Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni tarehe 20 Aprili 2026 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST; Mapadre, Watawa, Makatekista na Wafanyakazi katika shughuli za kichungaji Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni tarehe 20 Aprili 2026 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST; Mapadre, Watawa, Makatekista na Wafanyakazi katika shughuli za kichungaji   (@Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Angola: Hotuba Kwa Viongozi wa Kanisa

Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake, amelishukuru Kanisa nchini Angola kwa kazi kubwa ya Uinjilishaji wa kina unaofanywa nchini humo, kwa ajili ya tumaini katika Kristo Yesu lililopandwa katika nyoyo za watu na kwa ajili ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Baba Mtakatifu Leo XIV amelishukuru Kanisa kwa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Angola mintarafu misingi imara ya upatanisho na amani; shukrani za pekee ni kwa Maaskofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Angola kuanzia Jumamosi tarehe 18 hadi Jumanne tarehe 21 Aprili 2026, imenogeshwa na kauli mbiu “Papa Leo XIV, Hujaji wa Matumaini, Upatanisho na Amani, Ibariki Angola.” Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 20 Aprili 2026 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika eneo la tambarare lililoko Saurimo, Kusini mwa Angola Baba Mtakatifu kabla ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumatatu tarehe 20 Aprili 2026 ametembelea na kuzungumza na wazee wanaotunzwa na Jimbo kuu la Saurimo, lililoko Kusini mwa Angola. Kituo hiki cha kutunzia wazee kinaitwa “Nyumba” ambamo wazee wanaishi katika mazingira ya kifamilia, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu alivyopenda kuwatembelea rafiki zake kama ilivyokuwa nyumbani mwa Mtakatifu Petro, Mtume na kwa rafiki zake Maria, Martha na Lazaro, hapo akakaribishwa kama Mwalimu. Baadaye jioni amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST; Mapadre, Watawa, Makatekista na Wafanyakazi katika shughuli za kichungaji pamoja na kusikiliza shuhuda mbalimbali katika maisha na utume wa Kanisa kutoka kwa watu wa Mungu nchini Angola kwenye Kanisa la Parokia ya Bikira Maria wa Fatima. Jumanne, tarehe 21 Aprili 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha hija yake ya Kitume nchini Angola. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake, amelishukuru Kanisa nchini Angola kwa kazi kubwa ya Uinjilishaji wa kina unaofanywa nchini humo, kwa ajili ya tumaini katika Kristo Yesu lililopandwa katika nyoyo za watu na kwa ajili ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Baba Mtakatifu Leo XIV amelishukuru Kanisa kwa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Angola mintarafu misingi imara ya upatanisho na amani; shukrani za pekee zinawaendea Maaskofu wanaosimamia mchakato wa kutangaza imani inayomwilishwa katika huduma ya upendo.

Papa Leo XIV akizungumza na wakleri, watawa na makatekista
Papa Leo XIV akizungumza na wakleri, watawa na makatekista   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Miaka 50 ya uhuru wa Angola; Moyo wa ukarimu katika wito wao, furaha ya kuwa Mitume wamisionari na kwamba mwaliko ni kuendelea kushikamana na Kristo Yesu, kwa kujifunza kutoka katika shule yake kwani: Yesu ni njia, ukweli na uzima; kwa kujenga na kuimarisha umoja kati ya Maaskofu na Mapadre wao na kuendelea kuwa waaminifu kwa maisha na wito wao. Baba Mtakatifu amewatia moyo kukuza ndani mwao hisia mpya ya upatanisho kwa kuwaelimisha watu wa Mungu nchini Angola katika njia za amani na kuthamini ushuhuda wa maridhiano kati ya watu wanaowahudumia, baada ya kuvumilia majaribu yenye uchungu, wameweza kuthubutu kusamehe, sasa ni wakati wa kufurahi pamoja nao na kusherehekea zawadi ya amani na kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake, amelishukuru Kanisa nchini Angola kwa kazi kubwa ya Uinjilishaji wa kina unaofanywa nchini humo, kwa ajili ya tumaini katika Kristo Yesu lililopandwa katika nyoyo za watu na kwa ajili ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi, ustawi na maendeleo yanayosimikwa katika msingi upatanisho na amani. Shukrani za pekee zinawaendea Maaskofu wanaotangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika huduma ya upendo. Amewapongeza viongozi wote wa Kanisa kwa sadaka na majitoleo yao kwa kuacha yote kwa ajili ya Injili na kwamba, watapata maradufu pamoja na udhia na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. Rej. Mk 10:29-30.

Papa Leo XIV amewapongeza Viongozi wa Kanisa kwa huduma makini
Papa Leo XIV amewapongeza Viongozi wa Kanisa kwa huduma makini   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV amewapongeza kwa kukumbatia wito wao, upendo kwa Kristo Yesu na jinsi wanavyowarutubisha watu wa Mungu kwa kweli za Kiinjili na kwamba, kwa kujisadaka zaidi, Kristo Yesu anawakirimia maradufu, mwaliko kwa viongozi hawa kumfungulia Kristo Yesu malango ya nyoyo zao, ili waweze kupata maisha ya kweli. Vijana walioko kwenye nyumba za malezi kamwe wasisite kuitikia wito wao na hivyo kumfuasa Kristo Yesu katika Mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili na kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wameweza kuingizwa katika familia hii kubwa ya Kanisa. Mwenyezi Mungu anawakirimia furaha ya kuwa Mitume wamisionari anawaimarisha ili kupambana na vikwazo katika maisha na hatimaye kuwajalia matumaini kama zawadi kutoka kwake. Wakumbuke kwamba, zawadi kubwa waliyoipokea katika maisha ni Roho Mtakatifu waliyempokea wakati wa Ubatizo anayewawezesha kufanana na Kristo Yesu mintarafu utume na maisha yao, tayari kushiriki katika ujenzi wa jamii ya Angola ambayo iko huru, nzuri na kwamba, hii ni jamii inayojipambanua kwa kujipatanisha. Baba Mtakatifu amewashukuru Makatekista hususan walioko Barani Afrika kwa mchango wao mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Jubilei ya Maadhimisho ya Miaka zaidi ya 50 ya uhuru wa Angola, yaani tarehe 11 Novemba 1975 na kwamba, nchi hii inapaswa kukita maisha yake katika Sheria ya upendo na matendo yao yaendelee kuwatambulishwa kwamba, wao ni wafuasi wa Kristo Yesu, kwa kuendelea kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Rej. Mt 5: 13-16. Na kwamba wao ni viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu yaani Kanisa, hivyo wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo, kwa kujenga jumuiya zao kutoka katika undani wa maisha yao na kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele. Waendelee kujizatiti katika majiundo endelevu, huku wakidumu kutangaza Injili ya amani.

Watu wa Mungu waendelee kujikita katika malezi na makuzi
Watu wa Mungu waendelee kujikita katika malezi na makuzi   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV analitaka Kanisa nchini Angola kuendelea kujifunza kutoka katika shule ya Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Rej. Yn 14;6; kwa majiundo endelevu ili kuwasaidia waamini wao kuondokana na imani za kishirikina. Majiundo haya yanapaswa kuonesha umoja wa maisha ya ndani, huduma binafsi na katika kujenga na kustawisha zawadi ya maisha na wito Mtakatifu kwa: Maisha ya sala na tafakari ya kina; kwa kujenga mazoea ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kujisomea; kwa kuimarisha umoja kati ya Maaskofu na Mapadre wao; kwa kuonesha mshikamano na maskini na kwamba, familia ni mahali ambapo watu wote wanatakatifuzwa pamoja na kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu. Kanisa linaheshimu na kuthamini taasisi ya familia kwani kila nyumba ni mahali ambapo washiriki wake wote wanatakaswa. Familia ni chimbuko la maisha na wito mtakatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wanafamilia wao, kwa kuwajali, kuunga mkono sanjari na kulinda wito wao. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahimiza viongozi wa Kanisa, kuendelea kuwa waaminifu kwa Injili ya Kristo Yesu na kamwe wasitafute faida binafsi. Familia ziwasaidie watoto kwa sala na kuwatia moyo kwa ushauri makini, ili hatimaye, waweze kuwa ni watakatifu na kwa njia ya mfano wa Kristo Yesu wawe ni watumishi wa wote.

Papa Leo XIV amepata fursa ya kusikiliza shuhuda za maisha na utume wa Kanisa
Papa Leo XIV amepata fursa ya kusikiliza shuhuda za maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka viongozi wa Kanisa kuendelea kuwa waaminifu kwa Angola, kama vile walivyoshikamana na wote waliokuwa wanateseka, kwa ujasiri wakapinga vita na hatimaye, wakaonesha suluhu ya ujenzi wa amani. Anawatia moyo kukuza ndani mwao hisia mpya ya upatanisho kwa kuwaelimisha watu wa Mungu nchini Angola katika njia za amani na kuthamini ushuhuda wa maridhiano kati ya watu wanaowahudumia, baada ya kuvumilia majaribu yenye uchungu, wameweza kuthubutu kusamehe, kumbe, sasa ni wakati wa kufurahi pamoja nao na kusherehekea zawadi ya amani na kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo. Kanisa nchini Angola liendelee kujipambanua kwa kushiriki katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika sekta ya elimu na afya; na kwamba, sasa kuna mashuhuda wa imani kutoka Angola wanaoendelea kuwa wamisionari sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni watu waliokita maisha yao kwenye tunu msingi za Kiinjili wakathubutu kumwaga damu yao, kuliko kusaliti haki, ukweli, huruma, upendo na amani kutoka kwa Kristo Yesu. Hawa ni watu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wokovu wa roho za ndugu zao. Watambue kwamba, Bikira Maria, Mama mwenye Moyo Safi “Mamã Muxima” daima yuko pembeni mwao!

Maaskofu wa Angola wakimsikiliza Papa Leo XIV
Maaskofu wa Angola wakimsikiliza Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Wakati huo huo, Askofu mkuu José Manuel Imbamba wa Jimbo kuu la Saurimo ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Angola, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV kuzungumza na watu wa Mungu, amegusia kuhusu kiu ya watu wa Mungu nchini Angola ya kupenda amani, maneno yaliyosikika kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Benedikto XVI wakati wa hija zao za Kitume nchini Angola na kamwe wasiogope kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Angola. Mkutano huu umehudhuriwa pia na wawakilishi wa dini na madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene na kwamba, Kanisa nchini Angola linaendelea kujizatiti katika shughuli za kimisionari kwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitatu unaonogeshwa na kauli mbiu: “Wanafunzi waaminifu, wanafunzi wenye furaha” Rej. Mdo. 11:23–26 na kwamba hiki ni kipindi sala na tafakari kwa ajili ya Makleri na Watawa, kama sehemu ya ushuhuda wa Kanisa katika maisha na utume wake, ili kuboresha huduma kwa watu wa Mungu.

Papa Leo XIV amewapongeza viongozi wa Kanisa
Papa Leo XIV amewapongeza viongozi wa Kanisa   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu, Maaskofu nchini Angola wameamua kuunda Taasisi ya Wamisionari wa Bikira Maria, Mama mwenye Moyo Safi “Mamã Muxima” ili kujibu mahitaji ya huduma za kimisionari ndani na nje ya Angola. Kanisa pia linaendelea kuwekeza katika malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya. Ushuhuda uliotolewa na Padre, Mtawa na Katekista, ulijikita kuhusu: Injili ya matumaini inayojikita katika shughuli za kichungaji, liturujia, katekesi na shughuli za kijamii; Huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; Malezi na majiundo ya Makatekista, tayari kuinjilisha na kutamadunisha kama sehemu ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya: haki, amani, maridhiano; ujenzi wa udugu wa kibinadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na matumizi bora ya maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Baba Mtakatifu Leo XIV aliporejea kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Angola alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Esperança Maria Eduardo Francisco da Costa, Makamu wa Rais wa Angola aliyekuwa ameongozana na wanafamilia wake.

Hotuba Kwa Maaskofu
21 Aprili 2026, 18:02