Nia ya Maombi ya Papa kwa Mwezi Mei 2026:"Ili kila mmoja apate chakula"
Vatican News
Katika ulimwengu ambapo mamilioni ya watu hawana chakula bora, Papa Leo XIV anapaza sauti yake katika maombi. Katika nia yake kwa mwezi Mei 2026, nayoongoza na mada: “ili chakula kipatikane kwa wote, inavutia umakini kwa mojawapo ya changamoto kubwa zaidi za wakati wetu, yaani njaa na upotevu wa chakula. Kupitia kampeni ya "Ombeni na Papa", ya Mtandao wa Nia ya Maombi ya Papa Ulimwenguni inawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga kila mwezi katika nia ambazo Papa anazibeba moyoni mwake.
Katika sala yake, Baba Mtakatifu Leo XIV anabainisha kwa uchungu kwamba "mamilioni ya kaka na dada bado wanateseka na njaa, huku chakula kingi kikipotea mezani mwetu." Baba Mtakatifu kwa hiyo anatoa mwaliko wa kuamsha ufahamu mpya kwa waamini: Kujifunza kutoa shukrani kwa kila lishe, kula kwa urahisi na kushiriki kwa furaha, tukitambua matunda ya ardhi kama zawadi kutoka kwa Mungu "iliyokusudiwa kwa wote, na si kwa walio wachache tu." Papa anamwomba mwenyezi Mungu aziwezeshe Jumuiya kubadilisha "mantiki ya utumiaji hovyo kibinafsi" kuwa utamaduni wa mshikamano, kuhamasisha vitendo halisi: kampeni za kuongeza uelewa, ghara za chakula, na mtindo wa maisha wenye kiasi na uwajibikaji. Sala inahitimisha kwa ombi kutoka Injili katika: "Mtu yeyote asiondolewe kwenye meza ya pamoja."
Mgogoro wa Chakula Unaoongezeka Duniani
Takwimu za hivi karibuni kutoka katika mashirika ya Umoja wa Mataifa zinaonesha picha ya kuongezeka kwa dharura ya chakula . Kwa mujibu wa Mtazamo wa Chakula kimataifa wa Shirika la Mpango na Chakula Duniani(WFP) 2026, uliochapishwa, Watu milioni 318 wanakabiliwa na viwango vya mgogoro wa njaa au hali mbaya zaidi mwaka 2026. Ripoti hiyo hiyo inaonya kwamba mgogoro katika Mashariki ya Kati unaweza kuwasukuma watu wengine milioni 45 kwenye njaa kali ifikapo katikati ya mwaka. Zaidi ya hayo, njaa mbili za wakati mmoja zilithibitishwa katika sehemu za Gaza na Sudan mwaka 2025, wa kwanza wa karne hii.
Ripoti ya Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani ya 2025, iliyotolewa kwa pamoja na FAO, IFAD, UNICEF, WFP, na WHO, tayari zilionesha kuwa watu milioni 673 waliteseka kutokana na njaa mwaka 2024, na bilioni 2.3 walikuwa wakiishi katika hali ya uhaba wa chakula wa wastani au mkubwa. Zaidi ya watu bilioni 2.6 hawakuweza kumudu lishe bora. FAO na WFP pia wanaonya kwamba ukosefu wa usalama wa chakula utaendelea kuwa mbaya zaidi katika mwaka mzima wa 2026 katika angalau nchi na maeneo 16 yaliyotambuliwa kama maeneo yenye joto kali. Ukweli huu unatia wasiwasi zaidi ukilinganishwa na taka za chakula duniani. Kulingana na Kielezo cha Taka za Chakula cha Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), dunia hupoteza zaidi ya tani bilioni moja za chakula. Zaidi ya hayo, upotevu wa chakula na taka zinawakilisha tatizo kubwa la hali ya tabianchi, linalozalisha kati ya asilimia 8 na 10 ya uzalishaji wa gesi chafu duniani. Utata huu wa kimataifa unaokinzana ni ule ambao Papa Leo XIV anauweka katikati ya maombi yake kwa mwezi huu wa Mei.
Kutenda kwa dhamira mbele ya dhuluma
Mkurugenzi wa kimataifa wa Mtandao wa Maombi wa Papa Duniani, Padre Cristóbal Fones, alisisitiza umuhimu wa nia hii ya maombi na ukaribu wa kibinafsi wa Papa kwa sababu hii: "Nia hii inatoka moyoni mwa Papa." Inamsikitisha sana kwamba watu wengi duniani hawawezi kupata kitu muhimu na cha kibinadamu kama chakula. Kwa hivyo, anatualika sote tusibaki bila kujali, bali kutenda kwa dhamira, kuanzia na sala na kupitia ishara halisi za mshikamano. Mtandao wa Maombi ya Papa Duniani unakumbusha kwamba nia hii si tu wito wa kutafakari, bali pia kuchukua hatua. Papa Leo XIV anaalika Jumuiya nzima ya kibinadamu kuhamasisha mipango ya dhati hasa kuwa na ghala za chakula, kampeni za uhamasishaji, kupunguza upotevu wa majumbani na kutambua mkate "sio kama bidhaa ya walaji, bali kama ishara ya ushirika na utunzaji."
Mtandao wa Maombi ya Papa Ulimwenguni
Mtandao wa Maombi ya Papa Ulimwenguni ni Kazi ya Kipapa iliyokabidhiwa kwa Jumuiya ya Yesu. Ipo katika zaidi ya nchi 90 na inaleta pamoja jumuiya za kiroho za watu zaidi ya milioni 22, waliojitolea kuishi kila siku kwa nia ya kushirikiana katika utume wa Kristo. Kiini cha utume huu ni nia za maombi za kila mwezi za Papa, ambazo zinatualika kuzingatia changamoto zinazowakabili wanadamu na utume wa Kanisa. Kwa kuanzishwa mwaka 1844 kama Utume wa Maombi, Papa Francisko aliianzisha mnamo Desemba 2020 kama Mfuko wa Vatican na kuidhinisha sheria zake za mwisho mnamo Julai 2024.
Sala kamili ya Papa Leo XIV:
Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina
Bwana wa uumbaji, Ulitupatia ardhi yenye rutuba, na pamoja nayo, mkate wetu wa kila siku,
kama ishara ya upendo wako na ya mapaji yako.
Leo tunatambua kwa uchungu kwamba mamilioni ya kaka na dada zetu wanaendelea kuteseka kwa njaa,
wakati chakula kingi kinapotea bure katika meza zetu.
Uamshe ndani mwetu ufahamu mpya: kwamba tujifunze kushukuru kwa kila lishe,
kuitumia bila majivuno, kuikaribishana kwa furaha na kutunza matunda ya ardhi kama zawadi yako,
unayoitoa kwa wote, wala si kwa wachache tu.
Ee Baba mwema, utuwezeshe kubadili mantiki ya matumizi ya chakula ya kibinafsi ili tujenge utamaduni wa mshikamano.
Ziwezeshe jumuiya zetu zihamasishe ishara hizi kwa matendo kama vile: kampeni za uhamasishaji, ghala za vyakula,
na mtindo wa kiasi wa maisha na wenye uwajibikaji.
Wewe uliyemtuma Mwanao Mpendwa, Yesu, mkate uliomegwa kwa ajili ya maisha ya ulimwengu,
utujalie moyo mpya, wenye njaa ya haki na kiu ya udugu.
Na kwamba asiachwe mtu yeyote nje ya meza ya pamoja, na Roho wako atufundishe kutazama mkate
si kama kitu cha kutumia, bali kama ishara ya umoja na matunzo.
Amina.
Sali na Papa: https://www.popesprayer.va/it/pregaconilpapa/
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here
