Papa Leo XIV: Kumbukizi ya Miaka 44 ya Daraja Takatifu ya Upadre
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Msingi wa utumishi wa Wahudumu wa Daraja Takatifu, ni Kristo Yesu mwenyewe aliyekuja kutumika na kuutoa uhai wake kwa ajili ya wengi. Ekaristi Takatifu wanayoiadhimisha kila siku iwakumbushe kwamba, “chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa hukaa hali iyo peke; bali ikifa, hutoa mazao mengi” (Yn 12:24). Kristo ndiye chembe ya ngano ya Mungu na kutoka kwa Mungu ameshuka katika ulimwengu. Padri anapoadhimisha Ekaristi Takatifu, anagusa kwa mikono yake Mkate wa ngano ya Mungu ambaye ndiye Kristo Yesu mwenyewe, ambaye kutokana na mateso na kifo chake, chembe ya ngano imekuwa mkate kwa ajili ya ulimwengu mzima. Kwa hiyo, kwa mhudumu wa Daraja Takatifu, Ekaristi Takatifu, licha ya kuwa ishara kuu ya mavuno, furaha ya karamu ya harusi ambako watakuja wengi kutoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini (taz. Mt 8:11), vile vile ni ishara ya Msalaba, kiwango cha juu kabisa cha utumishi. Watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma, wanampongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuadhimisha Kumbukizi ya Miaka 44 tangu alipopewa Daraja takatifu ya Upadre, tarehe 19 Juni 1982 mikononi mwa Askofu mkuu Jean Jadot kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Monica Jimbo kuu la Roma. Daraja hili likakamilika kwa kuwekwa wakfu kuwa Askofu na sasa ndiye Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni huduma ambayo imehifadhiwa katika chombo dhaifu, lakini watu wa Mungu wanamshukuru Mungu kwa utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, unaotekelezwa na Baba Mtakatifu Leo XIV. Waamini wanaendelea kumsindikiza kwa sala na sadaka yao, huku wakimwombea fadhila ya unyenyekevu. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa aendelee kumlinda na kutunza Baba Mtakatifu Leo XIV katika maisha na utume wake na apende kuibariki huduma anayitoa kwa watu wa Mungu.
Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha jinsi kuhani anavyopaswa kuwa chembe ya ngano ya Mungu. Hapaswi tu kuridhika kutoa maneno na matendo ya nje, bali anapaswa kujibidisha katika maisha yake, akijitoa kwa kutumikia mpaka tone la damu. Wahudumu wa Daraja Takatifu wawajibike, awali ya yote, kuihubiri Injili ya Mungu kwa watu wote wakiushika utume wa Bwana asemapo: “Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe” (Rej Mk 16:15). Watu wote wanayo haki ya kulitafuta Neno la Mungu kutoka midomoni mwa mhudumu wa Daraja Takatifu ambaye anapaswa kulihubiri wakati ufaao na wakati usiofaa (Rej 2Tim 4:2). Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unasema kwamba, Mapadri wanaitwa na kuwekwa wakfu ili watumikie kwa unyenyekevu katika kazi ya kutakatifuza… na watende kazi kama wahudumu wa Yule anayetekeleza bila kukoma wadhifa wake wa kikuhani kwa ajili yetu kwa njia ya Roho wake. Wahudumu wa Daraja Takatifu wamepewa mamlaka ya kutoa huduma hii bila ya mastahili yao na tena wamepewa bure (Mt 10:8.)
Kwa hiyo, wahudumu wa Daraja Takatifu wanapaswa kutoa huduma yao ya utumishi kwa bidii na kwa nguvu zao zote bila masharti wala ubaguzi. Hata hivyo, kwa namna ya pekee, wamekabidhiwa hasa walio maskini na wanyonge zaidi. Ni vizuri viongozi wa Daraja Takatifu wakatafakari namna na jinsi wanavyotekeleza agizo hilo. Namna wanavyotoa huduma za kichungaji katika Jumuiya, Kigango, Parokia na pengine hata nje ya majimbo yao. Ni aina gani ya watu wanaokuwa nao karibu zaidi? Je? Maskini na wanyonge wanayo nafasi mioyoni mwao? Wahudumu wa Daraja Takatifu, inabidi wawe tayari kila wakati kutafuta siyo mapenzi yao binafsi, bali mapenzi ya yule aliyewatuma (Rej Yn 4:34; 5: 30; 6:38.) Kazi ya Kimungu ambayo walichukuliwa na Roho Mtakatifu kwayo, inapita nguvu na uwezo pia hekima ya wanadamu; kwa sababu: “Mungu alivichagua vitu vidhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu” (1Kor 1:27.) Kwa hiyo, mhudumu wa Daraja Takatifu anapaswa kutambua udhaifu wake na kufanya kazi kwa unyenyekevu, akijihakiki ni nini impendezayo Bwana na, hali amefungwa na Roho, anaongozwa katika yote na mapenzi yake yule anayetaka watu wote waokolewe; nayo mapenzi ya Mungu ataweza kuyagundua na kuyafuata katika mambo ya kila siku akiwatumikia kwa unyenyevu wote waliokabidhiwa kwake na Mungu kutokana na dhima anayotakiwa kutekeleza, na matukio mbalimbali ya maisha yake.
Kimsingi Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini hao, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo!
