Papa Leo XIV: Jumuiya ya Chuo Kikuu: Wajenzi wa Amani, Umoja na Mshikamano
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Chuo Kikuu kina dhamana na wajibu wa msingi wa kufundisha, kufanya tafiti, na kuhudumia jamii. Taasisi hizi hutumika kama kitovu cha uzalishaji wa: Ujuzi, maarifa, uundaji wa utu na maadili mema, na kutoa majibu ya kisayansi na kijamii kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii inayowazunguka. Dhamana na wajibu mkuu wa Chuo Kikuu unaweza kufupishwa katika nguzo kuu tatu: Ufundishaji na Ukuaji wa Kiakili: Kutoa mafunzo ya kitaaluma na kiutu ili kuandaa wataalamu, viongozi, na raia wenye uwezo wa kufikiri kwa kina na kutatua matatizo na changamoto zinazowakabili. Tafiti na Ubunifu: Kufanya tafiti makini zinazolenga kuchochea maendeleo endelevu, uvumbuzi, na kupata majibu ya kisayansi kwa changamoto za kiafya, kijamii, kiuchumi, na kiteknolojia. Huduma kwa Jamii: Kutumia utaalamu na tafiti zake kutoa mwelekeo, ushauri, na kuelimisha umma ili kujenga jamii yenye haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Bodi ya Magavana wa Chuo Kikuu cha Wayahudi Yerusalemu, Alhamisi tarehe 18 Juni 2026 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican na baadaye kutembelea mji wa Roma.
Roma ni kitovu cha Kanisa Katoliki, mahali ambapo imani ya Kikristo imekuwa na kushamiri na kwamba, mji wa Roma ni mahali ambapo watu kutoka katika tamaduni mbalimbali kwa miongo mingi wamekuwa wakikutana. Ni katika muktadha huu, Chuo kikuu nacho ni mahali pa watu kukutana, ili kukuza na kudumisha ujuzi na maarifa; ni mahali pa kufanyia tafiti na kukuza urafiki wa kijamii na udugu wa kibinadamu. Chuo kikuu kinapaswa kuwa ni mahali pa kuwakutanisha watu, ili kujenga na kudumisha utu wao wa kibinadamu licha ya tofauti zao za kitamaduni na lugha wanazozungumza kama nyenzo ya mawasiliano ya jamii. Chuo kikuu ni mahali muafaka pa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni katika ukweli na uwazi, kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kutoa fursa kwa kila mtu kukua na kukomaa, ili hatimaye, kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za kijamii, hata kama bado kuna hali ya kutoelewana au kusigana. Miundo mbinu hii ikitumiwa kikamilifu na kwa udumifu, inaweza kusaidia kubomolea mbali vikwazo na kinzani za kutoelewana na kutoaminiana katika jamii.
Baba Mtakatifu Leo XIV ameiambia Bodi ya Magavana wa Chuo Kikuu cha Wayahudi Yerusalemu kwamba, Jumuiya zao mbalimbali zinaweza kuendelea kuwa ni wajenzi wa amani ya kweli, kwa kufanya kazi kwa pamoja, katika hali ya unyenyekevu na utulivu. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda waja wake wanaothamini ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani na maridhiano; watu wanaotubu na kumwongokea Mungu kutoka katika sakafu ya nyoyo zao kama anavyosema Mzaburi katika ile Sala yake ya kuomba amani. “Na nisikie atakavyosema Mungu BWANA, Maana atawaambia watu wake amani, Naam, na watauwa wake pia, Bali wasiurudie upumbavu tena. Hakika wokovu wake u karibu na wamchao, utukufu ukae katika nchi yetu” Zab 85: 8-9.
Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wao wenyewe wanakuwa ni chemchemi ya haki, amani na maridhiano na kwa njia, hii wanaweza pia kuwashirikisha jirani zao na hivyo kuwa rahisi fadhila hizi kutambulikana katika maisha ya wachaji wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, anaendelea kusali kwa ajili yao ili Mwenyezi Mungu aweze kubariki juhudi hizi za kuwafunda mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano na kwamba, Jumuiya ya Chuo kikuu iendelee kuwa ni nguzo ya matumaini na umoja katika ulimwengu mamboleo ambao umegawanyika na kusambaratika sana. Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru na kuwapongeza kwa uvumilivu wao na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.
