Askofu Mkuu Sarah Mullally Mkuu wa Jumuiya ya Kianglikan Akutana na Papa Leo XIV: Ushuhuda
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa katika maisha na utume wake anaendelea kukazia: Uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma, kwani uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni mbegu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 27 Aprili 2026 amekutana na kuzungumza na Askofu mkuu Sarah Mullally mwenye umri wa miaka 63; Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cantebury na Mkuu wa Jumuiya ya Kanisa la Kianglikani Duniani “The Anglican Communion (AC)” iliyoundwa kunako mwaka 1534 baada ya Kanisa la Uingereza kujitenga na Kanisa Katoliki kutokana na uamuzi wa Papa Clement VIII kukataa kuridhia Ombi la Mfalme Henry wa VII la kutaka kuvunja ndoa yake na Catherine wa Aragon. Askofu mkuu Sarah Mullally ni mwanamke wa kwanza kuiongoza Jumuiya ya Kanisa la Kianglikani Duniani, takribani miaka 1400 iliyopita. Ziara yake ya kitume mjini Vatican imekuwa ni fursa adhimu ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki sanjari na kutembelea na kusali kwenye Makanisa Makuu ya Kipapa yaliyoko mjini Vatican. Askofu mkuu Sarah Mullally katika hotuba yake kwa Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia umuhimu wa Wakristo katika hija ya majadiliano ya kiekumene kuendelea kuitikia wito wa kuishi na kutangaza kwa pamoja Habari Njema ya Wokovu, katika uwazi na upya mbele ya jeuri, kinzani na migawanyiko, mabadiliko makubwa ya kijamii na kwamba, wanapaswa kuendelea kusimulia Injili ya matumaini kwamba, maisha yana thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Familia ya binadamu inaitwa kuishi katika udugu wa kibinadamu, kwa kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu wa Mungu. Watambue kwamba, maskini wana upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Kristo Mfufuka ameshinda nguvu za dhambi na mauti.
Askofu mkuu Sarah Mullally amempongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa ujumbe wake wa matumaini dhidi ya udhalimu unaomwandama mwanadamu katika Ulimwengu mamboleo. Hija yake ya Kitume Barani Afrika, ilisheheni maisha na furaha ya Injili, ujumbe mahususi kwa walimwengu. Licha ya mateso na mahangaiko mbalimbali, binadamu anatamani maisha katika utimilifu wake, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu mkuu Sarah Mullally amemwambia Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, mwezi Julai 2026 anatarajia kufanya hija ya kitume nchini Ghana na Cameroon, ili kuimarisha Umoja wa Kanisa Anglikani. Amemshukuru kwa Sala ya Kiekumene na kwamba, ataendelea kuungana na Baba Mtakatifu Leo XIV kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia; Sala kwa ajili ya kuombea haki na kwamba, kila mtu aweze kupata utimilifu wa maisha mintarafu mapenzi ya Mungu na kwamba, kwa njia ya Kristo Yesu wameweza kuunganisha sala zao mbele ya Mwenyezi Mungu. Ametumia fursa hii, kumwalika Baba Mtakatifu Leo XIV kutembelea Uingereza panapo majaliwa. Kwa pamoja wamesali kwenye Kikanisa cha Papa Urbano VIII.
Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Leo XIV ameonesha furaha kubwa ya kuweza kukutana na kuzungumza na Askofu mkuu Sarah Mullally katika kipindi hiki ambacho Mama Kanisa bado anaendelea kuadhimisha Sherehe ya Pasaka ya Bwana. Huu ni mwendelezo ya Majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika sala pamoja na jitahada za pamoja za kujenga na kudumisha amani kwa kuendelea kuwa ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa Injili ya amani. Hii ni changamoto kwa Wakristo wote kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Injili ya amani sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, utengano kati ya Wakristo unadhohofisha juhudi hizi za kutangaza na kushuhudia amani na kwamba, kuna haja ya kuendelea kung’oa vizuizi vinavyokwamisha utangazaji na ushuhuda wa Injili kwa pamoja, kwa kujenga umoja kamili, kwa kujitahidi kuvuka vikwazo na changamoto mamboleo, ili kwa pamoja waweze kutekeleza wito wao wa kumfahamu, kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hii ni changamoto kwa Wakristo kuendelea kutembea kwa pamoja katika urafiki, majadiliano ya kiekumene na maisha ya sala, ili Roho Mtakatifu aweze kuongoza hatua zao katika sala, unyenyekevu na kuendelea kujikita katika ujenzi wa umoja wa Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Mungu kwa wafuasi wote wa Kristo Yesu.
