Papa Leo XIV:Mambo muhimu katika Mkutano na Vijana na Familia,Aprili 22!
Na Angella Rwezaula-Vatican.
Katika mkutano wake wa mwisho barani Afrika, akiwa katika Hija ya Kitume baada ya kuanzia na Algeria, Cameroon, Angola na hatimaye Guinea ya Ikweta, Baba Mtakatifu leo XIV, baada ya siku yake kali kweli kweli aliweza kusikiliza ushuhuda wa Vijana na familia za Guinea ya Ikweta, waliokusanyika katika Uwanja wa Bata. Licha ya mvua iliyonyeshe nyingi hawakujali vijana wa Guinea ya Ikweta na wazazi wao, Jumatano tarehe 22 Aprili 2026. Zifuatazo ni picha zinazoonesha tukio hilo la kusisimua.
Kuanzia changamoto za wanawake mahali pa kazi hadi zile zinazotokana na ndoa, ambazo hukua katika uhuru, Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake mara baada ya kusikiliza shuhuda mbali mbali alisisitiza umuhimu wa kulinda maadili ya familia, hata wakati hukumu, ubaguzi, na dhana potofu zinapojaribu kuyadhoofisha.
Papa alisema "Kila kitu huchangia urithi wa mng'ao na wenye changamoto, ambao vizazi vipya vinaitwa kuuunga mkono na kuujenga."
"Maisha yaliyotolewa kwa Mungu ni ya furaha, lakini lazima yafanywe upya kila siku kupitia sala, sakramenti na muda unaotumika na ndugu na dada ambao Bwana anawaweka njiani mwetu. Katika ushirika wa mioyo na katika matendo ya wema kwa wale wanaohitaji, miujiza ya upendo hufanywa upya kila mara," Papa alibainisha.
"Wapendwa, mmekuja kwenye mkutano huu pamoja na familia zenu. Ni udongo wenye rutuba ambapo ukuaji wenu wa kibinadamu na Kikristo, kama mti mchanga na dhaifu, huzama mizizi yake. Basi, ninawaalika kumshukuru Bwana pamoja kwa zawadi ya wapendwa wenu."
"Wengi wenu mtajiandaa kupokea sakramenti ya Ndoa Takatifu. Kuwa wanandoa na wazazi ni dhamira ya kusisimua, agano la kuishi siku baada ya siku. Ndani ya agano hili, mtagunduana upya kila mara mnaposhirikiana na Mungu katika muujiza wa maisha na katika kujenga furaha kwa ajili yenu na kwa ajili ya watoto wenu."
"Kuweni tayari kukubali wito huu kama safari ya upendo wa kweli unaokua katika uhuru; kama safari ya matumaini, inayotokana na ufahamu kwamba Mungu hatakuacha kamwe; na kama safari ya utakatifu, ambapo daima unatafuta mema na furaha ya wengine."
"Familia inayojua jinsi ya kukaribisha na kupenda inakuwa chanzo cha mwanga na joto. Papa Francisko anaielezea familia vizuri kwa maneno haya: “Baba na mama, wanandoa wenye historia yao binafsi ya upendo… wanandoa wanaopenda na kuzaa maisha ni alama ya kweli na iliyo hai… inayoweza kumfunua Mungu Muumba na Mwokozi” (Wosia wa Kitume Amoris Laetitia, 9, 11)."
Baba Mtakatifu alisema, "Wapendwa vijana, wazazi na wote waliopo, hebu tuhamasishwe na uzuri wa upendo; hebu tuwe mashahidi wa upendo ambao Yesu ametupa na kutufundisha!"
"Tuoneshe kila siku kwamba ni vizuri kupenda, kwamba furaha kubwa zaidi, katika kila hali, hutokana na kujua jinsi ya kutoa na kujitoa wenyewe, hasa tunapowafikia wale wanaohitaji zaidi. Nuru ya upendo, inayohamasishwa katika nyumba zetu na kuishi kwa imani, inaweza kubadilisha ulimwengu, hata miundo na taasisi zake, ili kila mtu aheshimiwe na pasiwepo mtu anayesahaulika.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.
