Papa ameacha Mji Mkuu wa Algeria kuelekea nchi ya pili Cameroon kati ya Nne
Vatican News
Ndege ya Shirika la “ ITA Airways” ndani yake akiwemo Baba Mtakatifu Leo XIV ilimeondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Algiers -Houari Boumédiène saa 4.10 asubuhi masaa ya huko. Katika Safari ya ndege terehe 15 Aprili 2026 kuelekea moja kwa moja nchini Cameroon ikiwa ni kituo cha pili kati ya vinne, kwa Baba Mtakatifu katika Ziara yake ya Kitume Barani Afrika. Muda wa safari utadumu karibu masaa matano.
Papa alitembelea shule ya awali ya Notre Dame d’Afrique
Kabla ya kuondoka kwake asubuhi, baada ya kuaga Ubalozi wa Vatican nchini Algeria, Papa alitembelea Shule ya Awali ya “Notre Dame d’Afrique”- "Mama Yetu wa Afrika," inayoratibiwa na Watawa Wamisionari wa Upendo. Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Vatican iliripoti hili kwenye chaneli yake ya Telegram, ikibainisha kwamba "watoto walifanya onyesho fupi kwa ajili ya Papa, ambaye kisha aliwasalimia wao na Masista kabla ya kuondoka kwenda Uwanja wa Ndege."
Telegramu kwa Wakuu wa Nchi
Katika telegramu kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Bwana Abdelmadjid Tebboune Papa alionesha "shukrani kubwa" kwa "mapokezi na ukarimu wa joto" aliokutana nao wakati wa ziara yake nchini humo.
Wito wa nguvu wa Umoja
“Que tous soient un”, “May they all be one”, “In Illo uno unum”. Ni lugha tatu, zinatoa wito wa umoja: mbili za kwanza ni kifungu kutoka Injili ya Yohane; hata hivyo, ya mwisho ni kauli mbiu ya Papa Leo XIV iliyochukuliwa kutoka katika mahubiri ya Mtakatifu Agostino ambayo inaelezea wazo kwamba "ingawa sisi Wakristo tu wengi, katika Kristo mmoja tu wamoja." Huu ni mfumo wa kimaudhui ambao uwepo wa Papa nchini, utaenea karibu hadi Ikweta yote. Papa atakaa Yaoundé, mji mkuu, lakini pia atatembelea Douala, kitovu cha uchumi cha Cameroon, na Bamenda, Kaskazini Magharibi: eneo lililoharibiwa tangu 2013 na mzozo wa umwagaji damu na uliosahaulika kwa kiasi kikubwa, ambao umesababisha maelfu ya vifo na karibu watu 500,000 waliokimbia makazi yao ndani.
Programu Aprili 15
Baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Yaoundé-Nsimalen, Papa Leo XIV atakaribishwa na Waziri Mkuu Joseph Dion Ngute na Balozi wa Vatican nchini Humo Askofu Mkuu José Avelino Bettencourt. Baada ya nyimbo za mataifa na kuwasilishwa kwa wajumbe, Papa Leo XIV ataelekea kwenye Jumba la Umoja, makazi rasmi ya Rais Paul Biya, ambaye atamkaribisha yeye na mkewe, Chantal. Baada ya ziara ya heshima na mkutano wa faragha na kubadilishana zawadi, Papa Leo XIV atakutana na wawakilishi wa mamlaka, asasi za kiraia, na wanadiplomasia, tena katika Jumba la Rais. Hapo, atatoa hotuba yake, ikitanguliwa na hotuba ya Biya, rais wa nchi hiyo.
Kituo kinachofuata katika siku hii ya tatu ya Ziara ya kitume kitakuwa kutembelea Kituo cha Yatima cha Ngul Zamba, kituo kinachofadhiliwa pekee na michango, ambacho huwatunza vijana wenye umri wa miezi 18 hadi miaka 20. Hapo, nyimbo na ushuhuda vitamkaribisha Mrithi wa Petro, ambaye, baada ya kusalimiana na jumuiya, atasafiri hadi makao makuu ya Baraza la Maaskofu wa Cameroon kwa mkutano wa faragha na Maaskofu wa eneo hilo. Siku hiyo itahitimishwa katika Ubalozi wa Vatican nchini Cameroon ambapo Papa atakula chakula cha jioni faraghani.
Sasisho la mwisho ni saa 6.35 mchana na Angella Rwezaula.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here
