Tarehe 26 Aprili 2026 Dominika ya Mchungaji Mwema;  Siku ya 63 ya Kuombea Miito Duniani inanogeshwa na kauli mbiu "Utambuzi wa ndani wa zawadi ya bure ya Mungu inayochanua ndani kabisa ya mioyo yetu." Tarehe 26 Aprili 2026 Dominika ya Mchungaji Mwema; Siku ya 63 ya Kuombea Miito Duniani inanogeshwa na kauli mbiu "Utambuzi wa ndani wa zawadi ya bure ya Mungu inayochanua ndani kabisa ya mioyo yetu."  (@Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Leo XIV Siku ya 63 ya Kuombea Miito Duniani 2026

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV wa Siku ya 63 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa kwa Mwaka 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: "Utambuzi wa Zawadi ya Bure ya Mungu Inayochanua Ndani Kabisa ya Mioyo Yetu. Dominika ya Nne ya Kipindi Cha Pasaka inajulikana kama "Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema." Dominika tarehe 26 Aprili 2026 Papa Leo XIV anatoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 8 kutoka Jimbo Kuu la Roma. Hii ni Siku ya Miito.

BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA, - DAR ES SALAAM.

Ndugu wapendwa, wapendwa vijana! Tukiongozwa na kulindwa na Yesu Mfufuka, tunaadhimisha katika Dominika ya Nne ya Pasaka, ambayo pia huitwa “Dominika ya Mchungaji Mwema” Siku ya 63 ya Kuombea Miito Duniani. Hii ni fursa ya neema ambapo tunashiriki tafakari juu ya undani wa wito, unaoeleweka kama utambuzi wa zawadi ya bure ya Mungu inayochanua ndani kabisa ya mioyo yetu. Hebu tuchunguze pamoja njia ya kweli iliyo nzuri ya maisha ambayo Mchungaji anatuongoza. Njia ya uzuri: Katika Injili ya Yohane, Yesu anajieleza kuwa “Mchungaji mwema” (Yn 10:11). Kauli hii inahusu mchungaji mkamilifu, halisi na wa mfano, kwa kuwa yuko tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake, kwa jinsi hiyo akidhihirisha upendo wa Mungu. Yeye ndiye Mchungaji anayetuleta karibu naye, ambaye muono wake unadhihirisha kwamba maisha ni mazuri kweli tunapomfuata. Si macho ya mwili wala hisia za uzuri peke yake zinazoweza kutambua uzuri huu; bali tafakari ya kina na maisha ya ndani yanahitajika. Ni yule tu anayetulia, kusikiliza, kusali na kukaribisha mtazamo wa Mchungaji ndiye anaweza kusema kwa ujasiri: “Namwamini; maisha pamoja naye yanaweza kuwa mazuri kweli. Nataka kutembea katika njia hii ya uzuri.” Kilicho cha pekee zaidi ni kuwa, katika kuwa mfuasi wake, mmoja anakuwa kweli “mzuri”, uzuri wake unatubadilisha. Kama Mwanataalimungu Pavel Florenskij alivyoandika, maisha ya ukaa-pweke hayazai tu mtu ‘mwema’ bali mtu ‘mzuri’. Kwa hakika, zaidi ya wema, sifa ya pekee ya mtakatifu ni uzuri wa kiroho unaong’aa kutoka katika maisha yake ndani ya Kristo. Kwa njia hii, wito wa Kikristo unajidhihirisha katika kina chake chote kama kushiriki katika maisha ya Yesu, kwa kushiriki utume wake na kuakisi uzuri wake.

Dominika ya NNe ya Pasaka, Dominika ya Mchungaji Mwema
Dominika ya NNe ya Pasaka, Dominika ya Mchungaji Mwema   (@VATICAN MEDIA)

Uzoefu huu wa ndani wa maisha, imani na maana ulikuwa pia wa Mtakatifu Augustino, ambaye, katika Kitabu cha Tatu cha Maungamo, hali akitambua dhambi na madhaifu ya ujana wake, anamtambua Mungu kuwa “yuko ndani zaidi kuliko sehemu yake ya ndani kabisa.” Zaidi ya kujitambua binafsi, Augustino anagundua uzuri wa nuru ya kimungu inayomwongoza katika giza. Kwa kutambua uwepo wa Mungu katika vyanzo vya ndani kabisa ya roho yake, hatimaye alifahamu umuhimu wa kutunza maisha ya ndani kama mahali pa kukutana na Kristo, ambayo ni njia ya kuguswa na uzuri na wema wa Mungu katika maisha yetu wenyewe. Mahusiano ya aina hiyo yanajikita katika sala na ukimya, na yanapopaliliwa yanatufungua kupokea na kuitikia kwa uhai kwa zawadi ya wito. Si jambo la kulazimisha katu au kipimo kimoja kitoshacho kwa wote ambapo kila mmoja anakubaliana tu, bali, ni fursa ya kuutambua upendo na furaha. Hivyo, katika msingi wa kuthamini maisha ya ndani, tunapaswa kuanza mara moja utume wetu na kuhuisha ari yetu ya uinjilishaji. Kwa muono huu, ninamualika kila mmoja – katika familia, parokia, jumuiya za kitawa, hali kadhalika maaskofu, mapadre, mashemasi, makatekista, waalimu na waamini wote – kuwajibika kikamilifu katika kutengeneza mazingira yanayowezesha zawadi ya Mungu kukumbatiwa, kustawishwa, kulindwa na kusindikizwa, ili iweze kuzaa matunda mengi. Ni pale tu mazingira yetu yanapoangaziwa kwa imani hai, kutegemezwa kwa sala za daima na kutajirishwa na kuambatana kwa kindugu ndipo wito wa Mungu huchanua na kukomaa, na kuwa njia ya furaha na wokovu kwa ajili ya watu na ulimwengu. Kwa kushika njia ambayo Yesu, Mchungaji Mwema, anatuonesha, twaweza kujifahamu kwa undani zaidi kadhalika kumfahamu Mungu ambaye anatuita.

Hii ni Siku ya Kutoa Daraja Takatifu ya Upadre
Hii ni Siku ya Kutoa Daraja Takatifu ya Upadre   (@Vatican Media)

Ufahamu Unaotegemeana: “Bwana wa uzima anatufahamu na anaangaza mioyo yetu kwa jicho lake la upendo.” Hakika, kila wito unaanza na ufahamu na utambuzi wa Mungu ambaye ni upendo (rej.1Yoh. 4:16). Yeye anatufahamu fika; amehesabu nywele za vichwa vyetu (rej. Mt 10:30) na amepanga kwa ajili ya kila mmoja njia ya pekee ya utakatifu na utumishi. Bado ufahamu huu lazima uwe daima wa kutegemeana. Tunaalikwa kumfahamu Mungu kwa njia ya sala, kusikiliza Neno, Sakramenti, maisha ya Kanisa na matendo mema kwa kaka na dada zetu. Kama kijana Samweli, ambaye pasipo kutegemea alisikia sauti ya Bwana wakati wa usiku na akajifunza kuitambua kwa msaada wa Eli (rej. 1 Sam 3:1-10), nasi pia tunahitaji kutengeneza nafasi ya ukimya wa ndani ili kusikia kile ambacho Bwana anataka kwa ajili ya furaha yetu. Hili sio suala la maarifa ya juu au majifunzo ya kitaaluma, bali ni kukutana binafsi kunakobadilisha maisha ya mtu. Mungu anakaa ndani ya mioyo yetu. Wito unajumuisha mazungumzano ya ndani pamoja Naye ambaye anaita na anatualika tuitikie, pasipo kujali kelele za kiulimwengu ziletazo uziwi, kwa furaha halisi na ukarimu. “Msiende nje yenu wenyewe; rudini ndani yenu. Ukweli unakaa katika nafsi ya ndani.” Tena, Mtakatifu Agustino anatukumbusha jinsi ilivyo muhimu kujifunza kutulia na kutengeneza nafasi kwa ajili ya ukimya wa ndani, ili tuweze kusikia sauti ya Kristo. Wapendwa Vijana, isikilizeni sauti hii! Isikilizeni sauti ya Bwana anayewaalika katika maisha yaliyo kamili na yenye kuzaa matunda, anayewaita kuzitumia talanta zenu (rej. Mt 25:14-30) na kuunganisha mapungufu na madhaifu yenu pamoja na msalaba mtukufu wa Kristo. Hivyo, tenga muda, kwa ajili ya kuabudu Ekaristi; kutafakari kiaminifu juu ya Neno la Mungu, ili muweze kuliweka katika matendo kila siku; na kushiriki kwa uhai na ukamilifu katika maisha ya kisakramenti na kikanisa ya Kanisa. Kwa namna hii, mtaweza kumfahamu Bwana. Katika ukaribu wa urafiki wake, mtatambua namna ya kujitoa, iwe kwa njia ya ndoa, upadre, ushemasi wa kudumu, au maisha ya wakfu. Kila wito ni zawadi isiyopimika kwa Kanisa na kwa wale wanaoupokea kwa furaha. Kumfahamu Bwana inamaanisha kwanza kabisa kujifunza kujikabidhi kwake na kwa msaada wake, ambao ni mkubwa kwa kila wito.

Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za Huruma ya Mungu
Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za Huruma ya Mungu   (@Vatican Media)

Uaminifu: Ufahamu huzaa kujiamini, mtazamo ambao hutokana na imani na ni wa lazima kwa ajili ya kukaribisha wito wa mtu na kudumu katika wito husika. Hakika, maisha hujidhihirisha kama tendo endelevu la kuamini katika Bwana na kujiachia kwake, hata wakati ambapo mipango yake inakinzana na yetu. Tumfikirie Mtakatifu Yosefu, ambaye, pamoja na ujauzito wa fumbo na usiotarajiwa wa Bikira, aliuamini ujumbe wa kimungu uliodhihirishwa kwake katika ndoto na akamkaribisha Maria na mwanae kwa moyo mtiifu (rej. Mt 1:18-25; 2:13-15). Yosefu wa Nazareti ni mfano wa matumaini kamili katika mipango ya Mungu. Aliamini hata wakati ambapo kila kitu kilichomzunguka kilionekana kuzingirwa katika giza na mashaka, wakati ambapo matukio yalionekana kuwa kinyume na mipango yake binafsi. Aliamini na kujikabidhi kwa Mungu, akiwa na hakika katika wema na uaminifu wa Bwana. “Katika kila hali, Yosefu alitangaza “ndio” yake, mithili ya ile ya Maria wakati wa kupashwa habari na ya Yesu katika Bustani ya Getsemane.” Kama Jubilei ya Matumaini ilivyotukumbusha, ni lazima kustawisha imani thabiti na isiyotetereka kwa ahadi za Mungu, pasipo kukata tamaa. Lazima tushinde hofu na mashaka, hali tukiamini kuwa Bwana wa historia – wa ulimwengu na wa kila historia ya kila mmoja wetu – amefufuka. Hatutelekezi kamwe katika masaa yetu ya giza zito, bali huja kutawanya kila kivuli kwa nuru yake. Kwa njia ya nuru na nguvu ya Roho Mtakatifu, hata katikati ya majaribu na hatari, twaweza kuuona wito wetu ukikua na kukomaa, tukitafakari kikamilifu zaidi uzuri wa Yeye ambaye ametuita – uzuri ulioundwa kwa uaminifu na imani, pasipo kujali majeraha na kushindwa kwetu.

Waamini wanaalikwa kumfahamu Mungu: Sala, Neno, Sakramenti na Matendo
Waamini wanaalikwa kumfahamu Mungu: Sala, Neno, Sakramenti na Matendo   (@Vatican Media)

Ukomavu: Hakika, wito sio jambo la kudumu bila kubadilika, bali ni mchakato wa kukomaa unaotegemezwa na husiano wa ndani na Bwana. Kukua katika wito wa kila mmoja wetu maana yake ni kuwa pamoja na Yesu, kumruhusu Roho Mtakatifu atende katika roho zetu na katika mazingira ya maisha, na kutafsiri upya kila kitu katika mwanga wa zawadi hii. Kama mzabibu na matawi yake (rej. Yh 15:1-8), maisha yetu yote lazima yawe yamesimikwa katika muungano thabiti na hai pamoja na Bwana, ili tuweze kwa moyo wote kuitikia wito wake kupitia majaribu yetu na “kupogolewa” kwa lazima. “Maeneo” ambayo mapenzi ya Mungu hudhihirika wazi, na ambapo tunafaidika na upendo wake usio na kikomo, daima ni muungano halisi na wa kindugu tuwezao kuanzisha katika maisha yetu yote. Jinsi gani ilivyo na thamani kuwa na uongozi wa kiroho ulio wa kweli kwa ajili ya kutusindikiza katika kutambua na kukua kwa wito wetu! Jinsi gani ilivyo muhimu kung’amua na kupima maongozi ya Roho Mtakatifu, ili wito uweze kufikia kuzaa matunda katika uzuri wake wote! Kwa hiyo, wito, sio mali inayomilikiwa mara moja – kitu “kinachotolewa” mara moja tu basi. Badala yake, ni njia ambayo hujifungua sana kama maisha yenyewe. Zawadi ambayo tumepokea inapaswa sio tu kulindwa bali kustawishwa pia kwa njia ya uhusiano wa kila siku na Mungu ili iweze kukua na kuzaa matunda. “Hii ina manufaa, kwani inayaweka maisha yetu yote katika uhusiano kwa Mungu anayetupenda. Inatufanya kutambua kuwa hakuna chochote kile ambacho ni matokeo ya bahati nasibu tu bali kwamba kila kitu katika maisha yetu chaweza kuwa njia ya kumuitikia Bwana, ambaye ana mpango nasi wa kustaabisha sana.” Ndugu wapendwa, wapendwa vijana, ninawatia moyo kustawisha uhusiano wenu binafsi na Mungu kwa njia ya sala za kila siku na tafakari ya Neno. Tulia, sikiliza na jiaminishe. Kwa namna hii, zawadi ya wito wenu itaweza kukua, kuwaletea furaha na kuzaa matunda mengi kwa Kanisa na ulimwengu.  Bikira Maria, kielelezo cha kupokea zawadi za Mungu moyoni na mtaalamu katika kusikiliza, aandamane nanyi daima katika safari hii!

Kutoka Vatican, 16 Machi 2026

LEO PP. XIV

Ujumbe Siku ya Miito 2026
24 Aprili 2026, 10:32