Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 20 Aprili 2026 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika eneo la tambarale lililoko Saurimo, Angola. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 20 Aprili 2026 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika eneo la tambarale lililoko Saurimo, Angola.  (@Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Angola: Ibada ya Misa Takatifu Saurimo! Ekaristi!

Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake, alijikita zaidi katika Habari Njema ya Wokovu inayowasindikiza waamini kutambua lengo la ufuasi wao; Muujiza wa Yesu kuushibisha mkutano mkuu ambao haukumtafuta Mwalimu anayepaswa kupendwa, bali kiongozi anayeshangiliwa kwa ajili ya masilahi binafsi, mwaliko kwa wakristo kukutana na Kristo Yesu, ili awakirimie ujasiri wa kuwa ni wafuasi wake amini, tayari kushiriki utume na huduma kwa jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Angola kuanzia Jumamosi tarehe 18 hadi Jumanne tarehe 21 Aprili 2026, inanogeshwa na kauli mbiu “Papa Leo XIV, Hujaji wa Matumaini, Upatanisho na Amani, Ibariki Angola.” Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 20 Aprili 2026 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika eneo la tambarare lililoko Saurimo, Angola. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, alijikita zaidi katika Habari Njema ya Wokovu inayowasindikiza waamini kutambua lengo la ufuasi wao; Muujiza wa Yesu kuushibisha mkutano mkuu ambao haukumtafuta Mwalimu anayepaswa kupendwa, bali kiongozi anayeshangiliwa kwa ajili ya masilahi binafsi, mwaliko kwa wakristo kukutana na Kristo Yesu, ili awakirimie ujasiri wa kuwa ni wafuasi wake amini, tayari kushiriki utume na huduma kwa jirani zao.

Kristo Yesu ni chakula na kinywaji cha maisha ya uzima wa milele
Kristo Yesu ni chakula na kinywaji cha maisha ya uzima wa milele   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Kristo Yesu ni chakula cha uzima wa milele, mwaliko kwa wafuasi wake kutangaza Injili inayogeuza dhambi kuwa ni kielelezo cha msamaha na hii ndiyo imani inayookoa. Hii ni safari ya Kanisa la Sinodi ya ufufuko na matumaini na kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama walivyofanya mashuhuda wa imani na watakatifu, kwa kutangaza na kushuhudia matumaini, upatanisho na amani. Kristo Mfufuka anaendelea kuwaangazia na kuwapatia nguvu na kuwataka wafuasi wake, ili waweze kubadilika kadiri ya upendo wake na kwamba, Habari Njema ya Wokovu inawaimarisha katika kutambua lengo la ufuasi wao. Kristo Yesu, Neno wa Baba wa milele, alifanyika mwili ili kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni, kwa kuwafungua macho vipofu; kwa kutoa sauti kwa wale wanaonyanyaswa na kudhulumiwa; akawalisha wenye njaa na kiu ya haki; kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza. Katika muujiza huu, watu walikuwa wanamtafuta kwa ajili ya maslahi binafsi, kama mtoa huduma na wala hawakuguswa na mafundisho yake, kiasi kwamba, wakamezwa kwa fikra za imani ya kishirikina. Muujiza wa Yesu kuushibisha mkutano mkuu ambao haukumtafuta Mwalimu anayepaswa kupendwa, bali kiongozi anayeshangiliwa kwa ajili ya masilahi binafsi, mwaliko kwa wakristo kukutana na Kristo Yesu, ili awakirimie ujasiri wa kuwa ni wafuasi wake amini, tayari kushiriki utume na huduma kwa jirani zao na kamwe wasikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele. Rej. Jn 6:27. Na chakula hiki ni Kristo Yesu mwenyewe.  

Kristo Yesu anawalisha na kuwanywesha waja wake
Kristo Yesu anawalisha na kuwanywesha waja wake   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, zawadi ya Kristo Yesu inatoa mwanga juu ya hali ya sasa ya mwanadamu jinsi ambavyo tumaini la watu wengi linavyokatishwa tamaa na jeuri, inayotumiwa vibaya na wenye madaraka na kulaghaiwa na matajiri.  Kwa hiyo, dhuluma inapoharibu mioyo, mkate wa wote unakuwa miliki ya wachache.  Mbele ya maovu haya, Kristo Yesu anasikia kilio cha watu na kufanya upya historia yao kwa kuwainua kutoka katika kila anguko, akiwafariji katika kila mateso na kuwatia moyo katika utume wao. Ekaristi Takatifu ni mkate hai na historia yake haina mwisho. Kumbe, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu anafungua maisha ya waja wake na hivyo kuondoa mwisho wa historia yao ambayo ni kifo, kwani Kristo Yesu ni mkombozi wa dunia. Hii ndiyo Injili ambayo waamini wanashiriki na kuwafanya watu wote kuwa ni ndugu wamoja. Hii ndiyo Habari Njema inayogeuza dhambi kuwa ni chemchemi ya msamaha, kielelezo cha imani inayookoa maisha.

Waamini wanaalikwa kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka
Waamini wanaalikwa kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka   (@Vatican Media)

Ushuhuda wa Pasaka ni kwa ajili ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na kwamba huu pia ni ushuhuda wa ufufuko wa waja wake unaopata sauti kutoka kwa Kristo Yesu, kwani binadamu hakuzaliwa ili afe, awe mtumwa, anyanyaswe na kukandamizwa; aonje vurugu na unyonyaji; ukosefu wa uaminifu. Haya ni mambo yanayosigana na Ufufuo wa Kristo Yesu, zawadi kuu ya uhuru wa mwanadamu. Huu ni ukombozi endelevu katika maisha ya mwamini, kwani hii ni kazi ya Mwenyezi Mungu ambayo Wakristo wanapaswa kuiamini. Rej. Yn 6:29, mwaliko kwa waamini kumtolea Kristo Yesu shukrani, tayari kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya jirani zao na kwamba, Neno lake ni kanuni ya maisha na kipimo cha ukweli. Mzaburi anasema, “Heri ni wale waendao katika sheria ya Bwana” (Zab 119/118:1 Kumbe, katika mwanga wa ufuasi wao wa safari ya Kikanisa anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II, hii ni Sinodi ya ufufuo na matumaini, kwani mwamini akiwa na Injili moyoni mwake, atakuwa na ujasiri na kamwe hawezi kukatishwa tamaa na kwamba njia ambayo Mwenyezi Mungu amewafungulia waja wake haishindwi kamwe, kwani Kristo Mfufuka anatanguzana na waja wake, ili waishi Kisinodi.

Fumbo la Pasaka liwasaidie waamini kuishi Kisinodi
Fumbo la Pasaka liwasaidie waamini kuishi Kisinodi   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa imani, matumini na mapendo. Kwa kushiriki Ekaristi Takatifu, waamini wanageuka na kuwa ni vyombo vya huduma ya upendo, tayari kuwanyanyua wale walioteleza na kuanguka; na hatimaye, kujenga tena kifungo cha udugu wa kibinadamu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Shemasi Stefano, shuhuda wa imani. Rej. Mdo 6:8-15. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha mahubiri yake kwa kusema, kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama walivyofanya mashuhuda wa imani na watakatifu, kwa kutangaza na kushuhudia matumaini, upatanisho na amani na kwamba, Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya maisha mapya.

Kristo Mfufufka ni chemchemi ya furaha na maisha mapya
Kristo Mfufufka ni chemchemi ya furaha na maisha mapya   (ANSA)

Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Askofu mkuu José Manuel Imbamba wa Jimbo kuu la Saurimo, anasema, Jimbo kuu la Saurimo leo tarehe 20 Aprili 2026 kwa furaha na nderemo limempokea Baba Mtakatifu Leo XIV mjumbe wa matumaini, amani na udugu wa kibinadamu. Hili ni eneo ambalo bado linakabiliwa na changamoto za uinjilishaji wa awali, lakini kuna alama wazi na angavu za imani inayofasiriwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, mashuhuda hai wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika maisha ya mtu binafsi, familia, jamii na katika tamaduni. Uwepo wa Baba Mtakatifu Leo XIV kati yao umewaimarisha katika imani na kupyaisha matumaini na kwamba, wanaendelea kujizatiti katika ujenzi wa Kanisa, kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ujasiri wa kinabii, huduma kwa maskini kwa huruma na upendo, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa Angola inayosimikwa kwenye haki, amani na upatanisho. Hii ni changamoto ya kumwilisha upendo, amani na udugu wa kibinadamu, ili kurutubisha udugu wa kibinadamu, maisha ya kijamii, ushuhuda wa imani inayowaunganisha watu wote wa Mungu na kuwa ni kitu kimoja.

Ibada ya Misa Saurimo

 

20 Aprili 2026, 17:29