Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kusema kwamba, Barani Afrika kuna vita, kinzani na migogoro kutokana na: Ukosefu wa usawa, vitendo vya kigaidi sanjari na misimamo mikali ya kidini na kiimani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kusema kwamba, Barani Afrika kuna vita, kinzani na migogoro kutokana na: Ukosefu wa usawa, vitendo vya kigaidi sanjari na misimamo mikali ya kidini na kiimani.  (ANSA)

Papa Leo XIV: Majadiliano ya Kidini ni Sehemu ya Vinasaba Vya Maisha na Utume wa Kanisa

Papa Leo XIV anasikitika kusema kwamba, Barani Afrika kuna vita, kinzani na migogoro kutokana na: Ukosefu wa usawa, vitendo vya kigaidi sanjari na misimamo mikali ya kidini na kiimani, & wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, hotuba za chuki na uhasama; udini na ukabila mambo yanayoendelea kumong’onyoa tunu msingi za maadili, maisha ya kiroho na utu wema, hasa miongoni mwa vijana. Kumbe, majadiliano ya kidini ni chombo muafaka kwa taifa na kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka 60 iliyopita walitoa tamko kuhusu majadiliano ya kidini kwa watu wa nyakati hizi linalojulikana kama “Nostra Aetate." Hili ni tamko linalokazia pamoja na mambo mengine: Dhamana ya Kanisa katika kuhamasisha umoja na upendo kati ya watu wa Mataifa; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kusimama kidete kutangaza na kushuhudia pamoja utu na heshima ya binadamu. Kanisa Katoliki linatambua mambo ya kweli na matakatifu katika dini mbalimbali, lina heshimu na kuthamini namna yao ya kutenda na kuishi; sheria na mafundisho yao. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, Kanisa litaendelea kutangaza kwamba: Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima na ambaye ndani mwake mwanadamu anapata utimilifu wa maisha ya utauwa na upatanisho kati yake na Mwenyezi Mungu. Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; ustawi na mafao ya wengi. Kanisa linatambua kwamba, bado kuna changamoto nyingi na vikwazo vya kufanyiwa kazi, lakini hadi hapa linapenda kumshukuru Mungu kwa jiitihada zilizokwisha kufikiwa katika medani mbalimbali za maisha. Katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Mama Kanisa anaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali kufahamiana, kuheshimiana na kushirikiana kwa dhati katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Jumuiya ya Waamini wa dini ya Kiislam walipokutana na Papa Leo XIV
Jumuiya ya Waamini wa dini ya Kiislam walipokutana na Papa Leo XIV   (ANSA)

Ikumbukwe kwamba, majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji, linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani.Waamini wanaweza kujenga na kudumisha umoja, udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii kwa kusaidiana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Mama Kanisa anakazia: Umuhimu wa watu kuishi katika umoja, upendo na mshikamano kwa sababu majadiliano ya kidini, udugu wa kibinadamu, haki na amani ni mambo msingi ya maisha ya watu wa Mungu. Kwa njia ya majadiliano ya kidini, watu wanakutana, wanazungumza, wanafahamiana na hivyo kuanzisha mchakato wa kutembea bega kwa bega kama ndugu wamoja. Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuwa ni shuhuda na chombo cha amani, kwa kufyekelea mbali yale yote yanayosababisha: chuki, kinzani na mipasuko ya kidini na kiimani.

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Nchini Algeria
Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Nchini Algeria   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa majadiliano ya kidini, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 9 Mei 2026 amekutana na kuzungumza na wakuu pamoja na wawakilishi wa Jumuiya ya Waamini wa Dini ya Kiislam kutoka Senegal, waliomtembelea mjini Vatican kwa lengo la kujizatiti zaidi katika ujenzi wa urafiki wa kijamii, dhamana na jitihada ya kudumisha jamii shirikishi inayosimikwa katika msingi wa haki, amani na maridhiano sanjari na udugu wa kibinadamu. Senegal kama inavyojulikana na wengi ni nchi ya “Teranga” yaani hii ni nchi ya upendo, ukarimu na mshikamano; nchi ambayo inakita mizizi yake katika mafungamano ya kifamilia, amani na utulivu, kati ya waamini wa dini mbalimbali nchini humo. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, huu ndio msingi wa majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini na tamaduni mbalimbali. Huu ni udugu unaopaswa kulindwa na kudumishwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Senegal na ulimwengu katika ujumla wake.

Jamii inahitaji diplomasia na majadiliano ya kidini
Jamii inahitaji diplomasia na majadiliano ya kidini   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kusema kwamba, Barani Afrika kuna vita, kinzani na migogoro kutokana na: Ukosefu wa usawa, vitendo vya kigaidi sanjari na misimamo mikali ya kidini na kiimani, bila kusahau wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika; hotuba za chuki na uhasama; udini na ukabila ni mambo yanayoendelea kumong’onyoa tunu msingi za maadili, maisha ya kiroho na utu wema, hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Kumbe, majadiliano ya kidini ni chombo muafaka kwa taifa kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho na kwamba, siasa na diplomasia ni mambo yanayoweza kuchota amana na utajiri wake kutoka katika tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kujenga utamaduni unaoheshimu na kuthamini tofauti msingi ndani ya jamii.

Papa Leo XIV: Walimwengu wanahitaji diplomasia na majadiliano ya kidini
Papa Leo XIV: Walimwengu wanahitaji diplomasia na majadiliano ya kidini   (@Vatican Media)

Ulimwengu mamboleo anasema Baba Mtakatifu Leo XIV unahitaji diplomasia na majadiliano ya kidini yanayosimikwa katika msingi wa haki, amani, ukweli na uwazi, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja wana haki na usawa mbele ya Mungu, Muumbaji. Jumuiya ya Kimataifa imetangaza kwamba, wanadamu wote wamezaliwa huru na wako sawa katika utu na haki. Ni katika muktadha huu wa udugu wa kibinadamu, katika chimbuko la la ubinadamu na imani, ndipo linalopazaliwa jukumu la pamoja la kukemea kila aina ya ubaguzi na mateso mintarafu misingi ya ubaguzi wa rangi, dini au asili ya mtu; kukataa kila matumizi mabaya ya jina la Mwenyezi Mungu kwa malengo ya: kijeshi, kiuchumi au kisiasa; kupaaza sauti ya kinabii kwa ajili ya watu wanaoteseka. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Ole wao wanaogeuza dini na jina la Mwenyezi Mungu kwa malengo binafsi wakiburuta kile kilicho kitakatifu na kukitumbukiza kwenye uchafu na giza! Baba Mtakatifu Leo XIV anamwomba Mwenyezi Mungu asaidie kuchipua ndani ya nyoyo za watu ile hamu ya watu kutaka kufahamiana; kujenga utamaduni wa kusikilizana, kwa kuishi pamoja, huku wakiheshimiana na kuthaminiana kama sehemu ya ujenzi wa udugu wa pamoja. Mwenyezi Mungu awajalie waja wake ujasiri wa kukita maisha yao katika majadiliano ya kidini, udugu wa kibinadamu na kuendelea kuthamini tofauti zao msingi kama utajiri na amana, inayowahamasisha kujizatiti katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika msingi wa haki, amani na maridhiano kama sehemu ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu; mambo yanayoweza kuzaa matunda mengi ya ushirikiano kati ya watu wenye tofauti msingi!

Papa Leo XIV Majadiliano ya Kidini
11 Mei 2026, 15:21