Papa Leo XIV kwa Jumuiya Katoliki ya Madrid:Mapadre watambue utendaji wa jumuiya zao!

Papa Leo XIV alikutana na Jumuiya ya Jimbo Kuu la Madrid nchini Hispania katika Uwanja maarufu wa Santiago Bernabéu,Jumatatu Juni 8.Kwa wawakilishi wa Kanisa mahalia,Papa aliwakumbusha kuwa,"lazima wajifunze upya sanaa ya kiroho ya kuwa na urafiki,bila hiyo hata kutangaza Injili kunaweza kuwa marudio yasiyo na tija,kupoteza ufanisi wake na kuacha nafasi ya kuchanganyikiwa na kutoaminiana.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Muwe kila mtu, kama Biblia iliyo wazi: Neno la Mungu lipatikane katika nyuso zenu na katika maisha yenu. Upendo, kiukweli, ndiyo lugha inayomfanya kila mtu ajisikie yuko nyumbani na zaidi wema wa waliowachache unaweza kushinda hofu ya wengi. Haya yalikuwa ni maneno ya kutia moyo na ushauri kutoka katika hotuba ya Baba Mtakatifu Leo XIV, kwa washiriki wa Mkutano na Jumuiya ya Jimbo la mji mkuu wa Hispania, ambapo alikutana nao, Jumatatu jioni  ikiwa ni kufunga siku ya tarehe 8 Juni 2026 katika Uwanja maarufu wa Santiago Bernabéu huko Madrid, baada ya siku nzima ya mikutano yake akiwa katika ziara yake ya nne ya kitume inayoongozwa na kauli mbiu:“Inua macho yako." Uwanja huo ulijaa furaha kubwa kwa wadogo na wakubwa wa Jumuiya nzima Katoliki ya Madrid na wengine kutoka nje ya mji huo.

Sanamu ya Bikira Maria Uwanjani
Sanamu ya Bikira Maria Uwanjani   (@Vatican Media)

Shuhuda za hali halisi ya Kanisa Mahalia:umoja katika utofauti

Baada ya kusikiliza ushuhuda wa wawakilishi kutoka hali halisi tofauti za Kanisa la Madrid, Baba Mtakatifu Leo XIV alionesha furaha yake ya kuweza kuunganisha sauti yake kwenye wimbo huo mkubwa wa imani, na ule wa familia ya kikanisa wanaojifunza sanaa ya umoja, katika utofauti. Na akitoa maoni yake kuhusu maneno aliyoambiwa na Askofu Mkuu wa Madrid, Papa Leo XIV alisema kwamba, "namba, data na ukweli hazitoshi kuunda jumuiya. Mioyo yetu inahitaji kuimba, yaani, kutafsiri matukio na hali kwa kusherehekea pamoja na wengine maana inayoakisi. Kwa Kanisa, hili hutokea kwa njia ya kipekee katika liturujia, ukumbusho mkubwa wa historia ambao umetuokoa."

Kundi la mapadre waliimba mbele ya Papa
Kundi la mapadre waliimba mbele ya Papa   (@Vatican Media)

Upendo unatuwajibisha

Katika muktadha huo, Papa Leo XIV alibainisha kwamba,  kuimba ni usemi muhimu wa maisha na utamaduni wa Kikristo, wenye uwezo wa kusambaza furaha na matumaini katikati ya matatizo. Kwa hivyo, Kanisa la Jimbo linaitwa kushuhudia Injili katika nyanja mbalimbali za jamii, likisindikizana na watu katika kutafuta fursa mpya. Kwa hivyo, Papa alionesha kwamba furaha ya Kikristo si hisia ya muda mfupi, bali ni mtazamo wa kina na wa kudumu unaoimarisha jumuiya na kuakisi ujumbe wa mitume, ambao hutualika kila mara kuishi kwa furaha.“Ni Evangelii Gaudium, yaani Injili ya furaha, jibu la pamoja kwa kazi ya Mungu katika Yesu Kristo: maisha yake, kifo chake, na ufufuko wake vimebadilisha  mtazamo wa historia milele  kwa wale waliokutana naye na kumfuata, hata kama kwa njia tofauti na katika njia tofauti. Leo pia, upendo wa Kristo unatuwajibisha (taz. 2 Kor 5:14), kitenzi ambacho Mtakatifu Paulo anatumia, pia kinamaanisha ‘hutuvutia,’ ‘hutushikilia pamoja,’ ‘hutumiliki’na hivyo hutuita kwa jukumu la kutenda.”

Uwanja ulipendeza na waamini kutoka jimbo Kuu Madridi na sehemu nyingine
Uwanja ulipendeza na waamini kutoka jimbo Kuu Madridi na sehemu nyingine   (@Vatican Media)

Ubatizo hubadilisha maisha ya watu kwa matendo ya Kristo

Na akizungumzia moja ya ushuhuda, Baba Mtakatifu Leo XIV  alionesha kwamba Ubatizo hubadilisha maisha ya watu kwa kina kwa kuzingatia maadili, vipaumbele, na matendo yao kwa Kristo. Shukrani kwa sakramenti hii, karama na uwezo wa mtu binafsi huacha kuelekezwa tu kwa faida ya kibinafsi na huwekwa katika huduma ya wengine na kwa manufaa ya wote. Hatupaswi kuogopa kwamba hautawahi kuleta umoja. “Katika suala hili, Papa alisisitiza kuwa Agano Jipya, katika aina mbalimbali za sauti zake, linashuhudia ushirika katika utofauti, yaani, uelewa uliotoweka Babeli, ambapo kila mtu, kulingana na maelezo ya Biblia, aliyelazimishwa katika mradi wa kidikteta na wa kibinadamu tu, aliishia kushindwa kuelewa jirani yake.”

Papa akihutubia
Papa akihutubia   (@Vatican Media)

Inawezekana kujenga pamoja udugu

Na akinukuu  Waraka wa Magnificat Humanitas, wa hivi karibuni aya ya 10, Papa Leo XIV alipendekeza, kama njia mbadala ya upatanisho na mkanganyiko, mfano wa Nehemia, ambaye alihusisha jamii nzima katika kujenga upya kuta za Yerusalemu. "Leo hii, kujenga upya kunamaanisha kutambua kwamba, katika wingi wa sauti na maono ambayo wakati mwingine hukumbusha mtawanyiko wa lugha, hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa: ule wa kujenga pamoja, kubadilisha utofauti kuwa rasilimali na kufanya usikilizaji na mazungumzo kuwa msingi wa pamoja wa kukuza haki na udugu. Na, katika kazi hii ya pamoja, Wakristo hupata njia yao wenyewe ya kujenga: kuelekeza hatua kwa Mungu, ili, katika mwanga wake, wingi usiweze kutoweka na kuwa machafuko, bali, katika utendaji wa sinodi, uwe nafasi ambayo ubinadamu hurejesha misingi yake imara na kusudi lake kuu." Kwa hivyo, Baba Mtakatifu alisisitiza kwamba kuna uhusiano maalum kati ya Kanisa na jiji, ambao unakuwa muhimu zaidi wakati wa mabadiliko. Uhusiano huu unajidhihirisha katika vifungo vya kibinafsi na vya kijamii na mbele ya vyama na taasisi.

Vijana wakitumbuiza
Vijana wakitumbuiza   (@Vatican Media)

Utume wa Kikristo una sifa unapokuwa katikati ya utamaduni mpya

Katika miji mikubwa, utume wa Kikristo unachukua sifa zake unapokua katikati ya utamaduni mpya na unaobadilika kila mara wa mijini. "Ufafanuzi katika jambo hili umekomaa sana katika safari ya sinodi, ambayo imeturuhusu kujuana na kusikilizana kwa undani zaidi katika mazingira ambayo jumuiya ya kijimbo inaishi na kuchukua sura. Swali linalokuwa muhimu zaidi ni: je, kile tulicho na tunachofanya kama Wakristo kinafikia 'ambapo masimulizi na dhana mpya zinaundwa,' yaani, 'kiini cha ndani zaidi cha roho ya miji' (ibid., 74)? Ni kweli kwamba kutoa jibu kunaweza kuwa vigumu, lakini inawezekana ikiwa tutatafuta ukweli pamoja." Kwa hivyo, Papa alikumbusha kwamba, ili kufikia moyo wa jiji, ni lazima tukuze ufahamu kwamba ukweli ni wa ala na unatuzidi kila wakati, tukuze hamu ya kukutana na Bwana Mfufuka, ambaye huwa anatutangulia, na labda tayari yupo ambapo hatujamtafuta bado. Kwa njia hiyo, kumtafuta na kumfuata ndio sharti la kumtaja: vinginevyo, hakuna uinjilishaji na leo tunaweza kuelewa hili vizuri zaidi kuliko hapo awali. "Katika miji mikubwa, zaidi ya maeneo mengine, wakati mwingine inaonekana kwamba hatuna ramani za kusafiri salama. Kisha ni lazima tujifunze tena sanaa ya kiroho ya kuwa na urafiki, ambayo bila hiyo hata kutangaza Injili kunaweza kuwa marudio yasiyo ya kibinafsi na, kupoteza ufanisi wake, huacha nafasi ya kuchanganyikiwa na kutoaminiana."

Mji wa madrid uliojaa tamaduni na roho tofauti kuishi pamoja

Papa Leo XIV  vile vile alisema kwamba, " Madrid ni mji mkubwa ambapo tamaduni  na "roho" tofauti huishi pamoja. Mungu anajua mioyo ya kila mmoja wa wakazi wake mmoja mmoja. Anawajua kama Yeye pekee anavyojua na anaweza, yaani, katika upendo na kwa hivyo, katika uhuru. Yeye ni huruma isiyo na kikomo na anatamani wote waokolewe. Anatamani hadi kufikia hatua ya kuwa mwili na kuchukua juu Yake dhambi zote, uovu, na ubaya wa ulimwengu. Mtazame Yesu Kristo!

Papa akishukuru familia ya Peru iliyotoa ushuhuda
Papa akishukuru familia ya Peru iliyotoa ushuhuda   (@Vatican Media)

Tazama Habari Njema, neema tuliyopokea na ambayo tumeitwa kushirikisha na kila mtu! Kwa maana wote, bila ubaguzi, wameumbwa kwa ajili ya uzima, na kwa ajili ya uzima katika ukamilifu wake."Uwepo wa Kanisa katika jiji kubwa ni mfano wa siri hii ya wokovu. Kitabu cha Yona kinanijia akilini, kito cha Biblia ambacho ninawaalika mkisome au kukisoma tena, kibinafsi na kama jumuiya. Sio kwa bahati mbaya kwamba ilikuwa hasa katika miji ambapo mitume walianzisha Kanisa changa, wakikutana na kukataliwa tu,  bali pia kukaribishwa katika sehemu zile ambapo, kwa kawaida zaidi, watu wanakabiliwa na utofauti na mabadiliko."

Tunaweza kutoa ushuhuda wa Injili wenye nguvu

Kwa pamoja, kama Kanisa la Jimbo, Papa Leo XIV alisisitiza tena, “tunaweza kutoa ushuhuda wa Injili unaoachilia nguvu bora za ubinadamu uliojaa picha na maneno, lakini wenye njaa ya haki na kiu ya ukweli. Kuwa tayari kukumbatia mwanzo mpya si kama ubaguzi, bali kama kanuni ya utume. Uwekezaji katika mabaraza ya parokia na majimbo hauna lengo dogo kuliko hili yaani la kubadilisha hisia za kila mtu kupitia kusikiliza kwa undani kile ambacho Roho analiambia Kanisa. Itakuwa aibu kuzipunguza hadi taratibu za urasimu tu," Papa alionya. "Hizi ni nafasi za kusikilizana na kufanya utambuzi, ambazo bila hizo kila mtu huenda kwa njia yake yenyewe, lakini pia tuna hatari ya kutoelewa mahali ambapo Bwana anataka tuwe, anatarajia nini kutoka kwetu, na ni mabadiliko gani anatuita. Tunaposhughulikia nafasi hizi, basi ibada inakuwa uhai, na vifungo vya udugu na mipango ya mshikamano huibuka miongoni mwa watu.”

Papa akibariki kabla ya kuacha uwanja
Papa akibariki kabla ya kuacha uwanja   (@Vatican Media)

Mapadre watambue utandaji wa jumuiya zao

Baba Mtakatifu Leo XIV akiendelea na hotuba yake aliwaalika mapadre waweze kutambua utendaji wa utambuzi wa jumuiya kama mojawapo ya fursa kubwa zaidi ambazo sinodi hutoa kwa huduma yao. "Na bila kupoteza mtazamo wa kile kilicho muhimu, kukaa mara kwa mara na watu wenu ili kutafsiri maisha ya ujirani, mabadiliko ya kiutamaduni, mivutano ya kijamii, na desturi za kikanisa kwa mwanga wa Injili kutaimarisha na kufariji huduma yenu." Pia Papa alisema "itasaidia kujitenga na kutengwa na kupata furaha ya Roho Mtakatifu. "Hakika, tunapopunguza maisha ya kikanisa kuwa utaratibu ambapo kila mtu anabaki amefungiwa katika tabia na majukumu yake, tunachokosa ni Roho. Roho huinua miito na kuwaunganisha, wakati mwingine huchochea msukosuko, majadiliano, na utafutaji wa mizani mipya. Msishtuke na haya yote; furahini nayo."

Huu ndiyo mdundo wa Injili unaoambukiza

Hatimaye Papa Leo XIV, alitoa wito kwa jumuiya nzima ya Kanisa kuwa “ Simulizi ambazo tumesikia usiku wa leo, zituambie, au tuseme ni kiasi gani cha maisha katika Kanisa hili. Na akikumbuka baadhi ya shuhuda za jumuiya ya Jimbo alionesha kwamba hili ndilo Kanisa, lenye mdundo wake wa Injili unaoambukiza. “Hili ndilo Kanisa, kaka na dada wapendwa! Huu ndio muziki wa Injili, pamoja na mdundo wake unaambukiza. Unapofikia moyo, humfanya mtu ahisi kukaribishwa kwa mikono miwili, kama dada aliyetoka Peru kuja Madrid. Wengi, kama yeye na familia yake, mwanzoni huhisi kuogopa kukaribia, kwa sababu wamesikia kuhusu ubaguzi na kukata tamaa."

Papa akiacha Uwanja
Papa akiacha Uwanja   (@Vatican Media)
Papa alisubiriwa kila kona ya kuzungukia Uwanja maarufu wa Madrid
Papa alisubiriwa kila kona ya kuzungukia Uwanja maarufu wa Madrid   (@Vatican Media)

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

08 Juni 2026, 20:47