Papa Leo tarehe 22 Aprili 2026 amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya pamoja na familia, wote hawa ni mashuhuda wa furaha, maana, msukumo na uzuri wa maisha yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Papa Leo tarehe 22 Aprili 2026 amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya pamoja na familia, wote hawa ni mashuhuda wa furaha, maana, msukumo na uzuri wa maisha yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.   (@Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Guinea ya Ikweta: Vijana na Familia

Baba Mtakatifu Leo XIV kuwasha tena moto wa imani, matumaini na mapendo kwa kuwaimarisha vijana wa kizazi kipya katika tunu msingi za Kiinjili, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa, huku wakiendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini humo. Katika mkutano wake na vijana na familia zao wamegusia kuhusu: Umuhimu wa kazi, Wito wa Daraja Takatifu ya Upadre na Ndoa na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji nchini Guinea ya Ikweta kuanzia mwaka 1855-2025, inanogeshwa na kauli mbiu “Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini” ni mwaliko kwa watu watakatifu wa Mungu nchini humo kuyaangalia yaliyopita kwa imani na kuanza kujielekeza katika hija ya imani na matumaini, ni wakati kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kuwasha tena moto wa imani, matumaini na mapendo kwa kuwaimarisha vijana wa kizazi kipya katika tunu msingi za Kiinjili, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa, huku wakiendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini humo. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumanne tarehe 21 hadi Alhamisi tarehe 23 Aprili 2026 amekuwepo nchini Guinea ya Ikweta na Jumatano tarehe 22 Aprili 2026 amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya pamoja na familia, wote hawa ni mashuhuda wa furaha, maana, msukumo na uzuri wa maisha yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Guinea ya Ikweta ni nchi ambayo ina utajiri mkubwa wa historia na utamaduni unaojipambanua katika huduma, umoja, ukarimu na hali ya kuaminiana na katika kufurahia maisha. Vijana wa kizazi kipya wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wanaokumbatia imani, tayari kuishuhudia, kama msingi wa maisha yao na ya nchi yao kwa siku za usoni. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa maridhiano, upendo, upatanisho; kwa kuheshimu na kusimamia haki msingi za kila raia, familia na kila kikundi. Wasimame kidete kulinda, kutetea na kudumisha: Utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ni maneno kuntu yanayopaswa kuongoza nyoyo za watu wa Mungu nchini Guinea ya Ikweta. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu kuendelea kuwa waaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakichangia katika mchakato wa ustawi wa familia katika shughuli zao za kila siku.

Vijana wamechagua kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kazi
Vijana wamechagua kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kazi   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema ushuhuda unaonesha kwamba, vijana wamechagua kujikita katika utamaduni wa juhudi, maarifa, na nidhamu, ili kuwawezesha kufanya kazi kwa bidii. Wakristo wanahamasishwa kushiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kuwaheshimu watu wote, changamoto na mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu wa kila binadamu. Francisko Martin, ametoa ushuhuda juu ya uzuri na utakatifu wa wito wa Daraja Takatifu ya Upadre, ambamo vijana wanasadaka maisha yao yote kwa ajili ya Mungu na wokovu wa ndugu zao. Huu ni wito ambao unahitaji ujasiri na udumifu, ili kupata furaha ya kweli. Ni wito unaosimikwa katika maisha ya tafakari ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti za Kanisa na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu; huduma inayopyaisha tunu hizi msingi katika maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre na Maisha ya kuwekwa wakfu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana wa kizazi kipya, ikiwa kama wanajisikia kuwa na wito wa Kipadre au Maisha ya kuwekwa wakfu, kamwe wasisite kufuata nyayo za Kristo Yesu kwani anasema: “Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele.” Mt 19:29.

Vijana wachangamkie wito wa Upadre na Maisha ya kuwekwa wakfu
Vijana wachangamkie wito wa Upadre na Maisha ya kuwekwa wakfu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, familia ni udongo mzuri wa kustawisha tunu msingi za Kikristo na kiutu, mahali ambapo, tunu hizi zinazama na hatimaye kuota mizizi; ni mahali ambapo utakaso unafanyika, ili familia ziweze kukua na kuchanua katika umoja; mahali ambapo Injili ya uhai inakaribishwa na kupokelewa, katika safari ya kumwendea Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima. Rej. Yn 14:6. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha vijana kwamba, wengi wao walikuwa wanajiandaa kupokea Sakramenti ya Ndoa takatifu na kwamba, huu ni utume nyeti, agano linalopaswa kumwilishwa kila siku ya maisha, mahali pa kuendelea kugunduana, kwa jinsi wanavyoshirikiana na Mwenyezi Mungu katika kazi ya uumbaji, ili kuhakikisha kwamba, wanashirikisha furaha kati yao pamoja na watoto wao. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana wa kizazi kipya kukumbatia na kuambata wito wa ndoa na familia kama safari ya upendo wa kweli unaokuwa na kushamiri katika uhuru; kama safari ya matumaini inayozaliwa kutokana na ujuzi kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hatawaacha; na kama safari ya utakatifu, ambamo daima wanatafuta mema na furaha ya wengine.  

Papa Leo XIV amegusia uzuri wa maisha ya ndoa na familia
Papa Leo XIV amegusia uzuri wa maisha ya ndoa na familia   (@Vatican Media)

Kwa upande wake, Victor Antonio ameshirikisha historia ya maisha yake inayosimikwa katika ukweli, badala ya kuwakatisha watu tamaa, hii ni historia inayowatia moyo watu wa Mungu kujikita katika ujenzi wa Ulimwengu bora na mahali pazuri zaidi pa kuishi; kwa kuheshimu Injili ya uhai na kuwajibika kwa ajili ya ulinzi na utunzaji wa walio wadogo zaidi; kwa kupenda, kujisadaka na kutunza. Haya ni maneno yanayopaswa kuwaongoza watu wa Mungu kutafakari kwa uzito juu ya umuhimu wa kutunza na kulinda familia sanjari na tunu msingi ambazo watu wanajifunza ndani mwake. Ni mwaliko wa kutoa ushuhuda wa kanuni maadili na utu wema, hata pale sadaka inapohitajika, ili kupunguza chuki na dhana potofu kama Jaime Antonio na Purificación walivyosema.

Vijana wawe ni mashuhuda wa imani, upendo, haki, amani na maridhiano
Vijana wawe ni mashuhuda wa imani, upendo, haki, amani na maridhiano   (@Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anafafanua uzuri wa maisha ya ndoa na familia kwa kusema, kwamba wanandoa ni watu wenye hadithi zao za upendo ubinafsi, wanandoa wanaopendana huzaa maisha wanaweza kumpendeza Mwenyezi Mungu, Muumba na Mwokozi wao. Amoris laetitia, 9, 11. Watu wa Mungu wanahimizwa na kuhamasishwa na uzuri wa upendo; wawe ni mashuhuda wa upendo ambayo Kristo Yesu amewapatia na kuwafundisha, kwa kuonesha uzuri wa kupenda kila siku ya maisha na kwamba furaha kuu, katika kila hali, inatokana na kujua jinsi ya kutoa na kujitolea wenyewe, hasa wanapowaendea maskini na wahitaji zaidi.  Nuru ya upendo, inayotunzwa katika nyumba zao na hivyo kuwawezesha kuishi kwa imani, inaweza kweli kubadilisha ulimwengu na hata hata miundo na taasisi zake ili kila mtu aheshimiwe na wala hakuna mtu anayesahaulika.

Papa na vijana
23 Aprili 2026, 15:24