Papa Leo XIV:“Kanisa ni moja lakini linajumuisha kila mtu”
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kiukweli, ni Kristo ambaye, katika zawadi ya Mwili na Damu yake, huwakusanya watu hawa pamoja ndani yake kwa njia dhahiri. Kuna na lazima kuwe na nafasi kwa kila mtu Kanisani, na kwamba kila Mkristo ameitwa kutangaza Injili na kutoa ushuhuda katika kila mazingira anayoishi na kufanya kazi. Haya yamo katika Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 11 Machi 2026 kwa waamini na mahujaji wengi wapatoa 16,000 waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Katika mwendelezo wa Katiksi zake kuhusu Hati za Mtaguso wa Pili wa Vatican kwa kudadavua Katiba ya Kidogma, Papa Leo XIV amejikita na mada ya “Kanisa Watu wa Mungu.”
“Mungu anafanya Agano, anawasindikia,anawatunza na kuwakusanya”
Awali ya yote lilisomwa somo kwa lugha mbali mbali kutoka Kitabu cha Nabii Yeremiha: “Hili ndilo Agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu,” (Yer 31,33). Kwa hiyo, Baba Mtakatifu Leo XIV alianza Katekesi yake kwa salamu na kuongeza: “ Tukiendelea na tafakari yetu kuhusu Katiba ya Kidogma, Lumen Gentium (LG), leo tujikite na sura ya pili, iliyojikita kwa “Watu wa Mungu” Mungu, aliyeumba ulimwengu na ubinadamu na anayetamani kumwokoa kila mwanadamu, anatimiza kazi yake ya wokovu katika historia kwa kuchagua watu maalum na kukaa kati yao. Kwa sababu hiyo, anamwita Ibrahimu na kumwahidi kuzidisha uzao wake kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko baharini;(Mw 22,17-18). Pamoja na watoto wa Ibrahimu, baada ya kuwaweka huru kutoka utumwani, Mungu anafanya agano, anawasindikiza, anawatunza, na kuwakusanya pamoja kila wanapopotea. Kwa njia hiyo, utambulisho wa watu hawa unatolewa na kitendo cha Mungu na kwa imani kwake. Wanaitwa kuwa nuru kwa mataifa mengine, kama taa itakayowavuta watu wote, wanadamu wote, kwake (rej. Is 2:1-5).
“Watu wanaopata mwili wa Kristo ni watu wa Mungu”
Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea kusema, “Mtaguso unasema "yote haya yalifanyika katika maandalizi na mfano wa agano jipya na kamilifu ambalo lingeanzishwa katika Kristo, na ufunuo huo kamili zaidi ambao ungewasilishwa kwa Neno la Mungu mwenyewe aliyefanyika mwanadamu" (LG, 9). Kiukweli, ni Kristo ambaye, katika zawadi ya Mwili na Damu yake, huwakusanya watu hawa pamoja ndani yake kwa njia dhahiri. Hawa wameundwa na watu kutoka kila taifa; wameunganishwa kwa imani katika Yeye, kwa kushikamana Naye, kwa kuishi maisha Yake, iliyoongozwa na Roho wa Mfufuka. Hili ni Kanisa: watu wa Mungu wanaopata uwepo wao kutoka katika mwili wa Kristo na ambao wenyewe ni mwili wa Kristo; si watu kama wengine, bali watu wa Mungu, waliokusanywa Naye na kuumbwa na wanawake na wanaume kutoka kwa watu wote wa dunia.
“Ni Watu wa kimasiha kwa sababu Kichwa chake ni Kristo,Masiha”
Kanuni yake ya kuunganisha si lugha, utamaduni, au kundi la kikabila, bali ni imani katika Kristo: kwa hivyo Kanisa, kulingana na usemi mzuri wa Mtaguso, ni kusanyiko la wale wanaomtazama Yesu kwa imani” (LG, 9). Ni watu wa kimasiha, hasa kwa sababu kichwa chake ni Kristo, Masiha. Wale walio wake hawajivunii sifa au vyeo, bali ni zawadi tu ya kuwa, katika Kristo na kupitia Yeye, mabinti na wana wa Mungu. Kwa hivyo, kabla ya kazi au kazi yoyote, kile kilicho muhimu kweli katika Kanisa ni kupandikizwa juu ya Kristo,kwa neema kuwa watoto wa Mungu. Hili pia ndilo jina pekee la heshima tunalopaswa kutafuta kama Wakristo. Papa Leo XIV alisisitiza tena kwamba: “Tuko ndani ya Kanisa ili kupokea uzima kutoka kwa Baba bila kukoma na kuishi kama watoto na ndugu zake miongoni mwa kila mmoja.
“Sheria inahuisha mahusiano katika Kanisa ni upendo”
Kwa hivyo, sheria inayohuisha mahusiano katika Kanisa ni upendo, tunapoupokea na kuupitia katika Yesu; na lengo lake ni Ufalme wa Mungu, ambao unasafiri pamoja na wanadamu wote. Likiwa limeunganishwa katika Kristo, Bwana na Mwokozi wa kila mwanaume na mwanamke, Kanisa haliwezi kamwe kujitenga, bali liko wazi kwa wote na kwa kila mmoja. Ikiwa waamini katika Kristo ni wake, Mtaguso unatukumbusha kwamba "watu wote wameitwa kuunda Watu wapya wa Mungu. Kwa njia hiyo, watu hawa, wakibaki kuwa wamoja na wa kipekee, lazima waeneze ulimwenguni kote na kwa vizazi vyote, ili kusudi ya mapenzi ya Mungu yaweze kutimizwa. Aliumba asili ya mwanadamu hapo mwanzo na anatamani kuwakusanya pamoja watoto wake waliotawanyika" (LG, 13).
“Mkristo ameitwa kutangaza Injili na kutoa ushuhudua mahali popote”
Baba Mtakatifu leo XIV, kwa njia hiyo aliongeza “hata wale ambao bado hawajapokea Injili, kwa namna fulani, wameelekezwa kwa watu wa Mungu, na Kanisa, likishirikiana katika utume wa Kristo, limeitwa kueneza Injili kila mahali na kwa kila mtu ( LG, 17), ili kila mtu aweze kuwasiliana na Kristo. Hii ina maana kwamba kuna, na lazima kuwe na nafasi kwa kila mtu Kanisani, na kwamba kila Mkristo ameitwa kutangaza Injili na kutoa ushuhuda katika kila mazingira anayoishi na kufanya kazi. Hivi ndivyo watu hawa wanavyoonesha ukatoliki wao, wakikumbatia utajiri na rasilimali za tamaduni mbalimbali na, wakati huo huo, wakiwapa upekee wa Injili ili kuwatakasa na kuwainua (Rej. LG, 13).”
“Kanisa ni moja lakini linajumuisha kila mtu”
Kwa maana hiyo, Papa Leo XIV alisisitiza tena: “Kanisa ni moja lakini linajumuisha kila mtu. Mtaalimungu mkuu alilielezea kwamba: "Sanduku moja la Wokovu, lazima likubali katika eneo lake kubwa utofauti wote wa wanadamu. Ukumbi mmoja wa Karamu, chakula kinachosambazwa kinatokana na viumbe vyote. Vazi la Kristo lisilo na mshono, na ni kitu kile kile na vazi la Yosefu, la rangi nyingi."Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV alibanisha, “Ni ishara kubwa ya matumaini—hasa katika siku zetu, inayooneshwa na migogoro na vita vingi, kujua kwamba Kanisa ni watu ambao wanaundwa wanawake na wanaume wa mataifa, lugha, na tamaduni tofauti wakiishi pamoja, kwa imani. Ni ishara iliyowekwa katika moyo wa ubinadamu, ukumbusho na unabii wa umoja na amani ambayo Mungu Baba anawaita watoto wake wote,” Papa Leo alihitimisha.
