Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 amefanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 amefanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania.  (@Vatican Media)

Hija ya 4 ya Kitume ya Papa Leo XIV Hispania: Shukrani na Baraka

Papa Leo Leo XIV Dominika tarehe 14 Juni 2026 amewaongoza watu wa Mungu kwa tafakari ya kina kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mt.Petro mjini Vatican. Ametumia fursa hii, kumshukuru Mungu, aliyemwezesha kufanya hija ya kitume nchini Hispania, anawashukuru watu wa Mungu nchini humo kwa mapokezi makubwa ya kukata na shoka waliyomfanyia wakati wa Hija yake ya Kitume nchini Hispania. “Que Dios bendiga siempre a España” yaani “Mungu Ibariki Hispania!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 amefanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inueni macho yenu.” Yn 4:35.” Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya kurejea tena Mjini Vatican, Dominika tarehe 14 Juni 2026 amewaongoza watu wa Mungu kwa tafakari ya kina kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ametumia fursa hii, kumshukuru Mungu, aliyemwezesha kufanya hija ya kitume nchini Hispania, anawashukuru watu wa Mungu nchini humo kwa mapokezi makubwa ya kukata na shoka waliyomfanyia wakati wa Hija yake ya Kitume nchini Hispania. “Que Dios bendiga siempre a España” yaani “Mungu Ibariki Hispania Daima.” Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya kupata mapokezi makubwa ya Kitaifa alikwenda kumtembelea Mfalme na Malkia wa Hispania, ambako alipata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao huko nchini Hispania. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amegusia kuhusu mchango mkubwa uliotolewa na Yakobo Mtume katika mchakato wa uinjilishaji wa watu wa Mungu nchini Hispania, kiasi cha kuchangia taalimungu na utume wake. Baba Mtakatifu anasema, yuko kati yao ili kuwatia shime, kupyaisha uaminifu wao, ili waweze kujikita katika mchakato wa upatanisho; ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kukoleza ujumbe wa amani. Amegusia pia kuhusu mchakato wa watakatifu Yohane wa Msalaba na Mtakatifu Thetesa wa Avila. Kanisa Katoliki linapenda kujielekeza katika huduma ya upatanisho na amani, kwa kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene.

Baba Mtakatifu Leo XIV akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Hispania
Baba Mtakatifu Leo XIV akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Hispania   (@Vatican Media)

Tangu mwanzo anasema Baba Mtakatifu Leo XIV Hispania imepokea Habari Njema ya Wokovu, utume uliofanywa na Yakobo Mtume na umuhimu wa taalimungu kama sehemu ya mwendelezo wa utume wa Kanisa unaopata chimbuko lake katika Sherehe ya Pentekoste, mambo ambayo yamechangia katika kuleta mabadiliko katika maisha na utamaduni wa watu wa Mungu nchini Hispania, hapa ni chemchemi ya ibada mbalimbali, amana na utajiri wa muziki mtakatifu, yote haya ni matunda ya watu wa Mungu nchini Hispania kukutana na Kristo Yesu; hawa kwa hakika ni watu wanaopenda na kuthamini Injili ya uhai. Baba Mtakatifu anasema, yuko kati yao ili kuragibisha mchakato wa upatanisho na ushirikiano miongoni mwa watu wa Mataifa, kwa kujikita katika utamaduni wa watu kukutana, ili kukoleza amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya wengi. Pia upo mvutano wa daima kati ya fikira na hali halisi ya mambo, changamoto ni kuendeleza majadiliano, ili ukweli uweze kujikita katika uhalisia wa mambo, kumbe, kuna haja ya kuendeleza mchakato wa kujitakasa, upatanisho na majadiliano; mambo msingi katika maisha.

Uinjilishaji wa kina ni sehemu ya maisha na vinasava vya Kanisa Hispania
Uinjilishaji wa kina ni sehemu ya maisha na vinasava vya Kanisa Hispania   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake kwa Bunge la Hispania, ameitaka Hispania kuendelea kuwa ni mahali pa watu kukutana, katika utamaduni ili hatimaye, kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu, chemchemi ya Injili ya matumaini. Amekazia utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuongozwa na kauli mbiu ya Umoja wa Ulaya “In varietate concordia” yaani “Umoja katika Utofauti” kwa kusimikwa katika tofauti za tamaduni, mapokeo na vipaumbele; mambo ambayo kwa pamoja yanaunda amana na utajiri mkubwa wa watu wa Mungu nchini Hispania. Mama Kanisa anatembea bega kwa bega na binadamu, anashiriki matumaini na madonda yake, anaendelea kusikiliza na kujibu maswali msingi ya binadamu wa kila nyakati na kwamba, kuna tofauti ya utendaji kati ya Kanisa na Serikali; na kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwa kuzingatia kwamba, uhuru ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu.

Papa Leo XIV akihutubia Bunge la Hispania
Papa Leo XIV akihutubia Bunge la Hispania   (@Vatican Media)

Kumbe, kuna uhusiano mkubwa kati ya sheria, kanuni maadili na utu wema na kwamba, kimsingi uongozi unabeba dhamana kubwa ya haki na uwajibikaji. Ndiyo maana hata katika ulimwengu mamboleo bado: Utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni vigezo msingi katika kupima mahusiano na mafungamano ya kijamii katika ngazi ya Kitaifa na Kimataifa. Leo hii kuna changamoto mamboleo kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, uchumi, tafiti na tiba; ulimwengu wa kidigitali unaogusa maisha ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake na kwamba, maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde hayana budi kudhibitiwa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, anayepaswa kuongoza maoni na maamuzi mintarafu: kazi, mshikamano, siasa za kijamii; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jamii inayosimikwa katika msingi wa haki inatambua na kuthamini utu wa binadamu unaotishiwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu ni fursa ya kuzama zaidi katika imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na hivyo kuendelea kupyaisha upendo kwa Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Nchini Hispania Sherehe hii ni kiini cha maisha ya waamini, upyaisho wa upendo wa Mungu na uaminifu kwa Mungu na kwamba, maandamano ya Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha imani ya Kanisa juu ya uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai, tayari kuwalisha waja wake kwa chakula cha uzima wa milele. Ndiye yule yule Kristo Yesu aliyejitambulisha na maskini, wanyonge na wale waliosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, ndiye pia chemchemi ya Injili ya upendo, tayari kuleta mageuzi na hivyo kuwafanya kuwa ni wajenzi wa Ulimwengu mpya. Daima wakumbuke kwamba, kwa muda wa miaka 40 Waisraeli walitangatanga Jangwani, changamoto na mwaliko kwa waamini katika Ulimwengu mamboleo, kutoanguka na kutumbukia katika vishawishi vya watu wa Agano la Kale. Hispania haina budi kubaki katika shule inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu na upendo wa jirani; na shule ya ukarimu tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga utamaduni wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kama kielelezo cha shukrani na upendo na matokeo yake, Kristo Yesu anazima: Kiu ya upendo, haki, amani na furaha ya kweli, tayari kuwakirimia wengine Injili ya matumaini, wale wote waliovunjika na kupondeka moyo!

Jubilei ya Miaka 100 tangu Mtumishi wa Mungu Gaudi afariki dunia
Jubilei ya Miaka 100 tangu Mtumishi wa Mungu Gaudi afariki dunia   (@Vatican Media)

Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Mtumishi wa Mungu Antoni Gaudì Cornet alipofariki dunia. Kazi yake inayojulikana zaidi ni Kanisa la Malipizi ya Dhambi la “Sagrada Familia.” Antonio Gaudí Cornet, aliyezaliwa tarehe 25 Juni 1852, pengine huko Reus, alikubali kusimamia ujenzi wa Kanisa hili mwaka mmoja mara baada ya kuwekwa kwa jiwe la msingi, kunako mwaka 1883, akiwa na umri wa miaka 31. Tangu wakati huo na kuendelea, alijisadaka maisha yake yote kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa hili, Nyumba ya Ibada, ambapo alionesha ujuzi wake wa kisanii, hisia zake za maisha ya kiroho na kidini. Kanisa hili kubwa limebuniwa kama safari ya kiroho inayosimulia maisha, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Jiwe la msingi liliwekwa rasmi tarehe 19 Machi 1882 na kutabarukiwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI mwaka 2010 na kwamba, ujenzi wa Kanisa hili bado unaendelea, ili kuwakumbusha waamini kwamba, maisha ya Kikristo ni safari endelevu kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Mungu. Ni kielelezo cha umoja, amani na utulivu; Nyumba ya Mungu, mahali pa sala kwa wadhambi, Msalaba unakuwa ni ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Kristo Yesu akishainuliwa juu ya Msalaba, utu na heshima ya binadamu vinang’ara na kwamba, hii ni kazi ya imani na sanaa vinavyosimama pamoja. Kanisa hili ni: “Biblia pauperum” yaani “Biblia ya Maskini” inayobeba amana na utajiri mkubwa katika mchakato wa Uinjilishaji. Hili ni Kanisa refu kuliko Makanisa yote Ulimwenguni, dir ana mwongozo kwa watu wa Mungu wanaofanya hija ya maisha ya kiroho, huku wakiwa na taa zao mikononi wakimsubiri Bwana arusi. Baba Mtakatifu Leo XIV amebariki Mnara wa Kristo Yesu na baadaye aewabariki watu wa Mungu waliohudhuria katika Ibada hii ya Misa Takatifu.

Biashara haramu ya binadamu inasigina utu, heshima na haki msingi
Biashara haramu ya binadamu inasigina utu, heshima na haki msingi   (@Vatican Media)

Jumuiya ya Kimataifa katika ulimwengu mamboleo, inakabiliana na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu kutokana na: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kidini na kikabila. Kuna umaskini mkubwa wa hali na kipato; uhalifu unaofanywa na magenge ya kitaifa na kimataifa pamoja na kuendelea kuibuka kwa mifumo mipya ya utumwa mamboleo pamoja na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Yote haya ni mambo yanayonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Biashara ya binadamu na viungo vyake ni donda ndugu katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka wahusika wote wa biashara ya binadamu sanjari na mifumo yote ya utumwa mamboleo kutubu na kumwongokea Mungu na watambue kwamba, siku ya mwisho, watawajibika mbele ya Mwenyezi Mungu.

Hija ya Kitume Hispania
16 Juni 2026, 14:46