Papa Leo XIV katika kituo cha Yatima:Katika familia hii,kaka yenu mkubwa ni Yesu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kwa kutazama historia ngumu ya watoto na vijana aliwapatia matumaini kwamba “Mahali popote ambapo kunaweza kuwa na umaskini, mateso, au ukosefu wa haki, Mungu yupo pamoja nanyi kwa sababu kwake, hakuna mgeni au aliyesahaulika.” Baba Mtakatifu Leo XIV alisema hayo kwa kutazama historia ngumu ya watoto na vijana na kuwapatia matumaini, alipotembelea Kituo cha Kutunza Watoto na vijana yatima wenye umri kuanzia miaka 3 hadi 20, cha Ngul Zamba, maana yake "Nguvu ya Mungu” huko Yaoundé
Katika Kituo hicho kuna watoto waliotelekezwa, wanafunzi waliotengwa kutoka katika taasisi zingine kwa kufanya uhalifu au kutumia dawa za kulevya, na hata watoto wenye ulemavu. Kituo cha watoto yatima kinasaidiwa na michango, mahalia ya familia" inayowatunza watoto na vijana, viongozi, waelimishaji, watu wa kujitolea, na watawa kutoka Shirika la Mabinti wa Maria, ambao hupambana kila siku na shida za kifedha na kimwili, wakijaribu kuwatafutia chakula na mahitaji ya msingi.
Kwa hiyo ndivyo ilivyoendelezwa Ziara yake ya Kitume ya Pili barani Afrika kati ya nne, jioni tarehe 15 Aprili 2026, mara baada ya siku ya safari ya ndege, kupokelewa uwanjani kwa heshima, kutembelea kwa faragha Rais wa nchi na kuhutubia Mamlaka, asasi za kiraia na wanadiplomasia. Katika salamu zake kwa umati wa watoto hao yatima na vijana, Baba Mtakatifu alisema, “wapendwa watoto, marafiki wapendwa, ninafurahi sana kutembelea kituo hiki cha watoto yatima, ambacho kimekuwa makazi yenu. Hapa, zaidi ya yote, ni Baba yetu wa Mbinguni anayewakaribisha kwa upendo kama watoto wake. Anataka kuwaonesha huruma yake na kuwavuta karibu na moyo wake.”
Katika familia hii, kaka yenu mkubwa ni Yesu
Kwa niaba yake, Papa Leo XIV aliongeza “mimi pia natamani kufanya vivyo hivyo. Hakika, mnaunda familia ya kweli hapa, pamoja na kaka na dada ambao wote wana historia kama hiyo iliyojaa mateso. Katika familia hii, kaka yenu mkubwa ni Yesu! Ni kuishi kama kaka na dada waliokusanyika kumzunguka ndiko kunakufanya muwe na nguvu, kuwasaidia kubeba mizigo ya maisha pamoja na kuwaruhusu kupata furaha ya kweli.”
Katika familia kubwa ya Mungu,hakuna mtu mgeni au amesahaulika
Baba Mtakatifu Leo XIV kadhalika alisema kwamba “Katika ulimwengu ambao mara nyingi huakisiwa na kutojali na ubinafsi, nyumba hii inatukumbusha kwamba sisi ndio tunaohitaji kuwatunza kaka na dada zetu, na kwamba, katika familia kubwa ya Mungu, hakuna mtu ambaye ni mgeni au amesahaulika, haijalishi ni mdogo kiasi gani.”
Ninyi ni wabebaji wa ahadi
Kama Baba, Papa Leo XIV aliwaeleza jinsi anavyojua kwamba “wengi wenu mmevumilia majaribu magumu. Baadhi yenu mmejua uchungu wa kufiwa na wazazi au wapendwa. Wengine wamepitia hofu, kukataliwa, kuachwa, kunyimwa na kutokuwa na uhakika. Hata hivyo, mmeitwa kwenye wakati ujao ambao ni mkubwa kuliko majeraha yenu. Ninyi ni wabebaji wa ahadi.” Kwa maana popote palipo na taabu, mateso au ukosefu wa haki, Mungu yupo; naye anajua kila mmoja wenu na yuko karibu sana nanyi. Kwa kufafanua zaidi Papa alisema, “Injili inatukumbusha kwamba Yesu anawajali hasa watoto kama ninyi, na mara nyingi aliwaweka katikati ya mkutano. Jueni kwamba anawatazama kila mmoja wenu leo hii kwa upendo huo huo.”
Kuwapa Watoto uwepo,sikio la kusikiliza,familia na mustakabali
Papa Leo XIV pia alipenda kutoa salamu na shukrani wote wanaowatunza watoto hao: wakurugenzi, waelimishaji, wafanyakazi, watu wa kujitolea na, bila shaka, Masista. Kujitolea kwao kwa uaminifu ni ushuhuda mzuri wa upendo. Kwa kuwatunza watoto hawa, wanapata kionjo cha furaha ambayo Bwana amewaahidi wale wanaowahudumia wadogo (taz. Mt 25:40). Uvumilivu wao unaonesha uso wa huruma ya Mungu. Kupitia uvumilivu na kujitolea kwao, hawanatoa zaidi ya msaada wa kimwili tu: bali wanawapatia watoto hawa uwepo, sikio la kusikiliza, familia na mustakabali. Kupitia kwao, huruma ya Mungu inadhihirishwa, ile ya huruma ya uaminifu ambayo haififii wakati wa majaribu na kamwe haikatishi tamaa.
Baraka na ulinzi wa Bikira Maria Mama Yetu
Papa aliwashukuru kwa yote wanayofanya, na aliwatia moyo wavumilie kwa ujasiri katika kazi hiyo nzuri ambayo wameifanya. Aliwapatia baraka zake za dhati, akiwakabidhi kila mmoja wao kwa ulinzi wa Bikira Maria, Mama yetu. Awe mwangalifu kila wakati, awafariji wakati wa huzuni na awasaidie kukua kama marafiki wa kweli wa mwanawe, Yesu.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here
