Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Barani Afrika: Huduma Kwa Wafungwa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wahudumu wa shughuli za kichungaji Magerezani kutoka sehemu mbalimbali za dunia tarehe 8 Novemba 2019 walikutana na kuzungumza na Hayati Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko aligusia kuhusu: matatizo yanayowakumba wafunga magerezani, umuhimu wa kuwa na mwono mpya kuhusu wafungwa na kwamba, huduma kwa wafungwa ni sehemu ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu ndilo ambalo limekabidhiwa dhamana ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafungwa magerezani, ili kuonesha wasiwasi na ukaribu wa Mama Kanisa kwa wafungwa wanaoteseka magerezani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni dhamana na wajibu wa Kanisa zima kama sehemu ya utekelezaji wa utume wake unaomwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu. Wakati wa hukumu ya mwisho, watu watahukumiwa kadiri walivyowatendea ndugu zake walio wadogo, na kwa kufanya vile, walimtendea Kristo Yesu mwenyewe. (Rej. Mt. 25:40) Kristo Yesu anajitambulisha kuwa kati ya watu wenye njaa, kiu, wageni, watu walio uchi, wagonjwa na wale walioko kifungoni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, taswira inayotolewa na magereza sehemu mbalimbali za dunia inaonesha ukweli wa jamii ambamo uchoyo, ubinafsi na utandawazi wa kutoguswa na mahangaiko ya jirani vinatawala. Kuna maamuzi ambayo yamefanywa kisheria lakini yanakiuka utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujidai kukuza na kutaka kudumisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Matokeo yake ni watu kutengwa na kutupwa magerezani kama suluhu ya matatizo mbalimbali yanayoisonga jamii. Lakini ikumbukwe kwamba, kuna kiasi kikubwa cha rasilimali na utajiri wa nchi unaotumika kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa magerezani, ikilinganishwa na kiasi cha fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuchochea kasi ya maendeleo fungamani ya binadamu, ambayo yangewezesha idadi kubwa ya wafungwa kupata kazi na kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya uvunjaji wa sheria.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ni rahisi sana kufumbia macho umuhimu wa elimu na malezi makini kwa jamii, sanjari na kushindwa kuona ukweli halisi wa matatizo na ukosefu wa haki na hivyo suluhu ya haraka inayoweza kupatikana ni ujenzi wa magereza, ili “kuwashikisha adabu wale wote wanaovunja sheria za nchi.” Umefika wakati wa kutoa msukumo wa pekee kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu kwa raia wote. Kwa bahati mbaya, magereza mengi yameshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuweza kutoa mafunzo bora zaidi, ili wafungwa wanapomaliza adhabu zao na kutoka magerezani waweze kuwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani. Ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, kuna uhaba mkubwa wa rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na changamoto za kijamii, kisaikolojia na kifamilia wanazokabiliana nazo wafungwa magerezani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, magereza yamegeuka kuwa ni mahali hatari sana, ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa. Mafunzo makini kwa wafungwa yanaanza pale ambapo wafungwa wanapewa fursa ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo, wanapopewa elimu makini na kufanyishwa kazi zenye staha. Yote haya lazima pia yazingatie huduma bora za afya kwa wafungwa pamoja na kuunda mazingira ambayo, wafungwa wataweza pia kushirikiana kwa karibu na raia wengine.
Jamii inapaswa kuwa na mwelekeo tofauti sana kwa wafungwa magerezani, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali, ili kuboresha maisha yao, kama sehemu ya faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kila mwamini awe ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa wafungwa, ili kuiwezesha jamii kukita mizizi yake katika misingi ya haki na amani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni nyenzo thabiti katika mchakato wa huduma kwa wafungwa magerezani. Huu ni mchakato unaowawezesha watu wa Mungu kutoa huduma kwa wafungwa na hivyo kujenga ndani mwao matumaini. Waamini waendelee kumtambua Kristo Yesu anayejitambulisha kati ya wafungwa magerezani. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wafungwa pamoja na familia zao, hasa katika kipindi hiki kigumu cha majaribio. “Njooni mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu.” Mt. 25:35.
Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 23 Aprili 2026 amefanya Hija ya Kitume ya Siku 10 kwa kutembelea: Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta kama hujaji na shuhuda wa matumaini, amani na upatanisho mkazo ni kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, ili kweli Afrika iwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Baba Mtakatifu Leo XIV amehitisha Hija yake ya Kitume Barani Afrika akiwa amebeba ndani mwake: Amana na utajiri wa imani, matumaini na mapendo. Hii ni hazina kubwa iliyojumuisha hadithi, nyuso, na shuhuda mbalimbali za furaha na huzuni, ambazo zinaendelea kuboresha maisha, utume na huduma yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kama ilivyokuwa kwenye Karne za Mwanzo za maisha na utume wa Kanisa, leo hii Kanisa Barani Afrika linaalikwa kuchangia kwa kiasi kikubwa utakatifu, ari, mwamko na utume wa kimisionari wa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa nchini Guinea ya Ikweta alipata fursa ya kutembelea Gereza Kuu la Bata lililoko Malaba na kuzungumza pamoja na wafungwa waliolowana kutokana na mvua kubwa iliyonyeesha mara tu baada ya kuanza hotuba yake, kielelezo cha baraka, ukaribu wa Mungu na kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwaacha waja wake. Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kusikiliza shuhuda za wafungwa na kwamba, hata katika mahangaiko, kamwe: Utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na matumaini, hayawezi kupotea na kwamba, hakuna mtu awaye yote anayetengwa na huruma na upendo wa Mungu na kwamba, kila mtu katika hali, makosa na historia yake anaendelea kubaki kuwa na thamani kubwa mbele ya Mungu, kama Kristo Yesu alivyowafunulia waja wake. Kristo Yesu aliwapenda wanadamu upeo, kiasi cha kuyamimina maisha yake, ili yawe ni chemchemi ya toba na wongofu wa ndani.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hija yake nchini Guinea ya Ikweta imemwezesha kupata tajiriba kwamba, hii ni nchi yenye utajiri wa tamaduni, lugha na mapokeo mbalimbali, changamoto ni kuendelea kuwekeza katika utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kuhakikisha kwamba, nguvu na uwezo wa kila mtu vinatumika kikamilifu. Haki jamii inalenga kuwasaidia wafungwa kujenga upya maisha ya wakosaji na wale waliokosewa, mwaliko kwa jamii nzima kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuganga na kuponya madonda yaliyojitokeza kutokana na ukosefu wa haki na kwamba, Injili ya matumaini ndio msingi wa mabadiliko ya ndani. Uwepo wao magerezeni ni fursa ya kufanya tafakari, upatanisho na ukuaji wa mtu binafsi. Yote haya yanawezekana ikiwa kama Gerezani wafungwa watapata fursa ya kusoma na kufanya kazi kwa heshima, kwani daima katika maisha ya mwanadamu kuna fursa ya kusimama tena na kuendelea kujifunza ili kuwa ni mtu mpya zaidi. Hata kama kati yao kuna wafungwa ambao wamejenga hisia ya kutopendwa na kutengwa na jamii, lakini wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwaacha na kwamba, Kanisa litaendelea kuwasindikiza na kwamba, vijana wa kizazi kipya wanahitaji kuona ushuhuda wa udumifu, uwajibikaji na imani thabiti; mambo yanayoweza kuwasha tena Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu Leo XIV aliwashukuru na kuwapongeza Maafisa wa Magereza wanaotekeleza dhamana, wajibu na huduma yao kwa kusimikwa katika: Usalama, heshima na utu wa kibinadamu, huku wakiendelea kuwasindikiza wafungwa kujenga na hatimaye, kurejea katika maisha yao ya kawaida, daima wasimike maisha yao katika Injili ya matumaini na kamwe wasiruhusu watu wachache kuwapoka matumaini yao, ili kwamba, kila siku iwe ni mwanzo mpya wa maisha yao.
Mwishoni Baba Mtakatifu Leo XIV aliiweka hija ya wafungwa hawa katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Huruma ya Mungu, ili awasindikize, awafariji na kuwalinda. Baba Mtakatifu mwishoni mwa hotuba yake, amewahakikishia sala na uwepo wake wa karibu, kwa kutambua kwamba, mtu aliyeteleza na kuanguka, anaposimama anakuwa imara zaidi na kwamba, Mwenyezi Mungu anawakirimia: amani, matumaini na nguvu za kuanza tena upya. Gereza hili lina wafungwa 651 kati yao wanaume ni 613 na wanawake ni 38. Lengo la Magereza ni kutoa fursa ya kuwa na mazingira salama yanayojali utu, heshima na haki msingi za binadamu; wafungwa waweze kupata fursa ya kupyaisha maisha yao, kwa kupatiwa fursa za elimu na mafunzo, ili kuwajengea mazingira ya kuweza kurejea tena katika jamii huku wakiwa ni watu wapya. Gereza hili linafuata pia Kanuni za Nelson Mandela (Nelson Mandela Rules), ambazo ni Kanuni za Msingi za Umoja wa Mataifa Kuhusu Wajibu wa Mawakili na Matibabu ya Wafungwa, mambo ambayo yameendelea kuwa mwongozo mkuu wa kimataifa wa haki za binadamu magerezani kufikia mwaka 2025. Mwaka 2025 unaadhimisha kumbukizi ya miaka 10 tangu kupitishwa kwa kanuni hizi zilizohuishwa.
