Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 18 Aprili 2026 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia na wawakilishi wa vyama vya kiraia na kitamaduni Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 18 Aprili 2026 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia na wawakilishi wa vyama vya kiraia na kitamaduni  (ANSA)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Angola: Hotuba Kwa Viongozi na Wanadiplomasia

Katika hotuba yake amesema, yuko kati yao kama hujaji anayetafuta dalili za uwepo wa Mungu nchini Angola. Ameonesha ukaribu wake kwa wahanga wa mafuriko makubwa yaliyolikumba Jimbo la Benguela. Amekiri na kutambua mshikamano wa watu wa Angola katika kuwasaidia waathirika wa mafuriko haya. Ameonesha nia yake ya kukutana na watu wa Mungu nchini Angola katika roho inayopata chimbuko lake katika amani, furaha ambayo si ngeni kwa huzuni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Angola kuanzia Jumamosi tarehe 18 hadi Jumanne tarehe 21 Aprili 2026, inanogeshwa na kauli mbiu “Papa Leo XIV, Hujaji wa Matumaini, Upatanisho na Amani, Ibariki Angola.” Anatembelea mji wa Luanda na Saurimo, kielelezo cha utajiri wa Angola; Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuangalia: changamoto na matumaini ya watu wa Mungu nchini Angola katika maisha na utume wa Kanisa mahalia; fursa, matatizo ya unyonyaji na ukandamizaji wa wafanyakazi kwenye machimbo ya madini, madhara yake katika mustakabali wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote nchini Angola. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anakaza kusema yeye ni shuhuda wa uhai wa Kanisa nchini Angola, mambo alioyaona wakati wa kumweka wakfu Monsinyo Germano Penemote kuwa Askofu mkuu na Balozi wa kwanza Vatican kutoka nchini Angola

Papa Leo XIV alipowasili Angola amepokea shada la maua.
Papa Leo XIV alipowasili Angola amepokea shada la maua.   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 18 Aprili 2026 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia wanaowakilisha Nchi zao pamoja na Mashirika ya Kimataifa, Wafanyabiashara maarufu pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia na kitamaduni kwenye Ikulu ya Angola. Katika hotuba yake amesema, yuko kati yao kama hujaji anayetafuta dalili za uwepo wa Mungu nchini Angola. Ameonesha ukaribu wake kwa wahanga wa mafuriko makubwa yaliyolikumba Jimbo la Benguela. Amekiri na kutambua mshikamano wa watu wa Angola katika kuwasaidia waathirika wa mafuriko haya. Ameonesha nia yake ya kukutana na watu wa Mungu nchini Angola katika roho inayopata chimbuko lake katika amani, furaha ambayo si ngeni kwa huzuni, hasira, kukatishwa tamaa na kushindwa; ni furaha ambayo hudumu na daima huzaliwa upya kati ya wale ambao wameweka mioyo na akili zao bila ushawishi wa utajiri wa mali inayotamaniwa na wengi, ili waweze kukwapua na kwamba, kuna umuhimu wa kuvunjilia mbali mzunguko huu wa maslahi ambayo hupunguza ukweli, na hata maisha yenyewe, kwa kuigeuza kuwa kama bidhaa.

Hija ya Kitume ya Papa leo XIV Angola 18-21 Aprili 2026
Hija ya Kitume ya Papa leo XIV Angola 18-21 Aprili 2026   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kwa dunia nzima Bara la Afrika ni chemchemi ya furaha na matumaini, fadhila ambazo ni za “kisiasa” matumaini ya vijana wa kizazi kipya kwa sasa na kwa maisha ya siku za usoni. Kwa hakika, hekima ya watu haiwezi kuzuiwa na itikadi yoyote, na hamu ya kutokuwa na mwisho ambayo inakaa ndani ya moyo wa mwanadamu ni kanuni ya mabadiliko ya kijamii ya kina zaidi kuliko programu yoyote ya kisiasa au ya kitamaduni. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema yuko katika yao kama kielelezo cha huduma ya mamlaka bora zaidi huhuisha watu na jumuiya na kwamba, Angola ina picha yenye mvuto mkubwa na kwamba, anapenda: kuwasikiliza na kuwatia moyo wale wote ambao tayari wamechagua njia za wema, haki, amani, uvumilivu na upatanisho. Sanjari na watu wote wenye mapenzi mema wanaounda utajiri msingi wa Angola. Ametumia fursa hii kuwaombea toba na wongofu wa ndani wale wote ambao wako kinyume cha maendeleo na upatanifu wa kidugu.

Papa Leo XIV amepata mapokezi ya kata na shoka nchini Angola
Papa Leo XIV amepata mapokezi ya kata na shoka nchini Angola   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna mateso, vifo na majanga ya kijamii yanayosababishwa na mantiki ya uchimbaji wa madini nchini Angola, kielelezo cha maendeleo baguzi, kipengele cha unyonge, ustaarabu wa kibiashara wa kupenda na kuthamini mali kama kikolezo cha maendeleo kwa siku za usoni hali ambayo vijana wa kizazi kipya wanaiona kabisa kuwa ni uwongo. Watu wa Angola ni mashuhuda kwamba, kazi ya uumbaji ni maelewano katika utajiri na utofauti na kwamba, wananchi wengi wa Angola wanateseka maelewano haya yanapokiukwa kutokana na kiburi cha watu wachache ndani ya jamii. Wananchi wa Angola wanabeba makovu ya unyonyaji, kumbe Bara la Afrika halina budi kuondokana kwa haraka na mienendo ya vita, kinzani, migogoro na uadui hali ambayo inasambaratisha mfumo wa kijamii na kisiasa wa nchi nyingi, na kuendeleza umaskini na ubaguzi. Ni katika mchakato wa watu kukutana tu, ndipo maisha yanachanua na kustawi na kwamba, majadiliano ni hatua ya kwanza hata kama migogoro na kinzani haziwezi kukosekana.

Baba Mtakatifu Leo XIV amepokea zawadi kubwa ya kinyago kutoka Angola
Baba Mtakatifu Leo XIV amepokea zawadi kubwa ya kinyago kutoka Angola   (@Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, migogoro inapojitokeza katika jamii kuna watu wanaotazama bila kufanya chochote, kuna wale wanao nawa mikono na kuendelea na maisha yao na wengine wanaukumbatia kiasi cha kuwafanya wafungwa, kwa kupoteza dira yao, kuchanganyiwa na kutoridhika kwao kwenye asasi na hivyo kufanya ujenzi wa umoja usiwezekane. Njia hii ni utayari wa kukabiliana na mgogoro uso kwa uso, kuutatua na kuufanya kuwa kiungo katika mnyororo wa mchakato mpya na kwamba, Heri wapatanishi! Rej. Evangelii gaudium, 227. Angola inaweza kufaidika na amana na utajiri mkubwa wa rasilimali za nchi ikiwa kama mawazo ya vijana wa kizazi kipya yatasikilizwa na kufanyiwa kazi; vita na kinzani zitaratibiwa na kufanywa kuwa ni chemchemi ya upyaisho; na ikiwa kama ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yatapewa kipaumbele cha kwanza kwa kukataa kutumia madaraka kwa ajili ya mafao binafsi; kwa kuwatenga na kuwagawanya watu; kwa kubomoa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na kuendelea kuwakatisha watu tamaa na kwamba, katika nchi nyingi duniani itikadi kali na ubaguzi zimekuwa ni zana za kisasa kama anavyosema, Papa Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii,” Fratelli tutti, 15.

Ilikuwa ni shangwe kubwa kwa watu wa Angola kumwona Papa Leo XIV
Ilikuwa ni shangwe kubwa kwa watu wa Angola kumwona Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, upendo, furaha na amani ni matunda ya Roho Mtakatifu. Gal 5:22 na kwamba, kila mmoja anaweza kupata fursa ya kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa sababu furaha ya kweli ni chemchemi ya upyaisho, maisha ya ndani ni kielelezo cha uhuru na kwamba, utamaduni wa watu kukutana ni sehemu ya ujenzi wa siasa bora na ya haki. Kanisa Katoliki nchini Angola litaendelea kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika maridhiano; jamii ambayo iko huru kutokana na mifumo mbalimbali ya ukoloni; kwa kutumia vyema karama na mapaji ya watu wa Mungu nchini Angola, bila kuwasahau watu wanaoishi vijijini. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha hotuba yake kwa viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia wanaowakilisha Nchi zao pamoja na Mashirika ya Kimataifa kwa kuwataka watu wa Mungu nchini Angola kuondoa vikwazo na vizuizi vya maendeleo kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mwanadamu; kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuendelea kutumaini pamoja na wale ambao Mwenyezi Mungu amewachagua na kuwawekea mbele zao na kwamba, hawa ni chemchemi ya tumaini lao. "Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni" (Zab 118:22), na kwamba, Kristo Yesu ni utimilifu wa mwanadamu na historia yake.

Hija ya Kitume Angola
19 Aprili 2026, 07:31