Hija ya Kitume Ya Papa Leo XIV Guinea ya Ikweta: Kanisa Barani Afrika & Elimu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji nchini Guinea ya Ikweta kuanzia mwaka 1855-2025, inanogeshwa na kauli mbiu “Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini” ni mwaliko kwa watu watakatifu wa Mungu nchini humo kuyaangalia yaliyopita kwa imani na kuanza kujielekeza katika hija ya imani na matumaini, ni wakati kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kuwasha tena moto wa imani kwa kuwaimarisha vijana wa kizazi kipya katika tunu msingi za Kiinjili, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa, huku wakiendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini humo. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumanne tarehe 21 hadi 23 Aprili 2026 anafanya Hija ya Kitume nchini Guinea ya Ikweta. Jumanne tarehe 21 Aprili 2026 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia wanaowakilisha Nchi zao pamoja na Mashirika ya Kimataifa, Wafanyabiashara maarufu pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia na kitamaduni. Baba Mtakatifu Leo XIV, na baadaye jioni alihutubia Mkutano wa Ulimwengu wa Utamaduni kwenye Chuo Kikuu cha Kitaifa, Kampasi ya León XIV, huko Malabo. Akiwa njiani kuelekea nchini Guinea ya Ikweta, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi 70 walioko kwenye msafara wake. Baba Mtakatifu Leo XIV ameukumbuka mchango, amana na urithi wa Papa Francisko katika maisha na utume wa Kanisa kwa hakika amekuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa Ulimwengu mamboleo; mragibishaji wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kanisa nchini Angola bado lina mchango mkubwa katika kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu mintarafu huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu, kwa ajili ya mafao ya wengi. Kanisa Katoliki kwa njia ya ushuhuda unaosimikwa katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili, linaweza kusaidia watu wa Mungu kufahamu haki zao msingi na hivyo kukoleza utekelezaji wa haki kwa wote. Baba Mtakatifu anasema, wazo la kuwatangaza Makardinali wapya bado linaendelea kufanyiwa kazi na kwamba, kuna uwezekano kwa Kanisa Katoliki Barani Afrika likapata Makardinali wapya, likiwemo Kanisa Katoliki nchini Angola. Baba Mtakatifu Leo XIV ameonesha furaha na matumaini yake makubwa kwa Kanisa Barani Afrika linaloendelea kuchanua na kucharuka katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni mwaliko wa kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa watu kuvutwa na uzuri, utakatifu na ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na wala si wongofu wa shuruti. Kanisa nchini Angola linaendelea kuongezeka na kupanuka na hivyo linahitaji kuanzisha Majimbo mapya na kuwasimika Maaskofu wapya wenye dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Changamoto hii inapaswa kufanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu kwa kushirikiana na Balozi wa Vatican nchini Angola. Kwa kufanya hivi, Maaskofu na Kanisa katika ujumla wake, litakuwa karibu zaidi na watu watakatifu wa Mungu.
Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Guinea ya Ikweta katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV azungumze na viongozi wa Serikali na wanadiplomasia amesema, hija hii ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV itasaidia sana kujenga na kuimarisha imani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini humo. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 90% ya wananchi wa Guinea ya Ikweta, iliyoinjilishwa takribani miaka 170 iliyopita ni waamini wa Kanisa Katoliki wanaotangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, hasa wakati wa kinzani na mipasuko ya kijamii katika ulimwengu wa utandawazi. Kwa hakika Baba Mtakatifu kutoka katika sakafu ya moyo wake, anahifadhi upendo kwa ajili ya watu wa Mungu nchini humo.
Baba Mtakatifu Leo XIV, katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Ulimwengu wa Utamaduni ulioandaliwa kwenye Chuo Kikuu cha Kitaifa, Kampasi ya León XIV, huko Malabo amekazia kwa namna ya pekee kabisa kuhusu: Umuhimu wa kuwekeza katika elimu kwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kutafuta ukweli sanjari na kutumia ujuzi na maarifa wanayopata kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; Mti wa Ceiba “Ceiba pentandra” unaojulikana kwa Lugha ya Kiswahili kama Msufi au Msufi-mwitu, ni alama ya Taifa la Guinea ya Ikweta wenye maana nzito, Mti wa Msalaba alama ya wokovu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu; Matunda ya Mti wa Ceiba yanakita mizizi yake katika mshikamano unaowezesha kupata maendeleo endelevu; kwa kutoa matunda ya akili na unyofu, ya umahiri na hekima, ya ubora na huduma, tayari kubadilisha maisha ili yawe ni zawadi kwa wengine na hivyo kutajirisha familia nzima ya binadamu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, uzinduzi wa Kampasi ya León XIV, unaonesha umuhimu wa kuwekeza katika elimu kwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kutafuta ukweli sanjari na kutumia ujuzi na maarifa wanayopata kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Chuo kikuu kinakuwa ni mahali pa watu kukutana na kuendelea kukua na kukomaa kama taasisi hai na kwamba, hii pia ni fursa ya ujenzi wa matumaini. Mti wa Ceiba unaojulikana kwa Lugha ya Kiswahili kama Msufi au Msufi-mwitu, ni alama inayobeba maana nzito kwa Taifa la Guinea ya Ikweta; changamoto na mwaliko kwa Chuo Kikuu kuwa ni taasisi iliyojikita vyema katika uzito wa masomo, katika kumbukumbu hai ya watu na katika kutafuta ukweli wa kudumu. Lengo ni kuiwezesha kukua kwa nguvu, kuboresha mawasiliano na hali ya historia iliyoko; kwa kuonesha kusudi la maisha kwa vijana wa kizazi kipya; kwa kutoa mafanikio ya kitaaluma, ili kutambua vigezo na nia ya kuhudumia. Katika Kitabu cha Mwanzo imeandikwa hivi: “BWANA Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.” Mwa 2:9. Hii inaonesha kwamba, mwanadamu amekirimiwa uwezo wa kufahamu, kutoa majina, kung’amua na kushangaa maana yake na kwamba, ufahamu, ujuzi na maarifa vimsaidie mwanadamu kufahamu ukweli wa mambo na kamwe ujuzi na maarifa visimfanye mwanadamu kujisikia kwamba, anajitosheleza mwenyewe, hali inayoweza kumsababishia kuchanganyikiwa na hatimaye, kukosa utu.
Mti wa Msalaba anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ni kielelezo cha Ukombozi; Ufunuo wa ukweli na siri ya Mungu. Rej. Kol 2:2-3; Ufunuo wa upendo unaonyannyua utu na heshima ya binadamu; kiu ya kutafuta ujuzi ili aweze kugangwa na kuponywa; kuutafuta ukweli katika unyenyekevu na kuhutumia kwa uwajibikaji mkubwa. Katika Kristo Yesu kuna uelewano kati ya ukweli na uwezo wa mtu kufikiri; Sababu na uhuru vinafunuliwa; ili uweze kutafutwa kwa uaminifu. Imani hutakasa na kuifungua kwa utimilifu ambao unapigania, hata kama haiwezi kuikumbatia kabisa. Kwa njia hii, mti wa Msalaba hurejesha kusudi la awali la kupenda maarifa. Hii ina maanisha kwamba kujua kunamaanisha kuwa wazi kwa ukweli, kuelewa maana yake na siri iliyomo. Kwa hivyo, utafutaji wa ukweli unabaki kuwa wa kibinadamu wa kweli: mnyenyekevu, makini na wazi kwa ukweli unaotutangulia, unaoita na kuwapita. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema ubora wa matunda ni muhimu, kwani mti utatambulikana kwa matunda yake. Rej. Mt 7:20. Kipimo cha Chuo Kikuu ni ubora wa wanafunzi wanaosoma Chuoni hapo, mkazo wa Mama Kanisa katika sekta ya elimu ni malezi na makuzi bora na wala si matokeo ya nje nje tu. Hii ni changamoto na mwaliko kwa Chuo Kikuu kuwa ni taasisi iliyojikita vyema katika uzito wa masomo, katika kumbukumbu hai ya watu na katika kutafuta ukweli wa huduma. Lengo ni kuiwezesha elimu kukua kwa nguvu, kuboresha mawasiliano na hali ya historia iliyoko; kwa kuonesha kusudi la maisha kwa vijana wa kizazi kipya; kwa kutoa mafanikio ya kitaaluma, ili kutambua vigezo na nia ya kuhudumia. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwapatia wingi wa baraka za Mwenyezi Mungu ambaye, katika Kristo Yesu Neno aliyefanyika mwili, ambaye amewaonesha ukweli kuhusu wao wenyewe na utu wao wa kweli, Rej. Gaudium et spes, 22; na hivyo kuwakabidhi wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Kikao cha Hekima, ili matunda haya yaweze kuwa tele na yawe pia mazuri.
Baba Mtakatifu Leo XIV amepata fursa ya kusikiliza shuhuda kutoka kwa mwanafunzi, jaalimu na mwakilishi kutoka katika Ulimwengu wa utamaduni: wamemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuonesha upendeleo wa pekee wa kuweza kukutana na vijana wa kizazi kipya, ili kuwatia shime, imani na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi; kwa kujikita katika mchakato wa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, kimaadili, kiutu na kijamii tayari kupambana na changamoto mamboleo katika maisha yao. Kama Maprofesa wanawajibika kushiriki kikamilifu katika malezi na majiundo kwa vijana wa kizazi kipya; kwa kuwasaidia kupata ujuzi na maarifa, ili elimu iwasaidia kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni dhamana inayo wadai Maprofesa kujitoa bila ya kujibakiza katika majiundo ya kiakili, tafiti, ili kukuza ufahamu wa kisayansi, kijamii na kiutu. Maprofesa ni amana na hifadhi ya ufahamu, ujuzi na maarifa, kumbe wanawajibika kurithisha maarifa haya kwa vijana wa kizazi kipya. Tafiti za kisayansi na teknolojia ni muhimu kwa huduma ya jamii, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; ili kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya: ukweli na usawa. Sayansi na imani ni medani mbili za maisha zinakumbatiana na kukamilishana. Sayansi na teknolojia ziwe ni kwa ajili ya huduma ya amani, maendeleo, utu na heshima ya binadamu.
