njia hii Jumuiya hii ya viongozi, inakuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa watoto na vijana waliodhaminishwa mbele ya uongozi wao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, mshikamano na ukomavu wao wa maisha machoni pa vijana na watoto ni mfano bora sana unaowasaidia kukua. Huu ni mwaliko wa kuandamana na vijana hawa, ili waweze kuonja na kung’amua uzuri wa imani katika ishara za kila siku na sala za pamoja; Katika maadhimisho mbalimbali ya Sakramenti za Kanisa; kwa kutambua na kuthamini wito wa kila mtu. Huu ni mwaliko wa kuitikia kwa ukarimu wito wa Kristo Yesu wa kupanda hadi kileleni kwa kutweka hadi kilindini katika huduma kwa watoto na vijana wa kizazi kipya; kwa kuendelea kutembea pamoja katika njia ya utu wema unaosimikwa katika kanuni maadili. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Mapadre na wahudumu wa maisha ya kiroho ni kielelezo na dhamana kati ya Mama Kanisa na Jumuiya yao, kwa kushirikisha huduma yao ya Kikuhani kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na watoto katika kutekeleza wajibu wa kazi ya elimu na ukuaji wa watoto na vijana kiroho. Viongozi hawa wanakumbushwa kwamba, mbinu ya Skauti ni kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, ili kukuza na kudumisha uhusiano, amana na utajiri wote wa kibinadamu; katika kuelimisha ili kuwapatia walengwa ufahamu maalum, ili kuweza kuwakutanisha wavulana na wasichana.
Lengo kuu la Chama cha Skauti ni kuwalea vijana na watoto ili waweze kuwa ni Wakristo na raia wema katika hatua mbalimbali za malezi na makuzi yao. Baba Mtakatifu Leo XIV anawapongeza kwa kuchagua kukuza na kudumisha mwelekeo wa Bara la Ulaya kiutamaduni ili kujenga Bara la Ulaya linalotoa kipaumbule cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; biashara inayosimikwa katika tunu msingi za kimaadili lakini zaidi ujenzi wa ubinadamu wa Kikristo! Ni katika muktadha huu, huduma inaunganishwa katika vipengele vyote vya mtindo wa Baden-Powel, yaani moyo wa falsafa yake ya elimu; kwa kuweka ujuzi kwa ajili ya mastahili ya wengine bila kutarajia malipo. Kwa njia ya ushuhuda wa imani, huduma huwaweka huru kutoka katika tabia ya utegemezi, hali ya kutojali na kufungwa katika uchoyo na hivyo kukuza na kudumisha hisia za uwajibikaji na huduma kwa kufanya hata mambo madogo madogo, vizuri zaidi hata kuweza kutunzana. Matukio ya uchunguzi wa kina yanabainisha na kuwasaidia wanadamu kugundua jinsi ambavyo ubinadamu unavyoangaziwa na kushughulikiwa na kazi ya Mungu, mwalimu wa kweli kwa watu wote. Baba Mtakatifu amewatia shime viongozi hawa kuendeleza shughuli za Chama chao kwa furaha na majitoleo makubwa na kwamba, anamwomba Roho Mtakatifu apende kuzidizisha na kuongeza karama zake kati ya viongozi hawa, ili wapate kunena kwa lugha ya upendo, maridhiano na amani. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewakabidhi viongozi hawa nchini ya ulinzi na maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.
