Papa Leo XIV:Mashabulizi ya angani baada ya migogoro ya karne ya 20,yangepigwa marufuku
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 23 Machi 2026 alikutana mjini Vatican na mameneja na wafanyakazi wa Shirika la Kitaifa la Ndege Italia(ITA Airways,) linalowasindikiza Mapapa katika safari zao za kimataifa. Papa XIV atatumia huduma hii pia kwa Ziara yake ya Kitume ya mwezi Aprili kwenda Afrika. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu alibainisha kwamba baada ya matukio ya kusikitisha ya karne ya 20, mashambulizi ya angani yangepaswa kupigwa marufuku milele! Badala yake kama tunavyojua bado yapo, na maendeleo ya kiteknolojia, chanya yenyewe, yanawekwa katika huduma ya vita. Haya sio maendeleo, ni kurudi nyuma!
Papa Leo XIV katika hotuba hiyo alisema kuwa, “inakuwa muhimu zaidi kupanga njia za amani angani.” Hivi ndivyo Papa anavyofanya na kile ambacho Mapapa wote wamefanya kupitia safari za kitume, ambapo “Askofu wa Roma, anaonekana kwa wote kama mjumbe wa amani.” Njia zake ndizo zinapaswa kuwa kila wakati: madaraja ya mazungumzo, kukutana, na udugu. Safari za Papa, kiukweli, ni “mojawapo ya alama zenye ufasaha zaidi za utume wa Warithi wa Petro katika enzi ya kisasa.”
Tamaduni iliyoanzishwa mwaka 1964 na Paulo VI na hija ya kihistoria kwenda Nchi Takatifu, mahali pa kuzaliwa kwa Ukristo, na kuendelea na Mapapa wote waliomfuata; Kwanza kabisa, Papa Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa aliyezunguka dunia akiwa na safari 104 nje ya nchi, kisha Papa Benedikito XVI akiwa na Ziara 24 za kimataifa, na Papa Francisko akiwa na Ziara zake za Kitume 47 katika nchi 66.
Na ziara hiyo haijawahi kusimama katika mabara matano, yaliyounganishwa kwa njia maalum, kwanza na Alitalia na sasa ITA Airways na wafanyakazi wao, iliyojumuisha sio tu wataalamu waliohitimu na wenye uzoefu, lakini pia watu wenye uwezo wa kuunda mazingira tulivu, karibu kama ya kifamilia, ambapo heshima inaunganishwa na kujitolea," anasema Leo XIV. Baba Mtakatifu Leo XIV anatarajiwa kusafiri na Ndege hiyo ya ITA tarehe 13 Aprili 2026, mwanzo wa safari yake ndefu ya kitume kwenda Afrika, (13-23 Aprili), ya pili baada ya Uturuki na Lebanon mnamo Novemba-Desemba 2025 (ikiwa ni pamoja na kituo kifupi cha Ufalme wa Monaco, Jumamosi tarehe 28 Machi 2026 ambayo Papa ataifikia kwa usafiri wa Helikopta.
Algeria, Camerun, Angola, na Guinea ya Ikweta ndizo sehemu ambazo Papa atafika kwa kusafiri na ITA Airways. Baba Mtakatifu aliwaleza kuwa “Kukutana nanyi, kunanipa fursa ya kutoa shukrani na shukrani zangu binafsi, na zile za Vatican, kwa huduma hii ya thamani." Ni Matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba "katika roho ya ushirikiano huu ulioimarishwa na wa kirafiki, makaribisho yaliyotolewa kwake, msafara wake, na waandishi wa habari waliosindikizana naye yataendelea kuonesha umakini na ukarimu huo maalum ambao nyakati tunazoishi zinazidi kuwa muhimu zaidi.” Papa aliwashukuru kwa sababu, katika utume ambao Bwana amemkabidhi, anajua anaweza kuwategemea.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.
