Baba Mtakatifu Leo XIV: Baraza la Pili la Makardinali 26-27 Juni 2026
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Waraka wa Kitume wa Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Novemba 2013, unatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya. Waraka huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa siku za usoni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi. Waraka huu wa kitume unachota amana na utajiri wake katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza na kushuhudia imani ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko, akayasoma na kuyafanyia tafakari ya kina na hatimaye, kuyaweka kuwa ni sehemu ya ujumbe wake kwa Familia ya Mungu wakati huu inapojielekeza katika hija ya Uinjilishaji Mpya, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye kiini cha Uinjilishaji na ndiye Mwinjilishaji Mkuu. Wakristo wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe katika mazingira mapya ya uinjilishaji. Baba Mtakatifu Francisko katika mwono huu wa kimisionari ambao ndio msingi wa waraka huu wa kitume anaugawa sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni mwaliko kwa Makanisa mahalia kuangalia changamoto na fursa zilizopo mintarafu tamaduni na hali halisi ya nchi husika. Baba Mtakatifu Francisko anatoa kigezo kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu na kwa kila mdau wa uinjilishaji, ili kwa pamoja waweze kuibua mbinu shirikishi katika mchakato wa uinjilishaji pasi na kujitenga kama kisiwa!
Baba Mtakatifu Francisko anabainisha nguzo kuu saba za uinjilishaji zinazopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mwono wa Uinjilishaji Mpya: Mageuzi ndani ya Kanisa kwa kutambua kwamba, Kanisa kimsingi ni la Kimisionari; vishawishi vya Wainjilishaji, Kanisa kama Familia ya Mungu inayotumwa Kuinjilisha; Mahubiri na matayarisho yake; Ushiriki wa kijamii wa maskini katika maisha na utume wa Kanisa; Amani na majadiliano ya kijamii ni kiini cha kazi ya Uinjilishaji inayofanywa na Mama Kanisa. Yote haya yanafumbatwa kwa umakini mkubwa katika huruma na upendo mfunuliwa wa Mungu unaogusa moyo wa kila mtu kwa kukutana na Kristo Yesu, chemchemi ya furaha inayomsukuma mwamini kushirikisha upendo huu kwa wengine. Baba Mtakatifu Leo XIV katika Barua yake kwa Makardinali wote anasema, Waraka wa Kitume wa Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” ni “Kerygma” yaani rejea na chombo makini cha kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, Ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu. Huu ndio utimilifu wa imani ya Kanisa, ambapo Neno la Mungu linafanyika ushuhuda hai unaoongoza maisha na utume wa Kanisa. Mwongozo huu ni utambulisho wa maisha ya Kikristo na Kikanisa; tayari kuanzisha mchakato wa wongofu wa shughuli za kichungaji na kimisionari na hivyo kuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, huu ni mwaliko kwa kila mbatizwa kupyaisha uhusiano wake na Kristo Yesu, kwa kuboresha maisha ya sala, kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji; kwa kujenga na kudumisha Kanisa la kimisionari, mahali pa watu kukutana katika umoja, upendo na ukarimu; kwa kujenga utamaduni wa kusikilizana, kusindikizana; toba, wongofu wa ndani pamoja na uponyaji.Jambo la msingi anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ni kuzingatia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujikita katika: Ushuhuda, majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; Kanisa linapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya matumaini, tayari kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa walimwengu. Waraka wa Kitume wa Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” unakazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa Sakramenti za kuingizwa katika Ukristo: Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu zinazoweka misingi ya maisha yote ya Kikristo, kwa kushiriki hali ya kimungu, kwa kujenga uhusiano na kuimarishwa kwa Sakramenti za Kanisa. Anakazia umuhimu wa ziara za kitume na kichungaji ziwe ni mahali muafaka pa maboresho ya uhusiano, maisha na utume wa kimisionari.
Wakati huo huo, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, katika barua yake kwa Makardinali amewaalika kujikita katika mambo makuu matatu: Hali ya Kimataifa, haki na amani; Dhana ya "vita ya haki" (Just War Theory) inazidi kupitwa na wakati katika ulimwengu mamboleo ambapo uharibifu mkubwa, uwepo wa silaha za maangamizi ni mambo yanayofanya uhalalishaji wa vita kuwa ni mgumu. Makardinali watakuwa na fursa ya kujadili Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde.” Kikao cha kwanza kinaongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV. Baraza la Makardinali ni fursa ya kushirikishana, kusikiliza, kusali na kutoa maamuzi ya pamoja mintarafu: Mchakato wa uinjilishaji mpya; Utamaduni wa nguvu na upendo wa kiraia; Utu wa kupendeza; Ujenzi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hatimaye ni mchakato wa utekelezaji wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV atatoa hotuba yake kama hitimisho na tarehe 29 Juni 2026 ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.
