Papa Leo XIV:Mtoke nje mkagundue utamaduni,watu na maisha!

Katika Siku ya kuombea Miito Duniani,Dominika Aprili 26,Papa Leo XIV aliongoza Misa Takatifu Katika Basilika ya Mtakatifu Petro na kuwaweka wakfu mapadre wapya kumi,wa Jimbo Kuu la Roma.Aliwaalika kukua katika ushirika na Jumuiya zao za Parokia na kuhakikisha kwamba Kanisa linabaki wazi kuwakaribisha watu wote.”Muwe msaada,wajenzi wa amani na urafiki wa kijamii.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika fursa ya Siku ya 63 ya kuombea Miito duniani ambayo imeadhimishwa tarehe 26 Aprili 2026, kwa Dominika itwayo ya Mchunguaji Mwema, kwa maneo matatu msingi: Kusimama, kusikiliza, kuamini katika muktadha wa Kauli mbiu yake ya  “Ugunduzi wa Ndani wa Zawadi ya Mungu.”  Katika muktadha huo, Baba Mtakatifu Leo XIV aliongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Basilika ya Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kuwaweka daraja la Upadre kwa Mapadre wapya 10 wa Jimbo Kuu la Roma.  Baada ya masomo na utangulizi na kuwapokea, Baba Mtakatifu alianza mahubiri yake  yakijikita na  Injili ya Yohane kwa kuzingatia Dominika Iitwayoy ya Mchungaji mwema.  

Papa alisema Dominika iliyojaa maisha! Ingawa kifo kinatuzunguka, ahadi ya Yesu tayari inatimia: "Mimi nilikuja ili wawe na uzima, na wawe nao tele" (Yh 10:10). Katika uwazi wa vijana ambao Kanisa linaomba wawe makuhani waliowekwa wakfu leo, tunaona ukarimu na shauku kubwa. Tunapokusanyika, tukiwa wengi na tofauti, karibu na Mwalimu mmoja, tunahisi nguvu inayotufanya tuwe wapya. Ni Roho Mtakatifu, anayewafunganisha watu na miito katika uhuru, ili mtu yeyote asiishi kwa ajili yake mwenyewe. Dominika ya kila Dominika  hutuita kutoka katika "kaburi" la kutengwa na kufungwa, ili tuweze kukutana katika bustani ya ushirika, ambayo mlinzi wake ni Mfufuka.

Huduma ya Padre ni kutafakari huduma ya umoja

Huduma ya Padre, ambayo wito kwa ndugu hawa unatualika kutafakari, ni huduma ya ushirika. "Uzima tele," kiukweli, unatujia katika kukutana kibinafsi na nafsi ya Mwana, lakini mara moja hufungua macho yetu kwa watu,  kaka na dada ambao tayari wanapata, au bado wanatafuta, "nguvu ya kuwa watoto wa Mungu" (Yh 1:12). Hapa kuna siri ya kwanza katika maisha ya Upadre.

Kwa kuwageukia mashemasi wa kupokea daraja la Upadre, Baba Mtakatifu Leo XIV alisema kuwa: “Wapendwa waamini, kadiri uhusiano wenu na Kristo ulivyo mkubwa zaidi, ndivyo mnavyozidi kuwa wa ubinadamu wetu wa kawaida. Hakuna upinzani, wala ushindani, kati ya mbingu na dunia: katika Yesu ni kuungana milele. Fumbo hili lililo hai na lenye nguvu hushirikisha moyo katika upendo usiovunjika: hushirikisha na kuutimiza. Hakika, kama upendo wa wanandoa, upendo unaohamasisha useja kwa ajili ya Ufalme wa Mungu,  lazima uhifadhiwe na kupyaishwa kila mara, kwa sababu kila upendo wa kweli hukomaa na kuwa na matunda baada ya muda. Mmeitwa kwa njia maalum, maridadi, na ngumu ya kupenda, na hata zaidi, ya kujiruhusu kupendwa, katika uhuru. Njia ambayo inaweza kuwafanya sio tu mapadre wazuri, bali pia raia waaminifu, wenye msaada, wajenzi wa amani na urafiki wa kijamii.

Sura ya Yesu na ishara za kushambuliwa na anaowapenda

Katika suala hilo Papa aliongeza kusema kuwa “marejeo ya Yesu kuhusu watu na vitendo vya uchokozi katika Injili iliyosomwa (Yh 10:1-10) yanashangaza: wageni, wezi, na majambazi, wanaovuka mipaka, huingia kati yake na wale anaowapenda. Wanakuja "kuiba, kuua, na kuharibu" (Yh 10 10), na zaidi ya yote, wana sauti tofauti na yake, isiyotambulika (Yh 10, 5). Kuna uhalisia mkubwa katika maneno ya Bwana: anajua ukatili wa ulimwengu anaotembea nao. Kwa maneno yake, anaamsha aina za uchokozi wa kimwili, lakini zaidi ya yote wa kiroho. Hata hivyo, hii haimzuii kutoa uhai wake. Kukemea kwake si kujikana, hatari haimfanyi akimbie. Hii hapa siri ya pili kwa maisha ya upadre: ukweli haupaswi kututisha. Ni Bwana wa uzima anayetuita. Huduma iliyokabidhiwa kwenu, wapendwa, iwasilishe amani ya wale ambao, hata katikati ya hatari, wanajua kwa nini wako salama,” Papa alikazia kusema.

Leo, hitaji la usalama huwafanya watu kuwa wakali, jumuiya hujifungia yenyewe binafsi, na husababisha kutafuta maadui na watu wanaolaumiwa isivyo haki kwa matatizo, makosa, au matukio hasi ya pamoja. Mara nyingi kuna hofu karibu nasi na labda ndani yetu. Usalama wenu usije ukawa katika nafasi mliyonayo, bali katika maisha, kifo, na ufufuko wa Yesu, katika historia ya wokovu ambayo inashirikisha na watu wenu,” Papa amewashauri. Ni wokovu ambao tayari unafanya kazi katika mema mengi, yaliyotimizwa kimya kimya, miongoni mwa watu wenye mapenzi mema, katika Parokia na katika  mazingira  ambayo wao watakuwa karibu nazo, kama wasafiri wenzao. Kwa hiyo wanachotangaza na kusherehekea kitawalinda hata katika hali na nyakati ngumu.

Kuweni kama bustani za uzima ambazo zitafufuliwa na kushirikishwa

Jumuiya ambazo watatumwa ni sehemu ambazo Mfufuka tayari yupo, ambapo wengi tayari wamemfuata kwa njia ya mfano. Watatambua majeraha yao, watatofautisha sauti yao, watapata wale watakao waonesha. Hizi ni jumuiya ambazo zitawasaidia pia kuwa watakatifu! Hivyo Papa amewaomba wao wawasaidie kutembea kwa umoja nyuma ya Yesu, Mchungaji Mwema, ili wawe sehemu, ya bustani za uzima ambazo zitafufuliwa na kushirikishwa. Mara nyingi watu wanakosa mahali ambapo wanaweza kupata uzoefu kwamba pamoja ni bora zaidi, kwamba pamoja ni pazuri, kwamba tunaweza kuishi pamoja.

Kuwezesha mikutano, kuwasaidia wale ambao vinginevyo hawangekutana, na kuleta mambo yanayopingana pamoja yote ni kitu kimoja na kuadhimisha  Ekaristi na Upatanisho. Kukusanyika daima  na ni tena, kuanzisha Kanisa. Taswira muhimu katika Injili ni ile ambayo, wakati fulani, Yesu anaanza kuzungumza kujihusu yeye. Alikuwa akijielezea kama "mchungaji," lakini wale waliomsikiliza walionekana kutoelewa. Kisha akabadilisha mtindo: "Amin, amin, nawaambia, Mimi ndimi mlango wa kondoo" (Yh 10:7). Huko Yerusalemu, kulikuwa na mlango ulioitwa hasa, "mlango wa kondoo," karibu na Bwawa la Bethesda. Kondoo na wana-kondoo waliingia hekaluni kupitia hilo, kwanza wakizama majini na kisha wakapelekwa kuchinjwa. Ni kawaida kufikiria Ubatizo.

Jubilei imetuonesha sura ya mlango:ni moyo wa mamilisho ya watu

"Mimi ndiye mlango," asema Yesu. Jubilei imetuonesha jinsi picha hii bado inavyozungumza na mioyo ya mamilioni ya watu. Kwa karne nyingi, mlango, mara nyingi ni lango halisi, umewaalika watu kuvuka kizingiti cha Kanisa. Katika baadhi ya matukio, kisima cha ubatizo kilijengwa nje, kama Bwawa la kale, ambalo chini ya varanda zake "walemavu wengi walikuwa wamelala, vipofu, viwete, na waliopooza" (Yh 5:3). Kwa njia hiyo Papa aliomba wote kujisikia kuwa  kama sehemu ya ubinadamu huu unaoteseka, ukingoja uzima tele. Katika kuwaingiza wengine katika imani, “mtawasha upya wenu wenyewe. Pamoja na wengine waliobatizwa, mtavuka kizingiti cha Fumbo kila siku, kizingiti hicho chenye uso na jina la Yesu. Kamwe msiufiche mlango huu mtakatifu, msiuzuie, wale wanaotaka kuingia.” "Hamkuingia, na mliwazuia wale waliokuwa wakiingia" (Lk 11:52): hii ni karipio kali la Yesu kwa wale walioficha ufunguo wa kufungua mlango ambao hungepaswa kuwa wazi kwa wote. "Mimi ndiye mlango," asema Yesu.

Acheni milango wazi ambapo wengi leo hii wanafunga

"Leo zaidi ya hapo awali, hasa pale ambapo idadi inaonekana kuonesha mgawanyiko kati ya watu na Kanisa," Papa Leo XIV aliongeza " acheni mlango wazi! Waruhusu watu waingie na muwe tayari kutoka. Hii ni siri nyingine kwa maisha yenu: ninyi ni mfereji, si kichujio. Wengi wanaamini tayari wanajua kilichopo zaidi ya kizingiti hicho. Wanabeba kumbukumbu, labda kutoka zamani za mbali; mara nyingi kuna kitu kilicho hai ambacho hakijaisha na kinachovutia; wakati mwingine, hata hivyo, kuna kitu kingine, ambacho bado kinavuja damu na kurudisha nyuma. Bwana anajua na anasubiri. Kuweni  dhihirisho la uvumilivu wake na huruma yake. Ninyi ni wa kila mtu! Hili liwe kipengele cha msingi cha utume wenu: kuweka wazi bawaba wazi na kuonesha, bila kuhitaji maneno mengi sana.”

Sio kujitenga na maisha:maisha hayaishii tu kwa parokia

Kwa upande mwingine, Yesu anasisitiza na kubainisha: "Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa kupitia mimi, ataokolewa, naye ataingia na kutoka, na kupata malisho" (Yh10:9). Hazuii uhuru wetu. Kuna ushirika unaokandamiza, ushirika ambao ni rahisi kuingia lakini karibu hauwezekani kuondoka. Siyo hivyo ilivyo kwa Kanisa la Bwana, wala kwa ushirika wa wanafunzi wake. Wale waliookolewa, Yesu anasema, "ingia, toka, na kupata malisho." Sote tunatafuta makazi, pumziko, na utunzaji: mlango wa Kanisa uko wazi. Papa ameonya kwamba “ Sio kujitenga na maisha: maisha hayaishii kwa parokia, chama, harakati, kikundi tu. Wale waliookolewa "hutoka na kupata malisho." Papa Leo XIV aliwahimizia watoke nje wakagundue utamaduni, watu, maisha! "Mshangae kile ambacho Mungu husababisha kukua bila sisi kukipanda," Papa alisisitiza.

Papa Leo aidha alisema,  "Wale ambao mtakuwa mapadre, waaminifu na familia, vijana kwa wazee, watoto na wagonjwa, wanaishi katika malisho ambayo lazima myajue. Wakati mwingine mnaweza kuhisi hamna ramani. Lakini Mchungaji Mwema anazo, na lazima msikilize sauti yake inayojulikana. Ni watu wangapi leo wanahisi wamepotea! Wengi wanahisi hawawezi tena kupata njia yao. Hakuna ushuhuda wa thamani zaidi kuliko ule unaosema: "Katika malisho mabichi hunilaza; Huniongoza kando ya maji tulivu. Hunihuisha roho yangu. Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake" (Zab 23:2-3). Jina lake ni Yesu: "Mungu anaokoa!" Kwa hili ninyi ni mashuhuda. "Hakika wema na uaminifu vitanifuata siku zote za maisha yangu" (Zab 23:6). Na kwa njia yo Kaka, dada, vijana wapendwa: na iwe hivyo!" Papa alihitimisha.

Papa kwa daraja la Upadrisho

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

26 Aprili 2026, 11:05