Papa Leo XIV,Chuo Kikuu:Kuunda dhamiri huru yenye uwezo wa kubadili maisha ya watu

Akikutana na ulimwengu wa Chuo Kikuu Katoliki cha Afrika ya Kati huko Yaoundé,Cameroon,Aprili 17,Papa Leo XIV alisema:Ukuu wa taifa hauwezi kupimwa kwa wingi wa rasilimali zake asili tu,wala utajiri wa taasisi zake,isipokuwa umejengwa katika dhamiri njema,yenye msingi katika ukweli.Ingawa bara la Afrika linafahamu vyema vipengele vyake vya kuvutia,pia linajua upande mweusi wa uharibifu wa mazingira na kijamii unaosababishwa na utafutaji usiokoma wa malighafi na ardhi adimu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, mara baada ya kutoka safari ya huko Douala mahali ambapo aliadhimisha misa na kutembelea kituo cha Afya katoliki, alasiri tarehe 17 Aprili 2026, hadi Yaoundé, nchini Cameroon, alihutubia Ulimwengu wa wasomi katika Jumuiya ya Chuo Kikuu Katoliki cha Afrika ya Kati, katika Ziara yake ya Kitume iliyoanza tangu Jumatatu Aprili 13, barani Afrika. Hotuba ya Papa Leo imezungukia juu ya kuondoa udanganyifu wa mgongano kati ya sayansi na imani, pia kukemea hatari ya maarifa ambayo hujisalimisha katika mantiki inayotawala.  Zaidi pia alibainisha kwamba ukuu wa taifa hauwezi kupimwa tu kwa wingi wa rasilimali zake za asili, wala hata kwa utajiri wa taasisi zake. Kiukweli, hakuna jamii inayoweza kustawi isipokuwa imejengwa katika dhamiri njema, yenye kusimikwa msingi wa ukweli. Papa alieleza juu ya hatari za Akili Unde na aliwapa vijana onyo la kutohama wakifikiria kutafuta mstakabali nje ya nchi yao, badala yake waitikie wito wa kulitumikia taifa lao.

Papa akikaribishwa na Chancela wa Chuo Kikuu Katoliki
Papa akikaribishwa na Chancela wa Chuo Kikuu Katoliki   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu awali ya yote baada ya kusikiliza salamu ya Mkuu wa chuo, shuhuda mbali mbali kutoka kwa vijana, alianza kwa salamu kwa wakuu na wote waliokuwapo. Alionesha furaha ya kuwahutubia katika Chuo hicho Katoliki kuwa, ni “kitovu cha ubora wa utafiti, uenezaji wa maarifa na malezi ya vijana wengi.” Alitoa shukrani zake kwa mamlaka ya kitaaluma kwa makaribisho yao ya joto na kwa kujitolea kwao mara kwa mara kwa huduma ya elimu. Papa alisema “Ni chanzo cha matumaini kwamba taasisi hii, iliyoanzishwa mwaka 1989 na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika ya Kati, inaweza kutumika kama taa kwa Kanisa na kwa Afrika katika utafutaji wake wa ukweli, pamoja na kukuza haki na mshikamano. Leo zaidi ya hapo awali, ni muhimu kwamba vyuo vikuu na hasa taasisi za Kikatoliki za elimu ya juu viwe jumuiya za kweli za maisha na utafiti, kuwatambulisha wanafunzi na maprofesa sawa katika udugu katika maarifa, "kama sharti la ndani la kupata uzoefu katika jamii furaha ya Ukweli na kufahamu kikamilifu maana yake na matokeo yake ya vitendo.”

Papa akibariki Sanamu ya Mtakatifu Agostino
Papa akibariki Sanamu ya Mtakatifu Agostino   (@Vatican Media)

Leo hii utangazaji wetu wa Injili na mafundisho ya Kanisa yanaitwa kuhamasisha utamaduni wa kukutana, kwa ushirikiano wa ukarimu na wazi na nguvu zote chanya zinazochangia ukuaji wa ufahamu wa ubinadamu wote. Papa aliongeza kuwa,  “Tunaweza kusema utamaduni wa kukutana kati ya tamaduni zote halisi ni muhimu, kutokana na kubadilishana zawadi za kila mmoja katika nafasi hiyo inayong'aa iliyofunguliwa na upendo wa Mungu kwa viumbe vyake vyote. Kama Papa Benedikto XVI alivyosema, “ukweli”, kwa dhati ni logos” ambayo inaunda “dia-logos” na hivyo mawasiliano na ushirika’” (Francisko, Katiba ya Kitume ya Veritatis Gaudium, 4b).

Wengine walikaa nje
Wengine walikaa nje   (@Vatican Media)

Chuo Kikuu kinasimama mahali pazuri pa urafiki,ushirikiano na tafakari

Hakika, wakati ambapo wengi duniani wanaonekana kupoteza marejeo yao ya kiroho na kimaadili, wakijikuta wamefungwa katika ubinafsi, upuuzi na unafiki, Chuo Kikuu kinasimama kama mahali pazuri pa urafiki, ushirikiano na, wakati huo huo, pa ndani na tafakari. Kuanzia asili yake katika Enzi za Kati, waanzilishi wake waliweka Ukweli kama lengo lake. Leo hii bado, maprofesa na wanafunzi wanaitwa kukumbatia utafutaji wa kawaida wa ukweli kama lengo lao na njia yao ya maisha, kwani, kama Mtakatifu John Henry Newman alivyoandika, "Kanuni zote za kweli huendeshwa na Mungu, matukio yote hukutana naye"(Hotuba: Wazo la Chuo Kikuu, II).

Sanamu ya Mtakatifu Agostino
Sanamu ya Mtakatifu Agostino   (@Vatican Media)

Upendo unaishi kila wakati katika mwili na roho

Wakati huo huo, kile ambacho Newman alichokiita "nuru ya wema,"  yaani, "nuru ya imani, iliyounganishwa na ukweli wa upendo," si "nje ya ulimwengu wa kimwili, kwani upendo huishi kila wakati katika mwili na roho; nuru ya imani ni nuru iliyofanyika mwili inayong'aa kutoka katika maisha angavu ya Yesu. Pia inaakisi ulimwengu wa vitu, inaamini mpangilio wake wa asili na inajua kwamba inatuita kwenye njia inayopanuka zaidi ya maelewano na uelewa. Kwa hivyo, mtazamo wa sayansi unafaidika na imani: imani inamtia moyo mwanasayansi kubaki wazi kila wakati kwa ukweli katika utajiri wake wote usioisha. Imani huamsha hisia muhimu kwa kuzuia utafiti kuridhika na mitindo yake na husaidia kutambua kwamba asili ni kubwa zaidi kila wakati. Kwa kuchochea mshangao kabla ya fumbo kubwa la uumbaji, imani hupanua upeo wa sababu ili kutoa mwangaza zaidi juu ya ulimwengu unaojifunua kwa uchunguzi wa kisayansi” (Francisko, Waraka wa Lumen Fidei, 34).

Wanazuoni
Wanazuoni   (@Vatican Media)

Afrika inaweza kutoa mchango mkubwa wa upenyo finyu kuelekea matumaini

Papa Leo XIV aliendelea kudadavua kuwa “Afrika inaweza kutoa mchango mkubwa katika kupanua upeo finyu wa ubinadamu unaojitahidi kuwa na matumaini. Katika bara lenu zuri, watafiti wameitwa hasa kujifungulia mitazamo ya taaluma mbalimbali, kimataifa na kitamaduni.  Leo, zaidi ya hayo, kuna haja ya haraka ya kufikiria kuhusu imani ndani ya mfumo wa muktadha wa kiutamaduni mamboleo na changamoto zilizopo, ili uzuri na uaminifu wake uweze kujitokeza katika mazingira mbalimbali, hasa katika yale yaliyo na alama nyingi za ukosefu wa haki, ukosefu wa usawa, migogoro na uharibifu wa kimwili na kiroho. Ukuu wa taifa hauwezi kupimwa tu kwa wingi wa rasilimali zake asili, wala hata kwa utajiri wa taasisi zake. Kiukweli, hakuna jamii inayoweza kustawi isipokuwa imejengwa katika dhamiri njema, iliyojengwa katika ukweli. Kwa maana hiyo, kauli mbiu ya chuo kikuu chenu: "Katika huduma ya ukweli na haki", Papa aliongeza :“inakumbusha kwamba dhamiri ya mwanadamu, inayoeleweka kama mahali pa ndani ambapo wanaume na wanawake hujikuta wakivutwa na sauti ya Mungu, ndiyo chanzo cha misingi ya haki na imara kwa kila jamii ambayo lazima iwekwe.”

Mmoja wa mwanafunzi aliyezungumza
Mmoja wa mwanafunzi aliyezungumza   (@Vatican Media)

Kuunda dhamiri huru yenye uwezo wa kubadili maisha ya watu binafsi na jamii

Kuunda dhamiri zilizo huru na zilizojaa utakatifu wa kutotulia ni sharti muhimu kwa imani ya Kikristo kuonekana kama pendekezo kamili la kibinadamu. Imani kama hiyo ina uwezo wa kubadilisha maisha ya watu binafsi na jamii, ya kuhamasisha mabadiliko ya kinabii mbele ya misiba na aina za umaskini wa wakati wetu, na kuhimiza utafutaji endelevu wa Mungu ambao hauridhishwi kamwe. Kwa hakika ni ndani ya dhamiri ambapo utambuzi wa maadili huundwa, ambapo tunatafuta kwa uhuru yaliyo ya kweli na ya haki. Dhamiri inapojali kuelimika na kuumbwa kwa usahihi, inakuwa chanzo cha njia thabiti ya kutenda, inayoelekezwa kwa wema, haki na amani. Katika jamii za kisasa, na kwa hivyo nchini Cameroon pia, tunaweza kushuhudia mmomonyoko wa maadili ambayo hapo awali yaliongoza maisha ya jamii. Kwa hivyo, leo hii kuna tabia ya kukubali desturi fulani ambazo hapo awali zilizingatiwa kuwa hazikubaliki. Mabadiliko haya yanaweza kuelezewa kwa sehemu na mabadiliko ya kijamii, shinikizo la kiuchumi na nguvu za kisiasa zinazounda tabia ya mtu binafsi na ya pamoja.

Wakristo hasa Wakatoliki vijana wa kiafrika hawapaswi kuogopa vitu vipya

Wakristo, na hasa Wakatoliki vijana wa Kiafrika, hawapaswi kuogopa "vitu vipya, Papa alisisitiza na kuongeza “Chuo Kikuu chenu, hasa, kinaweza kuunda waanzilishi wa ubinadamu mpya katika muktadha wa mapinduzi ya kidijitali. Ingawa bara la Afrika linafahamu vyema vipengele vyake vya kuvutia, pia linajua upande mweusi wa uharibifu wa mazingira na kijamii unaosababishwa na utafutaji usiokoma wa malighafi na ardhi adimu. Onyo la Papa kwamba “Msiangalie upande mwingine: hii ni huduma kwa ukweli na kwa wanadamu wote.

Papa akihutubia ulimwengu wa vyuo vikuu
Papa akihutubia ulimwengu wa vyuo vikuu   (@Vatican Media)

Kuenea kwa AI inayozidi kuunda na kupenya mawazo yetu na mazingira ya kijamii

Bila juhudi hii ngumu ya kielimu, marekebisho yasiyojali kwa dhana kuu yatakosewa kuwa uwezo, na kupoteza uhuru wa maendeleo. Hili ni kweli zaidi kutokana na kuenea kwa mifumo ya akili unde(AI), ambayo inazidi kuunda na kupenya mawazo yetu na mazingira ya kijamii. Kama kila mabadiliko makubwa ya kihistoria, hii pia haihitaji tu uwezo wa kiufundi, bali pia kwa uundaji wa kibinadamu unaoweza kuonesha mantiki iliyo nyuma ya uchumi, upendeleo uliojikita na aina za nguvu zinazounda mtazamo wetu wa ukweli. Ndani ya mazingira ya kidijitali, yaliyoundwa ili kushawishi, Papa Leo XIV alibainisha kuwa, mwingiliano umeboreshwa hadi kufikia hatua ya kufanya mkutano halisi kuwa wa ziada; utofauti wa watu katika mwili hupunguzwa, na mahusiano hupunguzwa hadi majibu ya utendaji. Pamoja na hayo Papa aliwaeleza kuwa “Wapendwa marafiki, hata hivyo, ninyi ni watu halisi!

Papa akipokea maua
Papa akipokea maua   (@Vatican Media)

Uumbaji wenyewe una mwili, pumzi, uhai wa kusikilizwa na kulindwa, Papa alisisitza. "Huugua na kuteseka"(taz. Rm 8:22), kama vile kila mmoja wetu anavyofanya. Uigizaji unapozidi kuwa kawaida, hudhoofisha uwezo wa mwanadamu wa utambuzi.” Na kwa njia hiyo “matokeo yake, miunganisho yetu ya kijamii hujifunga yenyewe, na kutengeneza mizunguko ya kujirejea ambayo haituachii tena kwenye uhalisia. Kwa hivyo tunaishi ndani ya viputo, visivyoweza kuingiliwa na kila mmoja. Tukihisi kutishiwa na mtu yeyote ambaye ni tofauti, tunakuwa hatujazoea kukutana na kuzungumza. Kwa njia hiyo, utengano, migogoro, hofu na vurugu huenea.”

Chuo Kikuu Katoliki kinaitwa kuchukua jukumu la  maarifa na kuunda akili

Kilicho hatarini si hatari tu ya makosa, bali mabadiliko katika uhusiano wetu na ukweli. Ni katika nyanja hii hasa ambapo Chuo Kikuu Katoliki kinaitwa kuchukua jukumu la hali ya juu zaidi. Kwani hakitoi maarifa maalum tu, bali kinaunda akili zenye uwezo wa utambuzi na mioyo iliyo tayari kwa upendo na huduma. Zaidi ya yote, kinawaandaa viongozi wa siku zijazo, maafisa wa umma, wataalamu na watendaji wengine katika jamii kutekeleza kwa uadilifu majukumu waliyokabidhiwa, kutekeleza majukumu yao kwa unyofu na kuweka shughuli zao ndani ya mfumo wa maadili kwa ajili ya manufaa ya wote.

Papa azungumza na Ulimwengu wa vyuo vikuu
Papa azungumza na Ulimwengu wa vyuo vikuu   (@Vatican Media)

Onyo la Papa kwa vijana kuhusu kuhama wakitafuta mustakabali

Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea kusema kuwa, “Wapendwa wana na binti wa Cameroon, wanafunzi wapendwa, katika kukabiliana na mwelekeo unaoeleweka wa kuhama,  ambao inawezekana kumfanya mtu aamini kwamba kwingineko kuna mustakabali bora,  unaoweza kupatikana kwa urahisi zaidi, kwanza kabisa, ninawaalika mwitikie kwa hamu kubwa ya kuitumikia nchi yenu na kutumia maarifa mnayopata hapa kwa manufaa ya raia wenzenu. Hii ndiyo sababu ya Chuo Kikuu chenu kilichoanzishwa miaka thelathini na mitano iliyopita ili kuunda wachungaji wa kiroho na watu walei waliojitolea kwa jumuiya: hawa ni mashuhuda wa hekima na haki, ambayo bara la Afrika linahitaji.”

Papa azungumza na wanachuo
Papa azungumza na wanachuo   (@Vatican Media)

Kutangaza habari njema ya Kristo kwa wote

Katika suala hilo, Papa alipenda kukumbusha usemi wa Mtakatifu Yohane Paulo II: Chuo Kikuu Katoliki "kinazaliwa kutoka moyoni mwa Kanisa" (Katiba ya Kitume Ex Corde Ecclesiae, 15 Agosti 1990, 1) na kinashiriki katika dhamira yake ya kutangaza ukweli unaotuweka huru. Uthibitisho huu unarejea kimsingi sharti la kiakili na kiroho: kutafuta ukweli katika vipimo vyake vyote, kwa imani kwamba imani na sababu hazipingani, bali zinasaidiana. Zaidi ya hayo, inatukumbusha kwamba maprofesa na wanafunzi wa Chuo Kikuu wanahusika katika kazi ya Kanisa ya "kutangaza habari njema ya Kristo kwa wote, katika mazungumzo na sayansi tofauti na katika huduma ya uelewa wa kina na matumizi ya ukweli katika maisha ya watu binafsi na jamii" (Francisko, Katiba ya Kitume Veritatis Gaudium, 8 Desemba 2017, 5).

Chuo kikuu Katoliki kina nafasi ya kipekee na isiyoweza kubadilishwa

Katika kukabiliana na changamoto za wakati wetu, chuo kikuu Katoliki kina nafasi ya kipekee na isiyoweza kubadilishwa. Katika suala hilo Papa alisisitiza kuwa, “hebu tuwatafakari waanzilishi wa taasisi hii, ambao waliweka misingi ambayo mnajenga juu yake leo. Miongoni mwao, Papa alimkumbuka kwa namna ya pekee Padre  Barthélemy Nyom, ambaye alihudumu kama Mkuu wa Chuo,  kwa miaka mingi ya 1990. Kwa kufuata mfano wake, lazima  kukumbuka kila wakati kwamba, pamoja na upitishaji wa maarifa na ukuzaji wa uwezo wa kitaaluma, chuo kikuu hiki kinatafuta kuchangia katika malezi fungamani ya mwanadamu. Usindikizaji wa kiroho na kibinadamu ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Chuo Kikuu Katoliki. Kupitia malezi ya kiroho, mipango ya huduma ya kichungaji ya chuo kikuu na nyakati za kutafakari, wanafunzi wanaalikwa kuimarisha maisha yao ya ndani na kuelekeza ushiriki wao katika jamii katika mwanga wa maadili halisi na ya kudumu. Kwa njia hiyo, wanafunzi wapendwa, mnajifunza kuwa wajenzi wa mustakabali wa nchi zenu husika na ulimwengu wenye haki na utu zaidi.

Ulimwengu wa vyuo vikuu
Ulimwengu wa vyuo vikuu   (@Vatican Media)

Kwa Maprofesa, kutoa haki na usawa,uadilifu,roho na huduma na uwajibikaji

Papa Leo XIV aliendelea na houba yake akisema "Wapendwa maprofesa, jukumu lenu ni muhimu. Kwa hivyo ninawahimiza kuiga maadili mnayotaka kutoa, zaidi ya yote haki na usawa, uadilifu, roho ya huduma, na hisia ya uwajibikaji. Afrika na dunia zinahitaji watu waliojitolea kuishi kulingana na Injili na kuweka vipaji vyao katika huduma ya manufaa ya woteMsisaliti wazo hili zuri! Mbali na kuwa viongozi wa kiakili, iweni mifano ya kuigwa ambayo ukali wao wa kisayansi na uadilifu wao binafsi huunda dhamiri za wanafunzi wenu."

Wawakilishi wa wasemaji katika Mkutano wa Papa na wanachuo
Wawakilishi wa wasemaji katika Mkutano wa Papa na wanachuo   (@Vatican Media)

Afrika lazima iwe huru kutokana na janga la ufisadi

Papa alikazia kusema kuwa “Kiukweli, Afrika lazima iwe huru kutokana na janga la ufisadi. Kwa vijana, ufahamu huu lazima uchukue mizizi kutokana na miaka yao ya malezi, kutokana na ukali wa maadili, kutokuwa na ubinafsi na mshikamano wa maisha unaooneshwa na waelimishaji na walimu wao. Siku baada ya siku, wekeni misingi muhimu kwa ajili ya ujenzi wa utambulisho thabiti wa maadili na kiakili. Kwa kutoa ushuhuda wa ukweli,  hasa mbele ya udanganyifu wa itikadi na mitindo inayopita, kwa sababu  mtakuza mazingira ambayo ubora wa kitaaluma unaunganishwa kiasili na unyofu wa binadamu.”

Ulimwengu wa Vyuo vikuu
Ulimwengu wa Vyuo vikuu   (@Vatican Media)

sifa kuu ambayo lazima ihuishe jumuiya ya chuo kikuu ni unyenyekevu

Hatimaye,  Papa Leo XIV  alisema “Mabibi na mabwana, sifa kuu ambayo lazima ihuishe jumuiya ya chuo kikuu ni unyenyekevu. Hata kama jukumu letu ni lipi au umri wetu, lazima tukumbuke kila wakati kwamba sisi sote ni wanafunzi, yaani, wanafunzi wenza pamoja na Mwalimu mmoja, ambaye aliupenda ulimwengu sana hata akatoa uhai wake. Ninawashukuru, na ninawapa baraka zangu za dhati!

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here

17 Aprili 2026, 18:39