Mtoto akitazama mji wa Gaza ukigeuka vifusi. Mtoto akitazama mji wa Gaza ukigeuka vifusi. 

Papa:Tuwe kama watoto na macho safi ya kutazama uhalisia ili tubaki wanadamu

Papa Leo XIV alituma barua yake iliyoelekezwa kwa mhariri wa"Avvenire"Marco Girardo,na kwa wasomaji wa "Popotus,"nyongeza ya kila Juma inayojikita na masuala ya watoto katika fursa ya maadhimisho ya miaka 30.Papa anahimiza kutowaacha kwani wanaweza kupata marafiki bora au mjumbe wa maarifa yote katika vibodi vya mazungumzo ya AI,hivyo kudhoofisha ujuzi wao wa akili na uhusiano.Ili kubaki binadamu,tunahitaji kudumisha mtazamo kama wa kitoto kuhusu ukweli.

Vatican News

"Katika siku hizi zenye wasiwasi mkubwa kuhusu vita vinavyotishia mustakabali wa wanadamu," ni lazima tuwatazame watoto ili macho yao "yaliyopotea" yaweze kuwaongoza kwenye uongofu wa kweli. Ni lazima pia tuwe kama watoto zaidi, tukiwa na "macho safi" ya kutazama uhalisia ili "tubaki wanadamu." Ndivyo Baba Mtakatifu Leo XIV anaandika katika Barua yake kwa Wasomaji wa Popotus, nyongeza za Kurasa kwenye Gazeti Katoliki la Avvenire zinazojikita na masuala ya watoto, kwa kuadhimisha miaka thelathini tangu kutolewa toleo lake la kwanza mnamo tarehe 23 Machi 1996.

Hatari za Enzi ya Kidijitali na AI

Katika barua yake, iliyotumwa kwa mkurugenzi wa Gazeti hilo Marco Girardo, Papa anashukuru chapisho hilo kwa kazi yake ya kusambaza matukio ya sasa kwa watoto: "Habari njema zinazotutia moyo, na habari mbaya zinazoweza kutufundisha kutorudia makosa yaleyale." Kwa kuzingatia hili, Papa anawasihi wazazi na walimu kuwalinda watoto "kutokana na wazo lisilo la kibinadamu la habari na la elimu." Sote tunahitaji elimu ya maisha yote, hasa leo, katika enzi ya kidijitali na akili Unde(AI). Na ili kubaki binadamu, tunahitaji kuhifadhi mtazamo kama wa mtoto kuhusu ukweli.

Papa anatoa onyo wazi kwamba "watoto wasije wakaamini kwamba wanaweza kupata marafiki zao wa karibu au mjuzi wa maarifa yote katika vibodi (Chatbot) vya mazungumzo ya Akili unde( AI,) hivyo kupunguza akili na ujuzi wao wa mahusiano, kupunguza ubunifu wao na mawazo yao." "Lazima tulinde utoto hao," Papa Leo alihimiza, "na kuongoza ukuaji wao ili waweze kuwa wahusika wakuu wa ulimwengu mpya."

Kurejesha uzuri wa Ulimwengu

Hakika, "kurejesha uzuri kwa ulimwengu kunawezekana," Papa Leo XIV aliwahakikishia  watoto wasomaji. "Mnaweza kuwasaidia wazee kuiona, kupitia gazeti hili lililokusudiwa kwenu ninyi, kwa mshangao mpya wa neema yake, kulifikiria kwa uaminifu, na kulijenga bila ubaguzi." Papa Leo XIV kwa kuwakumbuka wasomaji wa leo na wale wa jana ambao kwa sasa wanatimiza miaka 30, alieleza kwamba, "mnapokua, mtagundua mambo mapya kila wakati, mtajenga mambo mapya wenyewe; lakini kuna mambo ambayo lazima myathamini kila wakati kutoka miaka hii ya mwanzo ya maisha yenu: waamini wale wanaowapenda, lugha ya upendo ya ulimwengu wote, nguvu ya kuondoa tabasamu, ujasiri wa kuomba msamaha, na uzuri wa kufanya amani."

Mtazamo kwa Macho Safi

Papa anakumbusha maneno ya Yesu kwa wanafunzi wake: "Msipoongoka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni." Ujumbe ambao bado unafaa leo hii: "Kuwa kama watoto," alisisitiza tena, "sio kurudi nyuma, bali ni ufunguo wa kuona kiini cha kila kitu, kupata majibu ya kushangaza hata kwa maswali magumu zaidi." Labda ni kwa kutazama macho ya watoto waliochanganyikiwa na wanaokabiliwa na ukatili wa vita tu ndipo tunaweza kuongoka.

Kujifunza tena kutazamana machoni na kutazama ulimwengu kwa macho safi. Kwa hivyo, shukrani kwa wazazi na walimu kwa "utunzaji" wao na "upendo" wao katika kuwaelimisha "wenzao wadogo njiani," na mwaliko wa kuwasaidia "kutoa uzuri walio nao ndani, na kuuonesha kwa njia mpya kila wakati, zinazohusiana na historia, kumbukumbu, na maisha. Kila mmoja kulingana na upekee wake, ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu."

PAPA LEO XIV KWA AVVENIRE

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.

22 Machi 2026, 10:00