Wingo la mlipuko wa Bomu la atomiki,huko Hiroshima ulioharibu jiji hilo mnamo Agosti 6,1945. Wingo la mlipuko wa Bomu la atomiki,huko Hiroshima ulioharibu jiji hilo mnamo Agosti 6,1945.  Tahariri

Majisterio ya Mapapa na silaha ya atomiki

Maneno ya Warithi wa Petro dhidi ya silaha za nyuklia

Andrea Tornielli

Tangu janga lililosababishwa na mabomu ya atomiki huko Japani mnamo Agosti 1945, Kanisa limetafakari hatari ya binadamu kujiangamiza. Katika Ujumbe wake wa Radio wa siku ya Kuzaliwa kwa Bwana 1955, Papa Pio XII alizungumzia tishio la nyuklia, akielezea kwamba "hakutakuwa na kilio cha ushindi, bali kilio kisichofarijika cha wanadamu, ambacho kitatafakari kwa uchungu janga linalosababishwa na upumbavu wenyewe." Katika Waraka wa "Pacem in Terris," uliochapishwa mara baada ya Mgogoro wa Makombora ya Cuba, Papa Yohane  XXIII alisema kuhusu silaha za atomiki: "Binadamu wanaishi chini ya jinamizi la kimbunga ambacho kinaweza kutokea wakati wowote kwa nguvu isiyofikirika. Kwa kuwa silaha zipo; na ingawa ni vigumu kuamini kwamba kuna watu wenye uwezo wa kuchukua jukumu la uharibifu na mateso ambayo vita ingesababisha, haijatengwa kwamba tukio lisilotarajiwa na lisiloweza kudhibitiwa linaweza kuwasha cheche inayoanzisha mashine ya vita.

Mnamo Juni 1968, Papa  VI alisema: "Tunatumaini na tunaomba tena, kwa niaba ya wanadamu wote, kupiga marufuku kabisa ya silaha za nyuklia na upunguzaji wa silaha kwa ujumla na kamili." Wakati huo huo, Papa Yohane Paulo II,  mnamo Februari 1981 kutoka Hiroshima, alilia: "Mustakabali wetu katika sayari hii, ulio wazi kama ulivyo katika hatari ya kuangamizwa kwa nyuklia, unategemea jambo moja: ubinadamu lazima ufikie mabadiliko ya maadili. Katika wakati huu wa kihistoria, lazima kuwe na uhamasishaji wa jumla wa wanaume na wanawake wote wenye mapenzi mema. Ubinadamu umeitwa kupiga hatua zaidi mbele, hatua kuelekea ustaarabu na hekima. Mnamo Mei 2010, Papa Benedikto XVI alisema: "Ninahimiza mipango inayofuatilia upunguzaji wa silaha unaoendelea na uundaji wa maeneo yasiyo na silaha za nyuklia, kwa lengo la kuyaondoa kabisa kutoka katika sayari."

Papa Francisko, kutoka Hiroshima mnamo Novemba 2019, alikumbuka kwamba "matumizi ya nguvu ya atomiki kwa madhumuni ya vita, leo hii zaidi ya hapo awali, ni uhalifu si tu dhidi ya mwanadamu na hadhi yake, bali dhidi ya kila uwezekano wa mustakabali wa nyumba yetu ya pamoja." Aliongeza: "Matumizi ya nguvu ya atomiki kwa madhumuni ya vita ni kinyume cha maadili, kama vile kumiliki silaha za atomiki ni kinyume cha maadili, kama nilivyosema miaka miwili iliyopita. Tutahukumiwa kwa hili. Vizazi vipya vitasimama kama waamuzi wa kushindwa kwetu ikiwa tumezungumzia amani lakini hatujaifanikisha kupitia matendo yetu miongoni mwa watu wa dunia. Tunawezaje kuzungumzia amani huku tukijenga silaha mpya na za kutisha za vita? Tunawezaje kuzungumzia amani huku tukihalalisha vitendo fulani haramu kwa mazungumzo ya ubaguzi na chuki?"

Papa Leo XIV aliendelea kulingana na mwendelezo uliowekwa na majisterio ya watangulizi wake. Mnamo tarehe 14 Juni 2025, mwishoni mwa Katekesi ya Jubilei, alisema: "Hali nchini Iran na Israeli imezorota sana, na katika wakati mgumu kama huu, ninataka kufufua wito wangu wa uwajibikaji na busara. Ahadi ya kujenga ulimwengu salama zaidi, usio na tishio la nyuklia, lazima ifuatiliwe kupitia mikutano ya heshima na mazungumzo ya dhati, ili kujenga amani ya kudumu, iliyojengwa juu ya haki, udugu, na manufaa ya wote. Hakuna mtu anayepaswa kutishia kuwepo kwa mwingine."

Zaidi ya mwezi mmoja baadaye, katika ujumbe wa kuadhimisha miaka 80 ya mabomu ya atomiki ya Hiroshima na Nagasaki, aliandika: "Amani ya kweli inahitaji silaha kuwekwa chini kwa ujasiri, hasa zile zenye uwezo wa kusababisha janga lisiloelezeka. Silaha za nyuklia zinaudhi ubinadamu wetu wa kawaida na zinasaliti heshima ya uumbaji, ambao tunaitwa kulinda maelewano yao." Mnamo Agosti 6, katika Katekesi , akikumbuka mauaji yaliyosababishwa na silaha za nyuklia huko Japan, alitoa wito huu: "Licha ya kupita kwa miaka, matukio hayo ya kusikitisha yanaunda onyo la ulimwengu wote dhidi ya uharibifu unaosababishwa na vita na, hasa, na silaha za nyuklia. Natumaini kwamba katika ulimwengu wa leo, unaooneshwa na mivutano mikali na migogoro ya umwagaji damu, usalama wa uwongo unaotegemea tishio la uharibifu wa pande zote utaacha njia kwa vyombo vya haki, mazoezi ya mazungumzo, na uaminifu katika udugu."

Mrithi wa sasa wa Petro alirudi kwenye mada katika Ujumbe wake wa Siku ya Amani Duniani ya 2026, akisema: "Katika uhusiano kati ya raia na viongozi wa serikali, kushindwa kujiandaa vya kutosha kwa vita, kujibu mashambulizi, kujibu vurugu, kunaweza kusababisha kushindwa kwa hatia. Zaidi ya kanuni ya ulinzi halali, katika ngazi ya kisiasa, mantiki hii inayopingana ndiyo kipengele muhimu zaidi cha msukosuko wa kimataifa ambao kila siku unazidi kuwa wa kushangaza na usiotabirika. Sio kwa bahati mbaya kwamba wito unaorudiwa wa kuongezeka kwa matumizi ya kijeshi na maamuzi yanayotokana yanawasilishwa na viongozi wengi wa serikali huku kukiwa na uhalali wa hatari inayowakabili wengine. Hakika, nguvu ya kupotosha ya nguvu, na hasa kuzuia nyuklia, hujumuisha kutokuwa na mantiki kwa uhusiano kati ya watu ambao hautegemei sheria, haki, na uaminifu, bali hofu na utawala wa nguvu."

Mwishoni mwa Katekesi mnamo tarehe 4 Februari 2026, Papa Leo XIV alitangaza: "Kesho Mkataba Mpya wa START, uliosainiwa mwaka 2010 na Marais wa Marekani na Shirikisho la Urusi, unaisha. Mkataba huu uliwakilisha hatua muhimu katika kudhibiti kuenea kwa silaha za nyuklia. Katika kufufua moyo wangu kwa kila juhudi za kujenga zinazopendelea upokonyaji silaha na uaminifu wa pande zote, ninawasihi haraka msiache chombo hiki bila kutafuta kuhakikisha ufuatiliaji wake thabiti na mzuri. Hali ya sasa inatutaka tufanye kila tuwezalo ili kuepuka mbio mpya za silaha ambazo zinatishia amani zaidi miongoni mwa mataifa. Ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kubadilisha mantiki ya hofu na kutoaminiana na maadili ya pamoja yenye uwezo wa kuongoza chaguzi kuelekea manufaa ya wote na kufanya amani kuwa urithi unaolindwa na wote.”

Hatimaye, katika chapisho kutoka chapisho rasmi la Kipapa la Pontifex mnamo tarehe 5 Machi 2026, Papa Leo XIV aliandika: “Tuombe pamoja kwamba mataifa yaweze kuendelea kuelekea upunguzaji wa silaha kwa ufanisi, hasa upunguzaji wa silaha za nyuklia, na kwamba viongozi wa dunia waweze kuchagua njia ya mazungumzo na diplomasia badala ya vurugu.”

Hizi ndizo kauli za Papa, ambaye anaendelea kutoa wito wa kubomolewa kwa silaha zote za atomiki zilizopo zinazoweza kuharibu ubinadamu wote.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

17 Aprili 2026, 10:58