Papa Leo XIV: Kristo Yesu Akawaonea Huruma na Kuwaonesha Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unaopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Mwenyezi Mungu amedhihirisha kwa binadamu huruma yake kuu isiyo na mipaka kwanza kabisa kwa kumtuma Mwanaye wa pekee Kristo Yesu, kwa fumbo la umwilisho, utume wake hapa duniani, na hatimaye kwa njia ya Fumbo Takatifu la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Hata baada ya ufufuko na kupaa kwake Mbinguni, ameendelea bado kuonesha huruma yake kuu kwa njia ya Roho Mtakatifu anayefanya kazi ndani ya wafuasi wake.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha ya kweli; msamaha unaowawezesha wafuasi wa Kristo Yesu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu na hatimaye, huruma ya Mungu inakuwa ni faraja kubwa kwa wasioamini. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi haya yote kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo. “Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.” Mt 9:36-38.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika Tafakari yake, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 14 Juni 2026 amesema, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu; na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili anamwangalia binadamu anayedhulumiwa na kunyanyasika, kiasi cha kukosa nguvu. Anaona madonda ya vita kinzani na migogoro sehemu mbalimbali za maisha ya mwanadamu, anauona utupu wa maisha ya mwanadamu unaokita mizizi yake katika ulaji wa kupindukia. Anaona nyuso za bandia, familia zinazogubikwa na migogoro, vijana wanaoendelea kuota ndoto za mchana. Kristo Yesu anaona na kupenda; anaonesha huruma na upendo wake unaojenga ukaribu wa kidugu unaopania kuimarisha uhusiano wa dhati. Kristo Yesu aliwaona makutano kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, akajitosa bila ya kujibakiza kielelezo kwamba, kimsingi yeye ndiye Bwana wa mavuno, Mchungaji mwema anayetoa faraja ya Mungu kwa watu wanaoteseka; anawakirimia upendo pamoja utu, heshima na haki msingi za binadamu zinaposiginwa kwa umaskini; matumaini mahali ambapo watu wamevunjika na kupondeka moyo; na imani pale ambapo watu hawana tena imani. Kristo Yesu anataja majina ya Mitume, ambao kimsingi ni wamisionari na wahubiri.
Hawa ni akina Simoni aliyeitwa Petro na hapa yumo pia Yuda Iskariote naye ndiye mwenye kumsaliti, lakini Injili inabaki kwa watu wote Neno hai na la kweli kwa wote na kwamba, Ufalme wa Mungu umekaribia kwa sababu Kristo Yesu, Neno wa Mungu amefanyika mwili na hivyo kuwa ni jirani mwema kwa watu wote wa Mungu. Pale ambapo Neno la Mungu linatangazwa na kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; ubaya wa moyo unaanguka na kama usiku unaotoweka na kuacha mapambazuko na kama vile ufufuko ulivyoshinda dhambi na mauti. Kumbe, anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV mtazamo wa Kristo Yesu unaleta mageuzi yanayosheheni upendo na huo unakuwa ni mwanzo wa watu wapya na Kanisa linaloitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama walivyofanya Mitume wa Kristo Yesu na kwamba, wamepta bure, watoe bure.
Hii inatokana na sadaka ya Kristo Yesu aliyejisadaka bila ya kujibakiza na kwamba, hii ni sehemu chemchemi ya neema ya huruma ya Mungu inayoenea sehemu mbalimbali. Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kusali ili kumwomba Bwana wa mavuno: “Apeleke watenda kazi katika mavuno yake.” Mt 9: 38. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha tafakari yake kwa kusema kwamba, dhamana na utume wa uinjilishaji unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo Kristo Yesu anakuwa ni Msamaha kwa Ulimwengu; Huduma kwa wadogo, wanyonge na maskini; ni dhamana na wajibu wa haki na amani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba msaada kutoka kwa Bikira Maria mwingi wa neema, ili waamini waweze kujibu kwa furaha na ujasiri mkuu wito na utume unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.