Mkutano Mkuu Maalum wa Baraza la Makardinali 26-27 Juni 2026. Mkutano Mkuu Maalum wa Baraza la Makardinali 26-27 Juni 2026.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV,Makardinali:Ninahitaji usaidizi wenu;ninaomba uwazi na uaminifu

Katika hotuba ya Papa Leo XIV katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu Maalum wa Makardinali kutoka ulimwenguni kote,Juni 26,aliomba asindikizwe nao katika huduma yake kwa Kanisa,ili kutambua ishara za matumaini zinazokua kimya kimya,lakini pia kutopuuza magumu, kutoelewana na upinzani ikiwa ni pamoja na nchi zilizo na alama ya vita,vurugu,mgawanyiko wa kijamii au kidini.Papa alitoa mwaliko wa kuwa wajenzi wa ushirika na kwamba huduma yake haiwezi kuifanya peke yake.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Ninawategemea mnisaidie kutambua kile ambacho Roho anasema kwa Kanisa leo. Ninahitaji usaidizi wenu: wenye nguvu, dhahiri, na wazi. Ninahitaji kuhisi unaungwaji mkono na ninyi kama ndugu. Ushirika si matokeo yanayopatikana mara moja na kwa wote: unabaki kuwa uongofu wa kila siku, ambao huchukua umbo katika sala na kupitia mitazamo thabiti, mahusiano ya uaminifu, na nia ya kusikilizana. Haya yamo ni maneno ya nguvu yaliyosikika mbele ya Makardinali 180 kutoka Ulimwenguni kote  waliokusanyika mjini Vatican kwa ajili ya Mkutano maalum wa Pili, mjini Vatican wa  upapa wa Baba Mtakatifu Leo XIV ulioanza asubuhi tarehe 26 Juni na utahitimisha tarehe 27. Na ambao  umegawanyika katika vikao vinne. Katika Hotuba ya kina ya Baba Mtakatifu kwenye Ukumbi wa Paulo XIV alianza mara baada ya utangulizi wa Kardinali  Giovanni Batista Re, Dekano wa Makardinali na ambao alizungumza namo mwaka mnamo Januari 2026.

Mkutano Mkuu wa Makardinali
Mkutano Mkuu wa Makardinali   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu alianza kuwakaribisha na kuwashukuru kwa “dhati kwa kukubali tena mwaliko wangu. Uwepo wenu unaonesha kujali kwa Kanisa lote tunaloshiriki katika kuwahudumia Watu wa Mungu na utume tuliokabidhiwa na Bwana.” Papa Leo aliongeza “Katika Mkutano Mkuu wa Januari iliyopita, nilielezea matashi rahisi: kwamba mikutano hii itusaidie kujifunza zaidi na zaidi "kufanya kazi pamoja katika huduma ya Kanisa" na kufuata "mazungumzo yatakayonisaidia katika kutumikia utume na Kanisa lote."

“Haya hayakuwa maneno ya utangulizi tu. Ninaendelea kuamini kwamba hili ni moja ya majukumu muhimu zaidi yaliyokabidhiwa Baraza la  Makardinali. Sisi pia, kama Kanisa lote, tunajifunza kwa kusafiri.” Ushirika si matokeo yanayopatikana mara moja na kwa wote: unabaki kuwa uongofu wa kila siku, ambao huchukua umbo katika sala na kupitia mitazamo thabiti, mahusiano ya uaminifu, na nia ya kusikilizana. Katika miezi ya hivi karibuni, nimekumbusha mara kwa mara kwamba tumeitwa kuwa wajenzi wa ushirika wa Kristo, ushirika unaojitokeza katika Kanisa la kisinodi ambapo wote wanashirikiana katika utume mmoja, kila mmoja kulingana na karama na huduma yake.

Kama nilivyosema kwa Baraza la Wawakilishi la Curia Romana, ushirika huu "unajengwa, zaidi ya  maneno na hati, kupitia ishara na mitazamo halisi ambayo lazima idhihirishwe katika maisha yetu ya kila siku, ikiwa ni pamoja na mahali pa kazi" (Hotuba kwa Baraza la Wawakilishi la Curia Romana,Salamu za Noeli, Desemba 22, 2025). Sisi si walinzi wa mambo maalum, bali "wanafunzi na mashahidi wa Ufalme wa Mungu, walioitwa kuwa katika Kristo chachu ya udugu wa ulimwengu wote.”

Kusali sala ya Uje Roho Mtakatifu
Kusali sala ya Uje Roho Mtakatifu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu aliendelea kusema kuwa “Kwa sababu hiyo, nimetamani kazi yetu izingatie mada nne zilizounganishwa sana: Kwanza, tunaalikwa kutafakari ulimwengu ambao Kanisa limeitwa kutangaza Injili. Kabla ya kujiuliza la kufanya, lazima tusimame kabla ya ukweli, tukiutazama kwa macho ya imani na kujiruhusu kuchangamotishwa kwa kuwasikiliza kaka na dada zetu. Kama nilivyokumbuka juma chache zilizopita, "Yesu hutembea mitaani, hupita katika viwanja, hutembelea vitongoji vyetu, na hukaa katika sehemu za maisha yetu ya kila siku, kama Mungu wa karibu anayetembea pamoja na watu wake, kama Bwana wa historia" (Mahubiri katika Uwanja wa  Cibeles, Madrid, 7 Juni 2026).

Na leo hii pia, Bwana anaendelea kututangulia katika historia, na Kanisa linaitwa kwanza kabisa kutambua uwepo wake. Baadaye, tutatafakari pamoja utamaduni wa nguvu na ustaarabu wa upendo. Papa Leo XIV aliongeza kusema kuwa “ Wengi wenu mnatoka katika nchi zilizo na vita, vurugu, mgawanyiko wa kijamii au kidini. Lakini hakuna hata mmoja wetu aliye salama kwa aina nyingi za migogoro, ukandamizaji, na mgawanyiko unaozikumba jamii zetu leo. Kwa sababu hiyo, utambuzi tunaoitwa kuufanya unawahusu kila mtu na unachangamotisha utume wa Kanisa katika kila muktadha. Waraka wa Magnifica Humanitas unatupatia funguo muhimu za kutafsiri wakati huu.” Papa Leo kwa hati yake alisema “ Ninavutiwa sana kusikia jinsi kurasa hizi zinavyogusa Makanisa yenu, ni maswali gani yanaulizwa, mitazamo gani inafunguliwa, na hatua gani zinapendekezwa. Waraka unaendelea na safari yake unapokaribishwa, kufasiriwa, na kujumuishwa katika maisha halisi ya Makanisa.”

Utangulizi wa Dekano wa Makardinali
Utangulizi wa Dekano wa Makardinali   (@Vatican Media)

Kipindi cha tatu kitachunguza zaidi Magnifica Humanitas,  kwa kuchunguza mchango ambao Kanisa linaweza kutoa katika kujenga wema wa wote. Tunaishi katika wakati ambapo kishawishi cha kugawanyika kinakua na maslahi fulani yanashinda kwa urahisi. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanatukumbusha kwamba wema wa wote haujitokezi kwa hiari, bali unahitaji uwajibikaji wa pamoja. Kwa Kanisa, hii inachukua umbo maalum sana: mtindo wa kisinodi katika huduma ya utume wa Ufalme. Waraka wa Magnifica Humanitas unakumbuka hili katika kifungu namba 86, ukiongeza kwamba hii inahitaji uangalifu kwa jinsi maamuzi yanavyofanywa na majukumu yanavyotekelezwa, kwa uwazi, tathmini, na uwajibikaji pamoja.

Hatimaye, tutatenga kikao kwa njia ya utekelezaji wa Sinodi. Kipindi hiki cha mwisho hakileti mada mpya, bali kinakusanya pamoja na kuunganisha kile tulichoshiriki katika vikao vilivyopita. Tukikabiliwa na majeraha ya ulimwengu, ujenzi wa manufaa ya wote, na utume wa Kanisa, sinodi inaonesha njia ya kusonga mbele: kusikiliza, kutambua, na kuchukua kwa pamoja jukumu la chaguzi ambazo Bwana anatukabidhi.

Wakati wa sala ya Roho Mtakatifu
Wakati wa sala ya Roho Mtakatifu   (@Vatican Media)

Sinodi si seti ya taratibu

Sinodi si seti ya taratibu kimsingi; kama nilivyosema mara nyingi, sinodi ni mtazamo, uwazi, na nia ya kuelewa. Wakati mwingine imetafsiriwa kama kupungua kwa mamlaka. Kiukweli, inatusaidia kuelewa kwa undani zaidi maana ya mamlaka yenyewe, ambayo ipo ili kulinda ushirika, kukuza ushiriki wa kila mtu, na kuongoza safari ya pamoja ya Kanisa. Vipindi hivi vinne vinapata umoja wao katika mtazamo wa kimisionari tulioshiriki katika Mkutano Mkuu uliopita ambayo nilikumbuka katika barua yangu Aprili iliyopita. Hatuko hapa kimsingi kutafakari maisha ya ndani ya Kanisa.”

Tunaweza kusasisha makanisa yetu leo ya kutangaza Injili na uaminifu?

Papa Leo XIV alieleza tena kwamba, “Mada zote tutakazozungumzia, mtazamo wetu wa ulimwengu, amani, wema wa wote, sinodi, yanaungana katika swali moja: tunawezaje kuyasaidia Makanisa yetu leo​​kutangaza Injili kwa uaminifu mkubwa, uhuru, na uaminifu? Utume si mojawapo ya kazi nyingi za Kanisa. Ni sababu yake ya kuwepo, na kwa sababu hiyo, pia inakuwa kigezo kinachoongoza utambuzi wetu. Tunapojifunza kusikilizana, kushiriki majukumu, kutambua utendaji wa Roho katika Makanisa tofauti, hatuboreshi tu njia yetu ya kufanya kazi: tunakuwa Kanisa lenye uwezo zaidi wa kukutana na wanaume na wanawake wa wakati wetu na kuwashuhudia furaha ya Injili.

Papa akisalimiwa na makardinali
Papa akisalimiwa na makardinali   (@Vatican Media)

Baba Matakatifu Leo XIV aliomba maombi kadhaa kwa Makardinali wake kuwa:  “ Kwa sababu hiyo, ningependa kuwaomba msaada maalum. Huduma ambayo Bwana amenikabidhi haiwezi kufanywa peke yangu. Inahitaji uzoefu wenu, hekima yenu ya kichungaji, ujuzi wenu wa Makanisa na watu waliokabidhiwa kwenu.” Baba Mtakatifu aliongeza “ "Ninawategemea mnisaidie kutambua kile ambacho Roho anasema kwa Kanisa leo. Ninahitaji msaada wenu: wenye nguvu, dhahiri, na wazi. Ninahitaji kuhisi ninaungwa mkono na ninyi kama ndugu." "Ninawaomba mnisindikize si katika siku hizi za kazi tu, bali pia katika huduma yangu ya kila siku kwa ushirika wa Kanisa la ulimwengu wote. Mnisaidie kusikiliza kile kinachojitokeza katika Makanisa, kutambua ishara za matumaini ambazo mara nyingi hukua kimya, lakini pia kutopuuza magumu, kutoelewana, na upinzani ambao unaweza kupunguza kasi ya safari."

Papa akisikiliza kwa makini
Papa akisikiliza kwa makini   (@Vatican Media)

"Ninahitaji uhuru wenu, uwazi wenu, na uaminifu wenu. Ushauri wa dhati daima ni kitendo cha ushirika."  Pia ninawaomba, kila mmoja katika Kanisa na huduma yake, muunge mkono mtindo huu wa utambuzi wa kikanisa. Ninajua unahitaji uvumilivu na wakati mwingine huibua maswali.” Katika hilo Papa aliongeza kusema: “Hata hivyo, nina uhakika kwamba Bwana anatufundisha njia ya kiinjili zaidi ya kuishi pamoja jukumu alilotukabidhi. Uaminifu wa ushuhuda wetu na matunda ya utume wetu pia hutegemea hili." Kwa hivyo ninawatia wa  moyo kuishi kazi ya kikundi kwa imani. Ninajua kwamba, kwa wengi wetu, hii si njia ya kawaida ya kuendesha Mkutano Mkuu.  Lakini hii pia ni sehemu ya njia ambayo Bwana anatuongoza.”

Papa akiingia ukumbini
Papa akiingia ukumbini   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV aliendelea “Kwa kawaida, pia kutakuwa na nafasi ya michango ya kibinafsi, na, kama kawaida, kila mtu anakaribishwa kushiriki kwa uhuru uchunguzi wake au tafakari za kibinafsi. Lakini ninawaomba muuingie katika zoezi hili la kikanisa kwa kujiamini. Sisi pia tunajifunza sinodi kwa kuifanyia mazoezi; tunajifunza pamoja ili kukua katika ushirika. Niwakushukuru mapema kwa upatikanaji wenu, kwa uhuru wenu wa ndani, na kwa upendo wenu kwa Kanisa. Tumkabidhi Roho Mtakatifu siku hizi, ili atufanye tuwe watiifu kwa sauti yake na atupe neema ya kutafuta pamoja kile kinachohudumia Injili na mema ya Watu wa Mungu.Asante.” Alihitimisha Papa.

Mkutano Mkuu wa Makardinali
Mkutano Mkuu wa Makardinali   (@Vatican Media)
PAPA KWA MAKARDINALI JUNI 26
26 Juni 2026, 13:05