Papa Leo XIV kwa Amazonia:Kulinda umbaji kwa heshima ya maisha katika aina zote!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumanne tarehe 17 Machi 2026 aliwatumia Ujumbe kwa njia ya video washiriki wa Mkutano wa VI wa Baraza la Kikanisa la Amazonia(CEAMA), kuanzia tarehe 16 hadi 20 Machi 2026. Katika ujumbe huo, Papa anaanza na kusema: “Amani ya Bwana iwe nanyi! Ninawasalimu kwa furaha ninyi nyote, wachungaji wapendwa, wanaume na wanawake waliowekwa wakfu, na waamini walei, mliokusanyika Bogotá ili kushiriki katika Mkutano wa Sita wa Kanisa la Amazonia. Mnapitia wakati mzuri wa kumsikiliza Roho Mtakatifu ili kutambua njia za Jumuiya zilizosimika mizizi katika kanda hiyo. Kama sehemu ya maandalizi, ambayo yamesindikizwa na maombi, mmechagua kushirikisha nami baadhi ya hatua mlizochukua, pamoja na changamoto mnazokabiliana nazo.”
Maandalizi ya Mkutano wa 2028
Papa Leo XIV aliongeza kusema: “Mmenishirikisha mateso na matumaini ya wakazi wa eneo hilo, pamoja na kuongezeka kwa kuzorota kwa mazingira yake ya asili. Ninapenda kuelezea ukaribu wangu na wote walioathiriwa na hali hii. Kwa sababu hiyo, ninafurahi kwamba Mkutano huo, miongoni mwa malengo yake ya uundaji wa Upeo wa Kichungaji wa Sinodi, ambao unaweza kuwa chombo muhimu cha kuongoza tangazo la "Mungu anayempenda kila mwanadamu bila kikomo, ambaye ameonesha upendo huu kikamilifu katika Kristo" (Francisko, Waraka wa Kitume wa Baada ya Sinodi, Querida Amazonia, n. 64), “pia ninajua kwamba mtaendelea na uchaguzi wa urais kwa kipindi cha 2026-2030, ambaye kazi yake, miongoni mwa mambo mengine, itakuwa kuendelea kuhimiza utekelezaji wa Sinodi ya Amazonia na, wakati huo huo, kuandaa michango ya uzoefu wake kwa ajili Mkutano wa Kanisa la Ulimwengu mzima huku Roma, uliopangwa kufanyika 2028. Ninawahakikishia kuwasindikiza kwa maombi yangu katika hatua hii muhimu," Papa alibainisha.
"Ninafanya mambo mapya"
Kwa hamu ya kufungua njia mpya katika utume wa Kanisa katika nchi hiyo pendwa, Papa aliongeza kusema kwamba wao wamechagua maandishi ya kibiblia ili kuhamasisha tafakari zao isemayo: "Ninafanya jambo jipya; sasa linachipuka, je, hamlitambui?" (Is 43:19). Papa aliongeza kusema “Ni kweli, kitu kipya kinazaliwa; bado ni dhaifu, lakini tayari kinaendelea. Labda bila kutambulika, ni kama mbegu ya mti wa shihuahuaco, "mti mkubwa wa msituni," ambao hukua polepole sana lakini unakuwa na uwezo wa kuishi kwa zaidi ya miaka elfu moja, mti mkubwa wa mita ya makumi na wenye majani mengi, ambao unakuwa kimbilio salama kwa tai, toucans, macaws, marmosets, sakis, na kindi, na kujibadilisha kuwa na mfumo ikolojia wenyewe. Hii inaweza kutusaidia kuelewa, ndugu wapendwa, kile ambacho Kanisa linatamani: kuwa ishara ya umoja katika utofauti na kimbilio salama linalozalisha na kulinda maisha.”
Wakati ujao unatoa ahadi iliyojaa matumaini
Papa Leo kadhalika alisema kwamba “Mustakabali wenye matumaini uliotangazwa na nabii Isaya unafikia ukamilifu wake katika kifungu cha Kitabu cha Ufunuo kinachotuambia kuhusu mbingu mpya na dunia mpya, kwa sababu Mungu "hufanya vitu vyote kuwa vipya" (taz. Uf 21:5). Kwa hivyo, ninawaalika kufanya kazi kwa uaminifu wa imani iliyojikita katika Kristo ambaye hurudia, "Nimekupenda" (Uf 3:9), kwani ni upendo huu wa kibinadamu wa Yesu unaotubadilisha kuwa wanaume na wanawake wapya. Upendo huu, unaofikiriwa katika sala, unatutuma kujibu kwa ukarimu na ujasiri katika utume wetu. Kwa maana hiyo, tukitaka kuwa wa Kristo, "jitu halisi la msitu" na "mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote" (Kol 1:15), tumeitwa kuwa "Kanisa la Heri, Kanisa linalowapa nafasi watoto wadogo na kutembea katika umaskini pamoja na maskini" (Dilexi te, n. 21). Hakika, muktadha wa sasa unahitaji mwitikio wa kutosha kwa changamoto nyingi za kijamii, kimazingira, kiutamaduni, na kikanisa zinazoendelea katika eneo la Amazonia, zikitishiwa na hali za unyanyasaji na unyonyaji.
Mateso ya Kristo
Katika muktadha huo ua la mateso, ambalo umbo lake la kipekee linadokeza kwa njia ya kuvutia Mateso ya Kristo, na ambalo wamechagua kama ishara ya Mkutano, linawakilisha jukumu la kinabii la Kanisa na la washiriki wake wote, kila mmoja kulingana na dhamira yake mwenyewe: kutangaza kerygma na maisha mapya katika Kristo, kusindikizana na wale wanaoteseka, kulinda uumbaji na kuonesha heshima kwa maisha katika aina zake zote, hasa maisha ya mwanadamu. Lengo lingine la Mkutano wa Kanisa, ambao sasa wanaadhimisha miaka yake mitano, Papa alisema kuwa “ni kuunda Kanisa lenye "uso wa Amazonia," hamu ya Sinodi ya Maaskofu katika Mkutano Maalum wa Kanda ya Amazonia. Kazi hii inafuatiliwa kwa imani kwamba, "kupitia utamadunisho wa imani, Kanisa linatajirishwa na misemo na maadili mapya, likidhihirisha na kusherehekea fumbo la Kristo kwa ufanisi zaidi, likiunganisha imani kwa karibu zaidi na maisha na hivyo kuchangia ukatoliki kamili, si tu kijiografia bali pia kiutamaduni" (Hati ya Aparecida, n. 479).
Utamadunisho ni safari ngumu, lakini ni muhimu
Baba Mtakatifu aidha alisema kuwa “Kaka na dada wapendwa, utamadunisho ni safari ngumu lakini muhimu. "Lazima tukubali kwa ujasiri upya wa Roho, wenye uwezo wa kuunda kitu kipya kila wakati kwa hazina isiyoisha ya Yesu Kristo" (Querida Amazonia, nambari 69).” Kwa njia hiyo aliwatia moyo, wachungaji na waamini, kuendelea pamoja katika kuimarisha utambulisho wa wanafunzi wa kimisionari katika Amazonia, kuendelea kupanda kwenye mtaro ambao pia umemwagiliwa na damu ya wanaume na wanawake wengi waliowatangulia na ambao, wameungana na shauku ya Kristo, wamekuwa mzizi wa "mti mkubwa" unaokua katika Amazonia.” Akiwakabidhi matunda ya Mkutano huo wa Kikanisa kwa maombezi maalum ya Bikira Maria, Mama wa Muumba, Baba Mtakatifu aliwapa kwa uchangamfu Baraka yangu ya Kitume. “Na Baraka ya Mungu Mwenyezi, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, ishuke juu yenu na ibaki nanyi siku zote. Amina," alihitimisha.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.
