Jumatano, tarehe 22 Aprili 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mongomo. Jumatano, tarehe 22 Aprili 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mongomo.  (@Vatican Media)

Hija ya Kitume Papa Leo XIV Guinea ya Ikweta: Jubilei Miaka 170 ya Uinjilishaji

Papa Leo XIV katika mahubiri yake kwamba sasa ni zamu ya Waafrika kuwa wamisionari Barani Afrika na kwamba, wale wote waliojisadaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ni mwaliko kwa watu wa Mungu kwa nyakati hizi kuadhimisha Liturujia ya Kanisa kwa Ibada, kurutubisha imani yao kwa Kristo Yesu kwa kuimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; tayari kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji nchini Guinea ya Ikweta kuanzia mwaka 1855-2025, inanogeshwa na kauli mbiu “Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini” ni mwaliko kwa watu watakatifu wa Mungu nchini humo kuyaangalia yaliyopita kwa imani na kuanza kujielekeza katika hija ya imani na matumaini, ni wakati kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kuwasha tena moto wa imani kwa kuwaimarisha vijana wa kizazi kipya katika tunu msingi za Kiinjili, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa, huku wakiendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini humo. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumanne tarehe 21 hadi Alhamisi tarehe 23 Aprili 2026 anafanya Hija ya Kitume nchini Guinea ya Ikweta kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Kristo, Nuru ya Guinea ya Ikweta, Kuelekea Wakati Ujao wa Tumaini.”  Jumatano, tarehe 22 Aprili 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mongomo, Msimamizi na Mwombezi wa Guinea ya Ikweta, kama sehemu ya kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji. Ekaristi Takatifu ni kilele cha maisha na utume wa Kanisa, ni chakula cha Kanisa; Ni Kristo Yesu mwenyewe anayejisadaka kama chakula na kinywaji; Ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu na njia ya Mwenyezi Mungu kuweza kukutana na binadamu katika Ulimwengu mamboleo! Jubilei ya Miaka 170 ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa wema, upendo na ukarimu wake. Ni kipindi cha kuwashukuru kwa wale wote walijiojisadaka bila ya kujibakiza, kiasi cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya huduma kwa Habari Njema ya Wokovu. Ni watu waliobeba madonda ya watu wa Mungu nchini Guinea ya Ikweta, wakachangia kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu na kwamba, mateso na mahangaiko ni kielelezo cha uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Sasa Kanisa Barani Afrika linapaswa kujikita katika umisionari
Sasa Kanisa Barani Afrika linapaswa kujikita katika umisionari   (ANSA)

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Paulo VI alipotembelea kwa mara ya kwanza Bara la Afrika kwa kufanya hija ya kitume nchini Uganda kwanza kabisa aliitaka familia ya Mungu Barani Afrika kuwa mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake; kujenga na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu Barani Afrika. Alisema, viongozi wa kisiasa Barani Afrika wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa misingi ya haki, amani na maridhiano. Kanisa kwa kushirikiana na Serikali mbalimbali Barani Afrika zisaidie kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa: kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu, wanawake Barani Afrika wakipewa kipaumbele cha kwanza! Alilitaka Kanisa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, afya, kilimo na huduma bora za maji safi na salama.  Katika muktadha huu, Mtakatifu Paulo VI alikazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene Barani Afrika kama njia ya kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu. Alikazia pia umuhimu wa kukuza na kuendeleza mashirika na vyama vya kitume ili kusaidia majiundo, malezi na makuzi ya imani, tayari kuchangia katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu! Mtakatifu Paulo VI, katika hija yake ya kitume, aliwataka waamini kuiga mfano bora wa Mashahidi wa Uganda walioyamimina maisha yao kama kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Akawataka wawe jasiri na thabiti katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani. Ujasiri wa imani unawawezesha waamini kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao.

Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji wa kina
Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji wa kina   (@Vatican Media)

Hii ni historia endelevu na inayopaswa kukumbukwa anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake kwamba sasa ni zamu ya Waafrika kuwa wamisionari Barani Afrika na kwamba, wale wote waliojisadaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ni mwaliko kwa watu wa Mungu kwa nyakati hizi kuadhimisha Liturujia ya Kanisa kwa Ibada, kurutubisha imani yao kwa Kristo Yesu kwa kuimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; tayari kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi; mambo yanayohitaji rasilimali muda na sadaka, kama ilivyokuwa kwa Mitume na wafuasi wa Kristo Yesu katika Kanisa la Mwanzo, ingawa kati yao walilazimika kuzikimbia Jumuiya zao kutokana na madhulumu, lakini wakashuhudia uwepo angavu na endelevu wa Mungu kati pamoja nao kwa njia ya miujiza. Mdo 8:1-8. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha kwamba, mateso, shida na madhulumu ni mbegu ya Ukristo, changamoto na mwaliko wa kuzaa matunda ya ushuhuda wa furaha inayobubujika kutokana na Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mkate wa uzima unaoshibisha njaa na kuzima kiu ya mwanadamu! Rej. Yn 6:35.

Kauli mbiu: Kristo, Nuru ya Guinea ya Ikweta, Kuelekea wakati wa matumaini
Kauli mbiu: Kristo, Nuru ya Guinea ya Ikweta, Kuelekea wakati wa matumaini   (ANSA)

Kauli mbiu inayonogesha Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Guinea ya Ikweta ni: “Kristo, Nuru ya Guinea ya Ikweta, Kuelekea Wakati Ujao wa Tumaini.”  Watu wana njaa na kiu ya matumaini, haki inayozaa matunda ya amani na udugu wa kibinadamu. Huu ni wakati unaojengwa na kusimikwa katika neema na baraka za Mwenyezi Mungu. Mustakabali wa Guinea ya Ikweta unategemea uchaguzi wao makini; uwajibikaji na kwa dhamira ya pamoja ya kulinda Injili ya uhai na kusimama kidete kudumisha utu, heshima na haki msingi za kila mtu. Hii ni changamoto kwa Wabatizwa wote kujisikia kuwa wao ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu: kiroho na kimwili na hivyo kuwa ni mashuhuda na Mitume wa upendo na mashuhuda wa ubinadamu mpya na maendeleo endelevu ya binadamu yanapyaishwa. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, rasilimali, amana na utajiri wa nchi hii unakuwa ni baraka kwa watu wote wa Mungu, kwa kuendelea kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kulinda, kukuza na kudumisha utu na heshima kwa wote.

Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji wa kina
Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji wa kina   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV, mwishoni mwa mahubiri yake amewakumbuka kwa namna ya pekee wote wanaoteseka, maskini, wafungwa na watu wote wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kutokana na huduma mbovu za afya. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka watu wa Mungu Guinea ya Ikweta kuchukua hatima ya nchi yao mikononi mwao, kamwe wasiogope kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao; wawe ni wajenzi wa mustakabali wa matumaini, amani na upatanisho, kwa kuendeleza utume ulioanzishwa na wamisionari takribani miaka 170 iliyopita. Bikira Maria awaongoze katika safari hii, awaombee na kuwasaidia kuwa ni wanafunzi wakarimu na wenye furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Leo XIV kabla ya kuanza Ibada ya Misa Takatifu alipata nafasi ya kubariki Jiwe la Msingi la Kanisa kuu litakalojengwa kwenye Jiji la Amani, huko Guinea ya Ikweta. Hii ni baraka inayoashiria nguvu ya imani inayowaunganisha watu wa Mungu na hivyo kuwafanya kuwa ni ndugu katika Kristo Yesu; ndugu wa Baba mmoja katika upendo wa Mungu Muumbaji. Amewashukuru wote waliohudhuria katika siku hii muhimu na hivyo amewaombea heri na baraka itakayopyaisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa kurudia upya ahadi zao za kumfuasa Kristo Yesu katika Kanisa lake kwa uaminifu daima wakiunganishwa katika Kanisa Katoliki.

Watu wana kiu na njaa ya haki na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi
Watu wana kiu na njaa ya haki na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi   (@Vatican Media)

Kwa upande wake Askofu Juan Domingo-Beka Esono Ayang wa Jimbo Katoliki la Mongomo ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Guinea ya Ikweta, amesema kwa mara ya kwanza katika historia, kunako mwaka 1927 juhudi za uinjilishaji zilianza kushika kasi na tangu wakati huo, Kanisa limeendelea kujikita katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; katika malezi na majiundo ya watu wa Mungu: kitamaduni, kimaadili na kiroho kwa Kanisa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii kwa kutambua kwamba, “Furaha na matumaini, huzuni na mahangaiko ya wanaume na wanawake wa siku hizi, hasa wale walio maskini au wanaoteseka kwa njia yoyote ile, hizi ni furaha na matumaini, huzuni na mahangaiko ya wafuasi wa Kristo” Rej. Gaudium et spes, 1. Baraza la Maaskofu Katoliki Guinea ya Ikweta, linapenda kupyaisha uhusiano na urika wao katika mchakato wa uinjilishaji wa kina na Khalifa wa Mtakatifu Petro, katika kifungo cha amani, upendo na umoja. LG 23.

Jubilei Miaka 170 ya Uinjilishaji
22 Aprili 2026, 18:24