Maadhimisho ya Siku ya 102 ya Chuo Kikuu cha "Sacro Cuore," Milano, Italia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kunako mwaka 1919, watu watano mashuhuri akina Padre Agostino Gemelli, Ludovico Necchi, Francesco Olgiati, Armida Barelli pamoja na Ernesto Lombardo walianzisha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” “L'Università Cattolica del Sacro Cuore (UCSC) Jimbo kuu la Milano. Kilianza kufanya kazi rasmi tarehe 7 Desemba 1921 ili kujibu hitaji la mahali pa malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya nchini Italia, changamoto iliyovaliwa njuga na matokeo yake Chuo hiki kimeendelea kukua na kupanuka na hatimaye, kuwa ni jukwaa la malezi na majiundo ya kielimu kitaifa na kimataifa! Ni kati ya vyuo vikuu vya kikatoliki maarufu sana Barani Ulaya. Kuna wanafunzi zaidi ya 43, 302 wanaopata elimu bora na makini inayokidhi viwango vya soko la ajira Barani Ulaya. Ni Chuo kikuu ambacho kimewekeza sana katika elimu na tafiti makini, ili kuendelea kusoma alama za nyakati na hivyo kujibu kilio cha watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. Haya ni matokeo ya sadaka kubwa ya akili na ukarimu inayotekelezwa na wadau wa Jumuiya ya Chuo kikuu, bila kusahau kwamba, wanafunzi wana imani na wanathamini sana mchango huu mkubwa unaotolewa na Mama Kanisa. Elimu ni njia makini ya kujenga utu wa binadamu. Huu ni urithi mkubwa wa kiutamaduni na maisha ya kiroho unaotoa utambulisho wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore.” Kuelimisha maana yake ni kuwasha moto wa elimu unaoweza kushuhudiwa na mtu binafsi na jumuiya katika ujumla wake. Hii ni historia ya miaka zaidi ya 100 inayong’arishwa na imani, elimu, ujuzi na maarifa, tayari kujielekeza kwa siku za usoni na matumaini ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, huo ni utamaduni wa kutupa. Chuo kikuu ni mahali pa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini sanjari na mchakato wa malezi mtambuka yanayotekelezwa na wadau mbalimbali ndani ya jamii.
Baba Mtakatifu Leo XIV, katika hija yake ya kitume nchini Cameroon, Ijumaa jioni tarehe 17 Aprili 2026 alipata fursa ya kuihutubia Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika ya Kati, Taasisi inayojikita katika ubora wa utafiti, usambazaji wa maarifa na malezi ya vijana wengi, chemchemi ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya. Hii ni Taasisi iliyoanzishwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika ya Kati kunako mwaka 1989 kama kielelezo cha Kanisa Barani Afrika katika mchakato wa kutafuta ukweli, pamoja na kukuza haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mama Kanisa katika mafundisho yake mintarafu vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu, anasema kuwa hapa ni mahali pa kuragibisha utamaduni wa watu kukutana, kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi, kwa kujikita katika mchakato wa uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili, wote wakipania kutafuta ukweli na matumaini ili kukabiliana na ukosefu wa haki, usawa, vita na mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha ya kiroho; pamoja na mifumo mbalimbali ya umaskini katika ulimwengu mamboleo. Wanafunzi waliofundwa vyema, wanabadilika na kuwa vyombo na mashuhuda wa wema, haki na amani. Ni katika muktadha huu Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” “L'Università Cattolica del Sacro Cuore (UCSC) Jimbo kuu la Milano nchini Italia, Dominika tarehe 19 Aprili 2026 kimeadhimisha Siku ya 102 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Tajiriba ya Maarifa” inayosimikwa katika Injili ya upendo unaotangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa kama walivyofanya Mitume wa Yesu. Rej 1Kor 13:2.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Mario Delpini wa Jimbo kuu la Milano, Italia anakumbusha kwamba ujuzi hutokana na kupenda ujuzi, kwa sababu kitendo cha kujua ni matunda ya tamaa na msukumo maalum sana wa nafsi ya mwanadamu, hata kabla ya matumizi ya akili, ili hatimaye kukuza elimu ambayo inaepuka matumizi ya maarifa ya mzunguko mfupi na kiitikadi, na hivyo kuhakikisha maarifa ambayo, kwa kutambua ukweli na wema uliopo katika uhalisia, inaweza pia kutafsiri kuwa hekima kwa tunu ya maisha. Hayati Papa Francisko anasema, Chuo kikuu kinapaswa kuwa ni mahali pa malezi, makuzi na majiundo makini tayari kujikita katika tajiriba ya “Kerygma” yaani kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kujikita katika majadiliano katika ngazi mbalimbali; nidhamu, uadilifu na utu wema sanjari na matumizi bora ya mitandao ya kijamii, ili kupanua upeo wa ujuzi na maarifa unaokita mizizi yake katika haki.
Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, matumizi bora ya teknolojia ya akili unde yanahitaji kiwango cha kutosha cha uwajibikaji na maamuzi ya kimaadili, ili kuwawezesha vijana wa kizazi kipya kupata uwezo wa kufikiri kwa makini na kukua katika uhuru wa maisha ya kiroho na kwamba, mapinduzi ya kidijitali yanahitaji ujuzi wa kidijitali, elimu ya kibinadamu na kitamaduni ili kuelewa na kudhibiti utendakazi wa matumizi ya teknolojia ya akili unde. Baba Mtakatifu Leo XIV amegusia pia kuhusu uzinduzi wa mpango mkakati mpya wa maendeleo kwa ajili ya Bara la Afrika, ili kukuza na kueneza utamaduni wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu Kitaifa na Kimataifa; sanjari na dhamira ya kuimarisha maono ya Mafundisho Jamii ya Kanisa katika nyanja mbalimbali za maarifa; na hatimaye kustawisha maendeleo yake katika kukabiliana na changamoto mamboleo. Hizi ni sifa kuu za Chuo Kikuu cha Kikatoliki kinachojikita katika mchakato wa Uinjilishaji, elimu na utamadunisho wa imani ili kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na uzoefu wa watu mahalia.
