Papa Leo XIV Hotuba Kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 99 wa ROACO: 2026
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO, (R.O.A.C.O. Riunione Opere Aiuto Chiese Orientali), kuanzia Jumatatu tarehe 15 Juni 2026 limekuwa likiadhimisha Mkutano wake wa 99. Hiki ni kipindi cha kusali na kuwaombea wafadhili wa ROACO ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma mbalimbali zinazotolewa na ROACO kwa Makanisa ya Mashariki. Ni nafasi pia kwa ajili ya kuendelea kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuingilia kati na kuwakirimia waja wake amani, utulivu wa kisiasa, kijamii na kidini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mktano mkuu wa 99 unanogeshwa na kauli mbiu: “Majiundo ya Wakleri na Wamonaki wa Makanisa ya Mashariki.” Mkutano huu umefunguliwa na Kardinali Claudio Gugerotti, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki kwa Ibada ya Misa Takatifu na baadaye wajumbe wameendelea kuchangia mada mbalimbali mintarafu: Changamoto mamboleo kwa Makanisa ya Mashariki; Maisha na utume wa Chuo Kikuu cha Bethlehemu; Malezi na Majiundo ya Makleri na Wamonaki kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki; Hali halisi inavyoendelea huko Mashariki ya Kati, hii ni taarifa ambayo imetolewa na Askofu mkuu Paolo Borgia, Balozi wa Vatican nchini Lebanon.
Wajumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO, Alhamisi tarehe 18 Juni 2026 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye amekazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa waamini kuunga mkono juhudi za Kanisa katika maisha na utume wake; kwa kujitahidi kukuza na kudumisha utambulisho wake, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hii ni amana na utajiri unaofumbatwa katika Makanisa ya Mashariki, mwaliko kwa Makanisa haya kushirikisha amana na utajiri huu kwa Makanisa ya Magharibi. Makanisa ya Mashariki yana amana na utajiri mkubwa ambao waamini wake hawautambui bado katika Mapokeo ya Makanisa haya. Kanisa limeunganika katika umoja, lakini haliko sawasawa, kwani limezaa taalimungu, maisha ya kiroho na Mapokeo mbalimbali yanayoendelea kutumika katika maisha na utume wa Makanisa haya, changamoto na mwaliko kwa Makanisa haya kuzamisha tunu hizi katika maisha na utume wa Makanisa mahalia, ili umoja kamili wa Kanisa la Mashariki uweze kuonekana kama kielelezo cha chemchemi ya imani; mwanga wa neema unaobubujika kutoka katika amana na utajiri wa Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa katika utajiri na utakatifu wake; kielelezo cha sifa kwa Fumbo la Mungu anayepaswa kuabudiwa, kuhimidiwa na kutukuzwa.
Liturujia inaonesha nguvu ya sala na hivyo kuendelea kumimina amana na utajiiri sanjari na kufunua uzuri wa Mungu. Ni fursa kwa waamini kumshukuru Mungu, mintarafu taalimungu ya kibinadamu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wanasema kuna maelezo mbalimbali ya Kitaalimungu yanayokumbatiana na kukamilishana. “Hivyo haishangazi ikiwa mara kwa mara vipengele fulani vya fumbo lililofunuliwa vinahisiwa kwa usawa zaidi na kubainishwa waziwazi na Kanisa moja kuliko jingine.” UR, 17. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kuna umuhimu wa kuifahamu Liturujia ya Makanisa ya Mashariki, kuzama katika uelewa wa tasaufi ya Mababa wa Kanisa kutoka katika Makanisa ya Mashariki sanjari ya kujitahidi kumwilisha Mafundisho ya Mababa hawa yanayopata rutuba yake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Haya ni mambo ambayo yametiliwa mkazo hivi katika majiundo na malezi ya Majandokasisi. Kumbe, kuna haja pia ya kukazia malezi na majiundo makini ya Mapadre. Kuna uhusiano kati ya upendo, moyo ambao uko wazi na umejaa nguvu ya Roho Mtakatifu, changamoto kwa waamini kuendelea kuboresha maisha ya kiroho kwa njia ya sala, ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa; maisha adili na matakatifu, kielelezo cha imani tendaji, chemi chemi ya imani na maisha ya kimungu, kielelezo cha imani tendaji katika huduma. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanawekeza kwenye Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kielelezo cha imani tendaji; majadiliano katika ukweli na uwazi sanjari na ujenzi wa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hii ni changamoto kwa Makanisa ya Mashariki kujenga na kudumisha amani na utulivu kwani ukosefu wa amani athari zake ni kwa maskini na watu wa kawaida huko Mashariki ya Kati.
Baba Mtakatifu Leo XIV kwa mara nyingine tena ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya tafakari ya kina kuhusu matokeo ya vita, ukosefu wa haki, amani na utulivu, ili kuweza kuzuia vitendo hivi kwa kujikita katika maamuzi ya busara, adili na uwajibikaji. Historia inaonesha jinsi njama za unyanyasaji na ukandamizaji, mamlaka na utawala, faida zinazopatikana bila haki na bila hata aibu, zinavyorudisha nyuma ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba, Kristo Yesu, Bwana na Mfalme wa amani aweze kuwajalia waja wake amani ya kudumu na hivyo kukoleza moyo wa toba na wongofu wa ndani, ili kuheshimu utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, ustaarabu wa kuishi kwa amani uweze kurejea tena. Baba Mtakatifu amewatia shime wajumbe kuendelea kuishi katika upendo bila ya kukata tamaa na kuendelea kuweka tumaini lao kwa Kristo Yesu.
