Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Barani Afrika: Cameroon: Haki na Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumatatu tarehe 13 hadi 23 Aprili 2026 anafanya hija ya kitume ya Siku 10 kwa kutembelea: Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta “Equatorial Guinea” kama shuhuda na mjumbe wa matumaini, haki, amani na upatanisho ili kweli Bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Kanisa ni chombo na shuhuda wa upatanisho, dhamana ambayo limepewa na Kristo Yesu! Akiwa nchini Cameroon, Baba Mtakatifu Leo XIV kama kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki anapenda kufahamu kwa ukaribu zaidi: matatizo, changamoto na fursa kwa watu wa Mungu nchini humo, na kwamba, anatembelea nchini humo kuanzia tarehe 15 hadi 18 Aprili 2026 kama mjumbe na shuhuda wa matumaini, hasa kwa vijana wa kizazi kipya; ili kuragibisha na kukoleza mchakato wa haki, amani na upatanisho, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Cameroon kuendelea kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi na hali ya kuheshimiana. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Cameroon mwaka 1985, 1995 na Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI alitembelea nchini humo mwaka 2009 kama sehemu ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Bara la Afrika kuanzia tarehe 4 hadi 25 Oktoba 2009: Kanisa Barani Afrika Katika Huduma ya Upatanisho, Haki na Amani.
Na sasa ni zamu ya Baba Mtakatifu Leo XIV anayetembelea Cameroon kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Umoja Katika Kristo.” Hii ni kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika kauli mbiu yake ya Kiaskofu “In Illo unum uno” Yaani: “Ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.” Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa mintarafu Zaburi ya 127.Baba Mtakatifu Leo XIV analitaka Kanisa kuwa ni chombo cha matumaini, haki, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatano, tarehe 15 Aprili 2026 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia wanaowakilisha Nchi zao pamoja na Mashirika ya Kimataifa, Wafanyabiashara maarufu pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia na kitamaduni. Katika hotuba yake amekazia kuhusu: Ujenzi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kusikiliza na kuzima kiu ya haki na amani, ili kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa ni mjumbe na shuhuda wa matumaini, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Cameroon na kwamba, uongozi ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Kwa hakika ulimwengu mamboleo una kiu kubwa ya amani, kumbe kuna haja ya kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuthamini mchango wa wanawake katika sekta ya elimu, ujenzi wa jamii pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ulinzi na usalama ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwa kuzingatia pia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kujenga msingi wa haki, amani na maridhiano. Ili kweli Serikali iweze kutekeleza dhamana na majukumu yake ya kitaasisi na kitaaluma kwa uadilifu na unyofu, haina budi kusimama kidete kulinda na kudumisha haki na amani, kwa kuvunjilia mbali minyororo ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma na kwamba, faida ya kweli inatokana na maendeleo shirikishi ya mwanadamu, yaani, kukua kwa uwiano wa vipengele vyote vinavyofanya maisha duniani kuwa baraka. Serikali ya Cameroon iwezeke kikamilifu katika sekta ya elimu, mafunzo na kuwaendeleza vijana, ili kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo inayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV amegusia pia mchango wa Kanisa Katoliki katika sekta ya elimu, afya na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu nchini Cameroon. Kumbe, kuna haja kwa viongozi wa kidini kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho, kwa kupinga misimano mikali ya kidini na kiimani, ili kudumisha utu wa binadamu na maridhiano. Ni katika muktadha huu, Kanisa linataka kujipambanua kuwa ni chombo cha ushirika, umoja na mshikamano na Mataifa mbalimbali.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 16 Aprili 2026 amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Jumuiya ya watu wa Mungu Bamenda, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Bamenda kama sehemu ya ujenzi wa amani nchini Cameroon. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake, amewakumbusha kwamba, yuko kati yao kama mjumbe wa amani, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya amani; kujenga na kudumisha uhusiano kati ya Waislam na Wakristo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Bamenda iwe ni chumvi, mwanga na mafuta ya faraja na matumaini, tayari kuganga na kuponya; kwa kuwekeza katika elimu na kwamba, faida inayopatikana katika uwekezaji kamwe isitumike katika kukuza na kudumisha utamaduni wa kifo, bali wajenge na kudumisha Injili ya amani kwani kimsingi wananchi wote wa Cameroon ni ndugu wamoja, kumbe wanapaswa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Watu wa Mungu wanapaswa kutambua na kuthamini utume wao duniani, kuwa ni wakuleta mwanga na baraka; ni utume unaohuisha, unaofufua na kuponya pamoja na kuwaweka watu huru; kwa kuwa pamoja na wengine na kwa ajili ya wengine. Rej. Evangelii gaudium 273. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Cameroon kutembea kwa pamoja kila mtu mintarafu wito wake, kwa kupanua mipaka ya jumuiya zao; kwa kupendana wao kwa wao na kuendelea kumshukuru Mungu kwamba, machafuko ya kisiasa nchini Cameroon, hayajageuka na kuwa ni vita ya kidini.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bamenda, Alhamisi tarehe 16 Aprili 2026 “Bamenda International Airport” amekazia pamoja na mambo mengine kwamba: Mwenyezi Mungu yuko karibu sana na wale wote waliovunjika na kupondeka moyo; hawa ni wale ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa kwa umaskini wa hali na kipato; baa la njaa, magonjwa, mmong’onyoko wa kanuni maadili na utu wema; watu wanaopekenywa na rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma. Yote haya ni chanzo cha chuki na uhasama kati ya watu wa Mungu nchini Cameroon. Huu ni wakati wa kujikita ujenzi wa umoja wa Kitaifa na Kimataifa, mahali ambapo Injili ya amani na upatanisho vinatawala. Huu ni wakati wa kujikita katika upya unaobubujika kutoka kwa Mungu, anayeumba upya, anayewakirimia watu ujasiri na kuwapatia nguvu ya kupambana na maovu, ili kujenga na kustawisha wema.Waamini wanaalikwa kuambana na kujikita katika ushuhuda kama ule wa Mitume kwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa kuwa waaminifu kwa Mungu, ili kujielekeza katika maisha mapya yanayowawezesha kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, leo hii imani haina budi kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na uzoefu wa watu mahalia na kwamba, Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuleta mabadiliko ya kweli nchini Cameroon.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 15 Aprili 2026 alipata fursa ya kutembelea Kituo cha Watoto Yatima cha Ngul Zamba, huko mjini Yaoundè na kuwashukuru Watawa wanaowahudumia watoto hawa na kwamba Kristo Yesu anaishi kati yao kama Kaka yao mkubwa na hivyo kuunda familia kubwa ya Mungu, mahali ambapo kila mtu anaheshimiwa na kuthaminiwa na kwamba, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alitoa kipaumbele cha kwanza kwa watoto na kwamba, uvumilivu wao ni kielelezo cha huruma ya Mungu. Rej. Mt 25:40. Huduma yao inajikita katika ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza sanjari na ujenzi wa familia kwa siku za usoni.
