2026.05.02 Papa alikutana na wajumbe wa  Mfuko wa Kipapa. 2026.05.02 Papa alikutana na wajumbe wa Mfuko wa Kipapa.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV,Mfuko wa Kipapa:Hata leo hii Bwana anataka muwe vyombo vya amani

Katika Mkutano mjini Vatican,Mei 2 na Wajumbe wa Mfuko wa Kipapa Papa Leo XIV alitoa shukrani za dhati kwa shirika hilo ambalo kwa miaka 38 limeunga mkono mipango kwa ajili ya maskini katika sehemu mbalimbali duniani na"kushiriki katika ujumbe wa kuinjilisha wa Kanisa.Mapadre wengi watawa pia wameweza kupata elimu ya juu kutoka Vyuo Vikuu vya Kipapa jijini Roma ambayo vinginevyo isingewezekana na hivyo kuwaandaa kuwa viongozi wa baadaye katika Kanisa."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV alihutubia wasimamizi, wajumbe wa bodi ya wakurugenzi na wanachama wa Mfuko wa Kipapa, Jumamosi tarehe 2 Mei 2026 mjini Vatican. Kama kawaida alianza na ishara ya Msalaba na kuwatakia amani, akiwakaribisha kwa furaha na kuwatakia heri njema ya Hija yao jijini Roma na Vatican. Ingawa hii ni mara ya kwanza kukutana tangu alipopewa kuchukua nafasi ya Askofu wa Roma na Papa, Baba Mtakatifu alithibitisha kuwa  alikuwa  tayari ametambua kazi yao, hasa wakati wa miaka yake  ya huduma kama Askofu wa Chiclayo. “Mimi binafsi nilishuhudia matokeo chanya ya michango ya Mfuko huo kwani majimbo na  jumuiya za kidini zilibarikiwa na usaidizi kwa mipango mbalimbali kutokana na ukarimu wenu.”

PICHA YA PAMOJA YA WANACHAMA WA MFUKO WA KIPAPA
PICHA YA PAMOJA YA WANACHAMA WA MFUKO WA KIPAPA   (@Vatican Media)

"Nimekuwa nikiwatia moyo ili mfuko ufike duniani kote"

“Katika mwaka huu wa kwanza wa upapa wangu, Papa aliendelea “nimekuwa nikitia moyo kuona ufikiaji wa Mfuko duniani kote. Kwa hivyo ninashukuru sana kwa kujitolea kwenu kuendelea kumsaidia Mrithi wa Petro katika dhamira yake ya kujali mahitaji ya Kanisa la ulimwengu.” Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa katika suala hilo alifurahi kujua kwamba wanachama wa Mfuko huo wanaendelea kuongezeka kila mwaka na kwamba wameonesha nia yao ya kuongeza msaada wao na kutafuta njia mpya za kusaidia.

Kutangaza Injili leo hii,kupitia matendo na kujitoa kwa upendo

Ziara yao imefanyika wakati wa kipindi cha Pasaka, wakati unaozingatia utume na amani. Baada ya Ufufuko, Yesu aliwakabidhi mitume kazi ya kuwa wajumbe wake, akiahidi kusindikizana nao katika kazi yao na kuwa nao siku zote(Mk 16, 20; Mt 28, 20). Papa na maaskofu, kama warithi wa mitume, wanaendeleza ahadi hii kupitia mahubiri na kazi za uinjilishaji. Lakini washiriki wote wa Kanisa, kwa nguvu ya Ubatizo wao, wanashiriki jukumu la kutangaza Injili leo kupitia maneno na pia kupitia matendo ya kujitoa katika upendo. Kama Mtakatifu Yakobo alivyoandika kwa jumuiya ya Wakristo wa kwanza, imani bila matendo imekufa na haina nguvu ya kuokoa(Yakobo 2:17), na Injili zinatufundisha kwamba Bwana anatarajia wanafunzi wake kutunza mahitaji ya maskini na walio katika mazingira magumu zaidi(Mt 25, 31-46).

MKUTANO WA PAPA NA WANACHAMA WA MFUKO WA KIPAPA
MKUTANO WA PAPA NA WANACHAMA WA MFUKO WA KIPAPA   (@Vatican Media)

Ufadhili wa masomo kwa mapadre na watawa Ulimwenguni

Kwa kufadhili mipango, misaada ya kibinadamu, na ufadhili wa masomo kwa watu ulimwenguni kote, Mfuko wa Kipapa unashiriki katika utume unaoendelea wa kiinjili wa  Kanisa. Ukarimu wao umewawezesha watu wengi kupata uzoefu halisi wa fadhili na wema wa Mungu katika jumuiya zao. Mapadre wengi na wanaume na wanawake waliowekwa wakfu pia wameweza kupata elimu ya juu kutoka Vyuo Vikuu vya Kipapa  jijini  Roma ambayo vinginevyo isingewezekana, na hivyo kuwaandaa kuwa viongozi wa baadaye katika Kanisa. “Huenda Msiwahi kukutana na wale wote ambao wamefaidika na wema waenu,”-  kwa hivyo kwa niaba yao,  Papa Leo XIV alitoa  shukrani “zangu za dhati.”      Na zaidi Papa alionesha furaha kubwa kwamba mmoja wapo wa wale waliopokea ufadhili wa masomo alikuwa amekaa karibu naye.

PAPA NA WAJUMBE WA MFUKO WA KIPAPA
PAPA NA WAJUMBE WA MFUKO WA KIPAPA   (@Vatican Media)

"Hata leo hii Kristo anatamamani wanafunzi wake wawe vyombo vya amani"

Siku ya Dominika ya Pasaka, Bwana aliyefufuka aliwasalimia mitume wake kwa maneno, "Amani iwe nanyi!" (Yh 20:19), na hata leo hii, Kristo anatamani wanafunzi wake wawe vyombo vya amani. Mbali na kuhamasisha utume wa kiinjili wa Kanisa, kujitolea kwa Mfuko, pia husaidia kuhamasisha amani katika ngazi za kikanda na za  mahalia. Mtakatifu Paulo VI, aliandika kwamba “jina jipya la amani ni maendeleo,”(Waraka wa Popolorum progressio, n. 87).  Kwa hiyo Papa aliongeza kusema, alimaanisha kwamba “maelewano ya kweli si kutokuwepo kwa migogoro tu, bali hutokana na kuhamasisha maendeleo halisi ya binadamu (Popolorum progressio n. 76).

Kuhamasisha maendeleo fungamani kuptia mipango inayoungwa mkono na mfuko wa kipapa

Kuhamasisha maendeleo fungamani kupitia mipango inayoonekana kama ile inayoungwa mkono na Mfuko  ni njia ya uhakika ya kuhimiza maelewano miongoni mwa jamii na watu binafsi. Kwa hiyo kwa hisia hizo Papa Leo XIV aliwashukuru kwa uwepo wao siku hiyo na kwa yote wanayofanya ili “kuhamasisha utume unaostahili sifa wa Mfuko wa Kipapa.” Alikongeza kusema “Ninaomba maombi yenu ya kila mara kwa ajili ya huduma yangu kama Mrithi wa Mtakatifu Petro na kwa mahitaji ya Kanisa.” Kwa kuwakabidhi wao  na wapendwa wao kwa maombezi ya upendo ya Maria, Mama wa Kanisa, kwa hiari yake,   Baba Mtakatifu Leo XIV alitoa Baraka yake ya Kitume kama ahadi ya furaha katika Kristo Bwana wetu Mfufuka.

PAPA NA WANACHAMA MFUKO WA KIPAPA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

02 Mei 2026, 16:05