Papa Leo XIV:Katika nyakati za uwenda wazimu,ni muhimu kulinda maisha!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, mara baada ya Katekesi yake kwa waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 25 Machi 2026 alitoa salamu mbali mbali ambapo miongoni mwa mawazo yake ni kuhusu ulinzi wa Utakatifu wa Maisha kuanzia kutungwa kwake hadi kifo chake cha kawaida. Alibainisha hayo akiwasalimia Wapoland wote kwamba nchini Poland: “inaadhimisha siku ya Utakatifu wa Maisha." Kiukweli Papa aliongeza "tunahitaji mipango kama vile kuasili Mtoto aliyetungwa Kiroho, ambayo inazinduliwa leo. Katika wakati unaooneshwa na upumbavu wa vita, ni muhimu kulinda uhai kuanzia mimba hadi mwisho wake wa asili." Aliongeza baraka yake: "Nawabariki nyote!”
Salamu kwa waaozungumza Kireno:
Katika kuzungumza lugha ya Kireno Papa alisema: "Karibuni kwa uchangamfu kwa wahujaji wote wanaozungumza Kireno! Kaka na dada wapendwa, Yesu ametukabidhi jukumu la kuomba "kwa Bwana wa mavuno ili atume watenda kazi katika mavuno yake"(Lk, 10:2). Tuchukulie agizo hili kwa uzito na tuombe kila siku kwa ajili ya ongezeko la miito ya ukuhani na maisha ya wakfu. Bikira Maria, Mama wa Mwokozi, awalinde daima!"
Wanaozungumza Kiingereza
Kwa lugha ya Kiingereza Papa alisema: “Ninawakaribisha kwa uchangamfu mahujaji na wageni wote wanaozungumza Kiingereza, hasa wale wanaotoka Uingereza, Ireland, Tanzania, Israeli, Saudi Arabia na Marekani." Papa aliongeza "Ninawasalimu hasa wanafunzi wa Programu ya Roma ya Chuo Kikuu cha Dallas. Tunapoendelea na safari yetu ya Kwaresima, hebu tumwombe Bwana atupe neema ya kumwiga Mama Yetu Mbarikiwa katika "ndiyo" yake kamili kwa Bwana, na hivyo kufungua mioyo yetu kwa mapenzi yake kwa maisha yetu. Kwa nyote na familia zenu, ninawaomba furaha na amani ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu awabariki nyote!"
Wanaozungumza Kiarabu
Kwa lugha ya Kiarabu: Nawasalimu waamini wanaozungumza Kiarabu, hasa wale kutoka Nchi Takatifu. Wakristo wameitwa kuwa wanafunzi wenye upendo na wajumbe jasiri wa kutangaza Injili ulimwenguni kote. Bwana awabariki nyote na awalinde daima kutokana na maovu yote!"
Wanaozungumza Kifaransa
Kwa wanaozungumza Kifaransa: “Ninatoa salamu zangu za dhati kwa watu wanaozungumza Kifaransa, hasa mahujaji kutoka shule za Kifaransa. “Kaka na dada, tuwaombee Wachungaji wa Kanisa, kwamba, wakifanya kazi pamoja na kwa pamoja, waweze kutangaza Habari Njema kwa bidii na kuwasaidia waamini kushiriki kikamilifu katika kujenga Kanisa na ulimwengu wa amani.” Mungu awabariki!"
Hatimaye kwa lugha ya kiitaliano:
Papa hatimaye aliwasalimia na kuwakaribisha wanahija wa lugha ya kiitaliano kwa namna ya pekee waamini kutoka Jimbo Kuu la Carpi wakisindikizwa na Askofu Mkuu Erio Castellucci; Parokia ya Mtakatifu Maria wa Agnena huko Vitulazio, wakisindikizwa na Askofu Mkuu Pietro Lagnese; na ile ya Mchungaji Mwema huko Viestena wakisindikizwa na Askofu Franco Moscone. Amewasalimia Taasisi za Shule ya Mottola, Sora na na Mtakatifu Giovanni Gemini.
Wazo la Baba Mtakatifu pia limekwenda kwa vijana, wagonjwa, wenye ndoa wapya. Papa aliongeza: “Katika Sherehe ya Kupashwa, tunayoadhimisha leo, iwe mwaliko kwa wote kufuata mfano wa Maria Mtakatifu sana na kuwa tayari kufanya mapenzi ya Mungu kila wakati.” Na wote aliwatakia baraka.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.
