Mkutano wa Tatu wa Wazi wa Wataalam wa Kurekebisha Tamko la Taipei wa Chama cha Madaktari Ulimwenguni, uliofadhiliwa na PAV, WMA pamoja na Jumuiya ya Madaktari ya Israeli, ulifunguliwa na Askofu mkuu Renzo Pegoraro, Mkutano wa Tatu wa Wazi wa Wataalam wa Kurekebisha Tamko la Taipei wa Chama cha Madaktari Ulimwenguni, uliofadhiliwa na PAV, WMA pamoja na Jumuiya ya Madaktari ya Israeli, ulifunguliwa na Askofu mkuu Renzo Pegoraro,   (@Vatican Media)

Mkutano wa Kurekebisha Tamko la Taipei la Chama Cha Madaktari Ulimwenguni

Mkutano wa Tatu wa Wazi wa Wataalam wa Kurekebisha Tamko la Taipei wa Chama cha Madaktari Ulimwenguni, uliofadhiliwa na PAV, WMA pamoja na Jumuiya ya Madaktari ya Israeli, ulifunguliwa na Askofu mkuu Renzo Pegoraro, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha tarehe 1 Juni 2026 mjini Vatican na kuhitimishwa Jumanne tarehe 2 Juni 2026. Papa Leo XIV anawapongeza wataalam kwa juhudi zao za kurekebisha Tamko la Taipei la Chama Cha Madaktari Ulimwenguni; WMA.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taasisi ya Kipapa ya Maisha “Pontifical Academy for Life” (PAV) ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo tarehe 11 Februari 1994, kwa Motu Proprio, yaani Barua binafsi ya “Vitae mysterium, Fumbo la maisha.” Lengo la taasisi hii ni kusimama kidete kulinda na kutetea thamani ya maisha na utu wa binadamu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Taasisi hii ina dhamana ya kutafiti, kuunda utamaduni wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo na kuhabarisha wadau mbalimbali changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai duniani! Ni wajibu wa taasisi hii kutenda katika hali ya uwazi na kwa haraka na kwamba, inapaswa kuwajulisha viongozi wa Kanisa, taasisi za elimu maumbile na sayansi ya biolojia ya binadamu; taasisi za kiafya; vyombo vya mawasiliano ya jamii na jumuiya za kiraia kuhusu shughuli na tafiti zake kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Taasisi ya Kipapa ya Maisha, inawajibika kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu, utu na heshima yake, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kudumisha heshima kati ya vizazi. Ni wajibu wa taasisi hii kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya binadamu; kwa kuendeleza tunu msingi za maisha: kiroho na kimwili, ili kudumisha Ikolojia ya binadamu kwa kumpatia mwanadamu nafasi yake katika Kazi ya Uumbaji. Taasisi hii inapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi na Sekretarieti kuu ya Vatican, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kuheshimu na kuzingatia dhamana na wajibu wa kila taasisi katika ari na moyo wa kushirikiana, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa maisha. Taasisi inashirikiana pia na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu zinazojihusisha na tafiti kuhusiana na maisha ya binadamu.

Mkutano wa Chama Cha Madaktari Ulimwenguni: Tamko la Taipei
Mkutano wa Chama Cha Madaktari Ulimwenguni: Tamko la Taipei   (@Vatican Media)

Tamko la Taipei la Chama cha Madaktari Ulimwenguni ni sera kuu ya maadili ya matibabu iliyoanzishwa na Jumuiya ya Madaktari Ulimwenguni (WMA), kwa kuweka viwango vya kimaadili vya kimataifa kwa ajili ya ukusanyaji, uhifadhi, na matumizi ya nyenzo za kibiolojia ya binadamu na data ya afya katika hifadhidata za bioadamu na hifadhidata za afya. Tamko hili linashughulikia matumizi ya data nje ya matibabu ya moja kwa moja ya mtu binafsi, kama vile utafiti wa matibabu, biashara na maombi ya usimamizi. Nguzo zake kuu ni pamoja na: Idhini ya Taarifa: Ushiriki na uchangiaji wa sampuli za kibaolojia lazima uwe wa hiari kabisa, na wafadhili lazima waelezwe kikamilifu kuhusu madhumuni ya hifadhidata na hatari zake. Haki ya Kujitoa: Watu binafsi wana haki kamili ya kubadilisha idhini yao, kutoa data inayoweza kutambulika, au kuondoa nyenzo za kibayolojia kutoka kwa benki ya kibayolojia au hifadhidata wakati wowote bila kulipiza kisasi. Faragha na Usiri: Ulinzi mkali lazima uwekwe ili kuhakikisha kutokujulikana kwa mgonjwa na kulinda taarifa nyeti za afya ya kibinafsi. Sera ya Pamoja: Uwazi na Utawala: Hifadhidata lazima zidhibitiwe kwa uwajibikaji wa umma, uwazi, na uangalizi kutoka kwa kamati huru za maadili na utu wema. Mkutano wa Tatu wa Wazi wa Wataalam wa Kurekebisha Tamko la Taipei wa Chama cha Madaktari Ulimwenguni, uliofadhiliwa na PAV, WMA pamoja na Jumuiya ya Madaktari ya Israeli, ulifunguliwa na Askofu mkuu Renzo Pegoraro, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha tarehe 1 Juni 2026 mjini Vatican na kuhitimishwa Jumanne tarehe 2 Juni 2026. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba yake anapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wataalam hawa katika juhudi zao za kurekebisha Tamko la Chama cha Madaktari Ulimwenguni kuhusu masuala ya kimaadili: Mintarafu hifadhidata za afya na benki za viumbe hai.

Faragha ya mtu inapaswa kulindwa na kuheshimiwa
Faragha ya mtu inapaswa kulindwa na kuheshimiwa   (@VATICAN MEDIA)

Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” kwa kifupi “MH” anazungumzia aina mpya ya ukoloni ambao umeibuka na unalenga kubadilisha maisha ya mtu binafsi kuwa ni “data” zinazoweza kunyonywa, MH, 178, kumbe, uboreshaji unaoendelea na mabadiliko ya teknolojia una maanisha kusasisha sera zilizopo za usalama na kwamba faragha imekuwa suala la dharura na muhimu kwa sababu mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Rej. Mwa 1:26-27. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kila mwanadamu ni mtu asiyeweza kupunguzwa na wa pekee; wa thamani isiyokadirika, na kwa hiyo ni lazima alindwe dhidi ya aina mbalimbali za unyonyaji na biashara ambazo zinataka kumpunguza mtu huyo kama “seti ya data.” Baba Mtakatifu anahimiza utakatifu,  ukuu na utu wa mwanadamu na kwamba, hizi ni juhudi zinazopaswa kuvaliwa njuga kama msingi wa ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.

Papa Leo XIV: Magnifica humanitas: Utu, heshima na haki msingi
Papa Leo XIV: Magnifica humanitas: Utu, heshima na haki msingi   (@VATICAN MEDIA)

Kwa upande wake Askofu mkuu Renzo Pegoraro, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha katika hotuba yake ya ufunguzi amerejea safari ambayo waliianza kwa pamoja kunako mwaka 2017, kwa kujadili kuhusu huduma ya afya kwa watu walioko kufani; usawa katika utoaji wa chanjo na kwa sasa ni mkutano unaojadili kuhusu upyaisho wa masuala ya maadili na utu wema na kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV anaonya juu matumizi makubwa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayohatarisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, katika ulimwengu wa utandawazi. Hata katika maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, lakini utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa. Chama cha Madaktari Ulimwenguni kinatafsiri kanuni hii kwa kukazia kutouza au kuhamisha “data” katika muktadha wa utafiti shirikishi wa kimataifa; na kutoruhusu mantiki ya kibiashara au kisiasa kuondoa imani ambayo wagonjwa huweka katika mfumo wa huduma ya afya kwa kushirikisha “data” zao. Taasisi hii ya Kipapa pamoja na washirika wake wanatambua changamoto zinazoletwa na “data za afya” katika enzi kidijitali na kwamba, haziwezi kushughulikiwa kwa zana za kiufundi-kisheria au kwa kanuni dhahania pekee, bali zinahitaji maadili yanayojumuishwa katika utendaji, yenye uwezo wa kuongoza chaguo madhubuti za madaktari, watafiti, taasisi na watunga sera na sheria. Kanuni maadili na utu wema inapaswa kuwa ni dira na mwongozo mintarafu masuala ya uchumi na mazingira, masuala ya kijamii na kwamba, wanyonge na dhaifu katika jumuiya wanapaswa kulindwa. Matumizi ya teknolojia ya akili unde katika masuala ya dawa, miundo ya benki, mifumo ya afya kidijitali inaonesha nguvu kubwa. Kumbe, umuhimu wake kwa binadamu unategemea nguvu ya ulinzi wa kimaadili, unaoweza kujengwa karibu nao. Huu ni ulinzi kwa ajili ya watu binafsi; sanjari na uaminifu wa kijamii.

Utu wa Binadamu
02 Juni 2026, 16:59