Bodi ya Wakurugenzi wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Nchini Marekani, Jumatatu tarehe 4 Mei 2026 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican Bodi ya Wakurugenzi wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Nchini Marekani, Jumatatu tarehe 4 Mei 2026 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican   (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV: Tangazeni Injili ya Upendo Kwa Njia ya Huduma Kwa Maskini

Bodi ya Wakurugenzi wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Nchini Marekani, Jumatatu tarehe 4 Mei 2026 imekutana na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican. Huu ni muda wa sala na tafakari ya kina pamoja na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro, hali ambayo kimsingi inawasogeza karibu katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, ili kuwashirikisha wengine ile Injili ya upendo, inayomwilishwa katika huduma makini kwa watu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Nchini Marekani “Catholic Charities USA (CCUSA) ni muungano wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kutoka katika Majimbo 169 nchini Marekani yanayosimama kidete kupambana na baa la umaskini linalosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hili ni Shirikisho linalowahudumia watu wa Marekani bila ubaguzi wa aina yoyote. Shirikisho hili pia ni mwanachama wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis. Ni katika muktadha huu, Bodi ya Wakurugenzi wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Nchini Marekani “Catholic Charities USA (CCUSA), Jumatatu tarehe 4 Mei 2026 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican ilipomtembelea.

Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu
Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu   (@VATICAN MEDIA)

Huu ni muda wa sala na tafakari ya kina pamoja na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa umoja na ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro, hali ambayo kimsingi inawasogeza karibu katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, ili kuwashirikisha wengine ile Injili ya upendo, inayomwilishwa katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, Kristo Yesu daima yuko pamoja na waja wake hadi utimilifu wa dahari. Rej. Mt 28:20.

Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili
Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amegusia kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo katika kutoa huduma kwa maskini na kwamba, upendo wa Kristo Yesu unawabidisha, kuwashirikisha maskini ile furaha ya Injili na hivyo kuwa ni fursa ya kukutana na Kristo Yesu ambaye daima yuko pamoja nao! Kumbe, matumaini ya Fumbo la Pasaka yawe ni dira na mwongozo wao katika huduma kwa maskini! Kanisa la Mwanzo lilikita mizizi yake katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wahitaji zaidi. Wakakumbana na changamoto kama mtu binafsi na kama taasisi na kwamba, huduma hii ulikuwa ni utambulisho wao wa Kikristo na kwamba, hawawezi kukatishwa tamaa pamoja na changamoto na matatizo wanayokumbana nayo katika kutoa huduma, kwani Kristo Yesu amewahakikishia uwepo wake endelevu na angavu hadi utimilifu wa dahari.  

Msiogope, Kristo Yesu yuko daima kati pamoja na waja wake
Msiogope, Kristo Yesu yuko daima kati pamoja na waja wake   (@VATICAN MEDIA)

Hata katika ulimwengu mamboleo, bado Kristo Yesu anaendelea kusindikizana na waja wake kama alivyofanya kwa Mtakatifu Thoma na wale wanafunzi waliokuwa njiani kurejea Emau. Rej. Yn 20: 24-29; Lk 24:13-35. Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru wajumbe hawa na kuwatia shime kuendeleza utume wao unaofumbatwa katika huruma kwa maskini na wanyoge zaidi, kwa kutafuta suluhu zitakazowainua wale wanaoteseka kama Mtu binafsi na kama familia, ili kuwasaidia kubeba mzigo huu ambao ni mzito, lakini watambue kwamba, upendo wa Kristo unawabidisha. Rej. 2Kor 5:14. Ni katika upendo wa kweli watapata utulivu na utu wao kuheshimiwa. Upendo kwa Mungu na jirani unawawezesha waamini kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao, tayari kuwashirikisha maskini ile furaha ya Kristo Mfufuka na hivyo kukutana naye mubashara, tayari kujenga uhusiano wa dhati na Kristo Yesu ambaye yuko pamoja na kati yao. Rej. Mt 28:20. Kristo Mfufuka anawajalia amani, matumaini na maisha mapya, huku akifanya yote mapya. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, katika huduma yao kwa maskini wanaongozwa na matumaini ya Pasaka. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewatakia utume mwema na kwamba, ataendelea kuwasinikiza kwa sala zake na hatimaye, kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Msimamizi na Mwombezi wa Marekani.

Papa Leo XIV Injili ya Upendo
04 Mei 2026, 15:42