Papa Leo XIV,Torrevecchia:Kila kitu hubadilishwa kwa kukutana na Bwana!
Angella Rwezaula - Vatican.
Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Leo XIV, jioni ya Domenika ya Tatu ya Kwaresima, tarehe 8 Machi 2026 ametembelea Parokia ya Uwasilishaji wa Mtakatifu Maria Hekaluni huko Torrevecchia, Mashariki mwa Roma. Katika mahubiri yake kwa kuongozwa na Injili alianza kueleza kuwa: “Ninafurahi Dominika hii ya tatu ya Kwaresima kuwa miongoni mwenu. Ni hatua muhimu katika kumfuata Yesu, inayoongoza kwenye Pasaka yake ya Mateso, Kifo na Ufufuko. Katika safari hii, ukaribu wa Mungu na maisha yetu ya imani vimefungamana sana: akipyaisha neema ya Ubatizo ndani ya kila mmoja wetu, Bwana anatuita kwenye uongofu, hata kama anavyotakasa mioyo yetu kwa upendo wake na kazi za upendo anazotualika kuzifanya.”
Kiu ya Mwanamke msamaria ni kiu yetu
Papa aliongeza: “Katika suala hilo, kukutana kati ya Yesu na mwanamke Msamaria kunatuvutia kwa nguvu kubwa. Kiukweli, Injili ya leo hii haizungumzi nasi tu, bali pia inatuzungumzia na kutusaidia kufikiria upya uhusiano wetu na Mungu. Kiu ya mwanamke Msamaria ya uzima na upendo ni kiu yetu: ile ya Kanisa na ya wanadamu wote, waliojeruhiwa na dhambi lakini iliyojaa zaidi hamu ya Mungu. Tunamtafuta kama maji, Papa aliongeza “hata wakati hatutambui, kila wakati tunapohoji maana ya matukio, kila wakati tunapohisi jinsi tunavyokosa mema tunayotamani sisi wenyewe na kwa wale wanaotuzunguka. Katika utafutaji huu, tunakutana na Yesu. Tayari yuko pale, kisimani, ambapo mwanamke Msamaria anamkuta peke yake, chini ya jua la adhuhuri, amechoka na safari.”
Kristo anamfunua Mungu wa Mshangao
Mwanamke anakwenda kisimani wakati huo usio wa kawaida, labda ili kuepuka sura za chuki za wanawake wengine. Yesu anasoma moyoni mwake sababu ya kutengwa huku: ndoa zake zilizoshindwa na kuishi pamoja kwa sasa kunamfanya asistahili kusindikizwa na binti, wake wengine, na mama wa kijiji hicho. Na bado, Yesu anakaa kando ya kisima kana kwamba anamngojea. Mkutano huu wa kushangaza ni mojawapo ya njia ambazo, kama Papa Francisko alipenda kurudia, Kristo anamfunua Mungu wa mshangao: mzuri zaidi, ni ule unaobadilisha maisha ya mtu, popote wanapokutana naye na jinsi anavyojionesha mbele za Bwana.”
Papa Leo XIV alisisitiza kuwa “Mwanamume huyu anampenda mwanamke Msamaria kama ambavyo hapakuwa na mtu hapo awali. Alipokuwa akitafuta maji ya kila siku, anataka kumpa maji mapya, yaliyo hai, yenye uwezo wa kuzima kila kiu na kutuliza kila wasiwasi, kwa sababu maji haya yanatoka moyoni mwa Mungu, utimilifu usioisha wa kila matarajio. Kwa hivyo mpango wa Yesu unaanzisha utafutaji wa kitu bora zaidi kuliko maji yenyewe: "Kama ungalijua zawadi ya Mungu," Bwana anamwambia mwanamke.”
Mwana wa Mungu anatoa zawadi ya Uzima
Hii si lawama, bali ni ahadi: "Mimi niko hapa kukutambulisha kwa Mungu, anayejitoa kwako." Ndiyo, hasa kwa ajili yako, ambaye hukumjua, ambaye ulijiona kuwa mbali na mwenye hatia. Zawadi hii itakubadilisha: wewe mwenyewe utakuwa chemchemi inayobubujika hadi uzima wa milele. Badala ya kiu yako ya awali, iliyojaa uchungu na ukame wa kiroho, Mwana wa Mungu anatoa zawadi ya uzima uliopyaishwa na maji yanayotiririka kutoka katika huruma ya Baba. Kila kitu hubadilishwa katika kukutana na Bwana: mwanamke mwenye kiu anakuwa chemchemi, mtu aliyetengwa anakuwa na ujasiri. Mwanamke aliyejaa aibu sasa amejaa furaha; yule aliyekaa kimya kijijini anakuwa mmisionari kwa wakazi wake wote. Asingeweza kufikiria kwamba yeye, akiwa amechanganyikiwa na kushindwa na maisha, siku moja angeweza kuonja maji safi, zawadi safi kutoka kwa Mungu, na kuwa zawadi kwa wengine.”
Yesu ni Mwanaume, nabii, Masiha na Mwokozi
Papa aliuliza swali “Hili linatokeaje? Kwa kukutana na Yesu, kwa kuzungumza naye, Neno lililo hai la Mungu lililofanyika mwanadamu kwa ajili ya wokovu wetu. Masimulizi ya Injili yanaonesha kwa makini safari ya ukuaji wa mwanamke, anapotambua hatua kwa hatua sifa za msingi za utambulisho wa Yesu: mwanaume, nabii, Masiha, na Mwokozi. Kwa kusimama kando Yake na kufurahia kuwa Naye, naye mwanamke Msamaria anakuwa chanzo cha ukweli. Maji mapya ya zawadi ya Mungu yameanza kujaa moyoni mwake, na mara moja anahisi kulazimika kurudi kijijini kwake, hatimaye akiwa huru kutokana na aibu na akiwa na hamu ya kumjulisha Mkombozi wake kwa wote, Yesu, Yule aliyewezesha maajabu hayo yote,” Papa alisisitiza. Kwa njia hiyo “Anamkimbilia yule yule aliyemhukumu hapo awali, kama vile Mungu alivyomsamehe, na anasema, anatangaza, anashuhudia. Haja ya maji, ambayo ilimpeleka kisimani, sasa inatoa nafasi kwa hamu ya kushiriki upya mwingi uliombadilisha.”
Neema ya maji huosha kila dhambi na kuzima kila kiu
Papa Leo XIV aliendelea kudadavua Injili kwamba, “Wapendwa marafiki, kwa Ubatizo sote tumepokea neema ya maji mapya, ambayo huosha kila dhambi na kuzima kila kiu. Kama mwanamke Msamaria, vivyo hivyo leo hii katika Kwaresima tumepewa muda wa kugundua tena zawadi ya Sakramenti hii ambayo, kama mlango, imetuingiza kwenye imani na maisha ya Kikristo. Kama Mchungaji mwema na anayejali, Bwana anatusubiri na anatusindikiza kila wakati, popote tunapoishi na jinsi tulivyo. Kwa huruma huponya majeraha yetu na kuwa zawadi kwetu, akituwezesha kuwa zawadi kwa kaka na dada zetu.
Papa Leo XIV akijikita na muktadha wa Parokia ya pembezoni: “ Ninajua vyema kwamba jumuiya ya parokia yenu inaishi katika eneo lenye changamoto mbalimbali. Hapakosekani uhaba wa kutengwa, umaskini wa kimwili na kimaadili. Hata vijana na barubaru wana hatari ya kukua wakidanganywa na wahalifu wa kifo au kukata tamaa kuhusu mustakabali wao. Wengi wanasubiri nyumba, kazi inayohakikisha maisha yenye heshima, mazingira salama ambapo wanaweza kukutana, kucheza, na kupanga kitu kizuri pamoja. Kama vile kwenye kisima katika Injili, wanaume na wanawake wanafika katika parokia hii wakiwa wamejeruhiwa katika roho zao, wakiwa wamechukizwa na heshima yao, na wakiwa na kiu ya matumaini.”
Papa pongeza kazi yao ya haraka na ya ukombozi
Baba Mtakatifu amewapongeza: “Kazi yenu ya haraka na ya ukombozi ni kuonesha ukaribu wa Yesu, hamu yake ya kukomboa uhai wetu kutoka katika maovu yanayoutishia kwa pendekezo la maisha ya haki, ya kweli, na yenye kuridhisha. “Kuanzia na Ekaristi, moyo unaodunda wa kila jumuiya ya Kikristo, aliwahimiza “kuhakikisha kwamba shughuli za parokia ni ishara ya Kanisa ambalo, kama mama, linawajali watoto wake, bila kuwahukumu, bali linawakaribisha, linawasikiliza, na kuwaunga mkono wakati wa hatari.” Neno la Injili, ambalo linachipuka ndani yetu kama chanzo cha ukweli, limsaidie kila mmoja wetu kufungua macho yetu, ili kuweza kutathmini kwa busara yaliyo mema na yaliyo mabaya, hivyo kutengeneza dhamiri huru na za watu wazima.” Askofu wa Roma aliwasihi wasonge mbele “kwa kujiamini! Katika kila hali, Bwana anatembea nasi na kutuunga mkono njiani. Bikira Mtakatifu sana awasindikize na hatua zenu kwa imani kila wakati, na awape furaha ya kuwa watangazaji wanyenyekevu na jasiri wa Injili yake”.
Waliohudhuria misa hiyo walikuwa Kardinali Baldo Reina, Makamu wa Papa Jimbo Kuu la Roma, Paroko wa Parokia Paolo Stacchiotti, na mapadre wengine wanaohuisha maisha ya Parokia ya Uwasilishaji wa Mtakatifu Maria Hekaluni huko Torrevecchia, Padre Jokens Antony na Padre Richard Kenneth na mapadre wengine wengi walishiriki. Katika viti vya mbele Kanisani pia kulikuwa na waamini ambao ni wahusika wakuu wa maisha ya Kanisa hilo la kitongoji cha pembeni mwa Roma na ambao, kwa huduma yao ya kujitolea, wanajaribu kuzuia matatizo wanayopitia.
Asante kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here
