Ni katika muktadha wa Inter Milan kubeba ubingwa wa 21 wa “Serie A” nchini Italia baada ya kuwachapa Parma bao 2-0 na hivyo kutwaa Ubingwa wa Italia kwa mwaka 2025-2026 "Serie A" Ni katika muktadha wa Inter Milan kubeba ubingwa wa 21 wa “Serie A” nchini Italia baada ya kuwachapa Parma bao 2-0 na hivyo kutwaa Ubingwa wa Italia kwa mwaka 2025-2026 "Serie A"  (AFP or licensors)

Papa Leo XIV Umuhimu wa Michezo Katika Jamii: Mashuhuda wa Tunu Msingi za Kijamii

Ushindi wa Inter Milan ni matunda ya ushiriki na mchezo wa timu; nidhamu na udumifu, ili kuweza kufurahia ushindi. Hii ni fursa anasema, Papa Leo XIV kwa wachezaji kutafakari wakati huu wa kusherehekea ushindi wao, ujumbe ambao wangependa kuuwasilisha hususan miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kwani vijana wengi wanawaona wachezaji wa Inter Milan, kama mashuhuda wao na mifano bora ya kuigwa, mambo yanayowataka kuwajibika barabara katika utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, michezo, shule ya maisha na ya kisasa mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na walezi katika maisha na kazi; Ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, Mama Kanisa anaona michezo kama fursa ya kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha kama vile: Udugu wa kibinadamu, mshikamano na amani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema mapumziko yatumike kuimarisha afya ya kiroho na kimwili na kwamba, michezo pia inaweza kuimarisha, kustawisha na kukuza mahusiano ya kidugu kati ya wanadamu wa hali zote, mataifa na makabila mbalimbali. Kumbe, wakristo wanahimizwa kushiriki katika michezo, huku ikikolezwa na roho ya kiutu na ya kikristo. Rej. Gaudium et spes, n.61.

Wana michezo wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za kijamii
Wana michezo wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za kijamii   (ANSA)

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Mama Kanisa amekazia pia umuhimu wa michezo, utamaduni na elimu na kwamba, michezo ni lugha inayofahamika na wengi na kikolezo cha watu kukutana; kujadiliana na kwamba, bado kuna mengi ya kujifunza kutoka katika tamaduni za watu mbalimbali, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni. Michezo na maendeleo binafsi: Michezo ni chanzo cha furaha, mahali mtu anapoweza kujieleza kutoka katika undani wake; ni mahali pa kuonesha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali uchoyo na ubinafsi, kwa kujielekeza katika mafao ya wengi; michezo inatoa fursa ya watu kukutana na hivyo kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu; ni mahali pa kuratibu kinzani na migogoro, kwa kusameheana na kusahau. Makocha wanayo kazi na dhamana nyeti katika kujenga umoja kama timu, kati ya wachezaji. Michezo inamwendeleza mtu mmoja mmoja sanjari na kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii; kumbe michezo lazima ijitahidi kuwalenga watu wote ndani ya jamii, kwani ni sehemu muhimu sana ya maendeleo ya binadamu.

Wanamichezo wawe ni mifano bora ya kuigwa na vijana wa kizazi kipya
Wanamichezo wawe ni mifano bora ya kuigwa na vijana wa kizazi kipya   (ANSA)

Ni katika muktadha wa Timu ya Inter Milan kubeba ubingwa wa 21 wa “Serie A” nchini Italia kwa mwaka 2025-2026 baada ya kuwachapa Parma bao 2-0 na hivyo kupata fursa ya viongozi wa timu na wachezaji wa Inter Milan na mashabiki kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican Jumamosi tarehe 9 Mei 2026, walioonesha furaha ya pekee ambayo hata Baba Mtakatifu alishiriki pamoja nao. Haya ni matunda ya ushiriki na mchezo wa timu; nidhamu na udumifu, ili kuweza kufurahia ushindi. Hii ni fursa anasema, Baba Mtakatifu kwa wachezaji hawa kutafakari kwa kina na mapana, wakati huu wa kusherehekea ushindi wao, ujumbe ambao wangependa kuuwasilisha kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Italia, hususan miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kwani vijana wengi wanawaona wachezaji wa Inter Milan, kama mashuhuda wao na mifano bora ya kuigwa, mambo yanayowataka kuwajibika kikamilifu, kama mashuhuda wa tunu msingi za kijamii, kwani vijana wengi wanayo kiu na hamu ya kuwa na mifano bora ya kuigwa katika maisha yao na kwamba, kama wachezaji wanaweza kuwa ni mifano bora ya kuigwa na hata wakati mwingine mifano ya watu wa ovyo katika maisha ya vijana. Kumbe, wanapaswa kuwajibika barabara ili kweli waweze kuwa ni mifano bora ya kuigwa na vijana wa kizazi kipya! Mtakatifu Yohane Paulo II miaka thelathini iliyopita aliwakumbusha viongozi na wachezaji wa Inter Milan historia ya Soka nchini Italia na umuhimu wake na kuwataka kuhakikisha kwamba, watu wengi wanaweza kutambua ndani mwa ona katika tabia yao uhalisi na uadilifu usioyumba wala kutiliwa shaka. Na huu anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ndiyo matashi mema ambayo anapenda kuwaachia viongozi na wachezaji wa Inter Milan.

Papa Leo XIV Michezo
11 Mei 2026, 14:38