Papa Leo XIV: Wakristo katika Ulimwengu mamboleo wanaitwa na kutumwa kuwa ni washiriki wa ujenzi wa amani na Kristo Yesu, anayetamani hata katika ulimwengu huu kushirikisha zawadi ya ubinadamu. Papa Leo XIV: Wakristo katika Ulimwengu mamboleo wanaitwa na kutumwa kuwa ni washiriki wa ujenzi wa amani na Kristo Yesu, anayetamani hata katika ulimwengu huu kushirikisha zawadi ya ubinadamu.   (ANSA)

Papa Leo XIV Kanisa Katika Huduma Ya Haki, Amani na Upatanisho!

Washiriki wamepembua na kuchambua mada kuu tano ambazo ni: Amani na Kanisa; Amani, Sheria, na Uhamiaji; Amani na Uchumi; Utamaduni na Sanaa Zinazohamasisha Amani; na Amani, Ukweli, na Haki katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde. Mkutano huo ulitamatishwa na Emilce Cuda, Katibu wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini. Upatanisho ni jambo linalotangulia siasa, na kwa sababu hii wenyewe ni muhimu sana kwa kazi ya siasa yenyewe. Upatanisho ni muhimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Upatanisho Kimataifa, uliofanyika hivi karibuni uliwakusanya pamoja wanafunzi, maprofesa, na wataalamu kutoka nchi mbalimbali za Bara la Amerika, ili kufanya tafakari ya kina na hatimaye kutoa mapendekezo ya njia madhubuti za kujenga amani katika Bara la Amerika.  Tukio hili liliandaliwa na Chuo Kikuu cha Loyola cha Chicago pamoja na Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini (PCAL) kama sehemu ya Mpango mkakati wa “kujenga madaraja,” "Building Bridges Initiative" uliozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2022. Mkutano huu umeratibiwa na Kardinali, Blase Cupich Askofu Mkuu wa Chicago. Askofu mkuu Filippo Iannone, O.Carm., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini; Kardinali José Tolentino de Mendonça, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu; Sr. Nathalie Becquart, Naibu Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Sinodi; na Askofu Mkuu Lizardo Estrada, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM. Washiriki wamepembua na kuchambua mada kuu tano ambazo ni: Amani na Kanisa; Amani, Sheria, na Uhamiaji; Amani na Uchumi; Utamaduni na Sanaa Zinazohamasisha Amani; na Amani, Ukweli, na Haki katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde. Mkutano huo ulitamatishwa na Emilce Cuda, Katibu wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini.

Amani ya kweli ni safari ya upatanisho na Mungu, kati ya watu na kazi ya uumbaji
Amani ya kweli ni safari ya upatanisho na Mungu, kati ya watu na kazi ya uumbaji

Upatanisho ni jambo linalotangulia siasa, na kwa sababu hii wenyewe ni muhimu sana kwa kazi ya siasa yenyewe. Bila nguvu ya upatanisho kuumbwa ndani ya mioyo ya watu, majukumu ya kisiasa kwa ajili ya amani yanakosa msingi wake wa ndani na kwamba, utakaso wa ndani wa mtu ni sharti la msingi linalodaiwa kabla ya kujenga haki na amani kwa uwepo wa Mungu. Kwa kweli, ni neema ya Mungu inayowapatia waamini moyo mpya na kuwapatanisha naye na wao kwa wao. Ni Kristo aliyeurudisha ubinadamu katika upendo wa Baba. Upatanisho chanzo chake ni katika upendo huo; unaotokana na uamuzi wa Baba wa kufanya upya uhusiano wake na wanadamu, uhusiano uliovunjwa na dhambi ya mwanadamu.Katika Kristo Yesu, “katika maisha yake na katika huduma yake, lakini hasa katika kifo na ufufuko wake, Mtume Paulo alimwona Mungu Baba akiupatanisha ulimwengu (vitu vyote mbinguni na duniani) naye, bila kuhesabia dhambi ya binadamu (rej. 2Kor 5:19; Rum 5:10; Kol 1:21-22). Kwa hakika, ni upatanisho halisi tu unaoweza kuleta amani ya kudumu katika jamii. Hili ni jukumu la lazima la viongozi wa serikali na watemi wa kijadi, lakini inawahusu pia raia wa kawaida. Baada ya kutokea migogoro, upatanisho ambao mara nyingi hupatikana kimyakimya na bila majigambo, hurudisha umoja wa mioyo na kuishi pamoja kwa utulivu. Kutokana na upatanisho, baada ya vita vya muda mrefu Mataifa yanaweza kurudisha amani, na jamii iliyojeruhiwa vikali na vita vya wenyewe kwa wenyewe au na mauaji ya kimbari inaweza kujenga tena umoja wao.

Kardinali Blaise Joseph Cupich wa Jimbo kuu la Chicago
Kardinali Blaise Joseph Cupich wa Jimbo kuu la Chicago   (Copyright: Ukrainian Greek Catholic Church - UGCC)

Kwa njia ya kutoa na kupokea msamaha kumbukumbu zilizojeruhiwa za watu binafsi na za jumuiya zimepata kupona, na familia ambazo zilikuwa zimegawanyika zimeungana tena kwa utulivu. “Upatanisho hushinda matatizo, hurudisha heshima ya watu binafsi na hufungua njia ya maendeleo na amani ya kudumu kati ya watu katika kila ngazi. Ili uwe na ufanisi, upatanisho huu lazima uendane na tendo la kijasiri na la kikweli, lisilo na unafiki ndani yake: ufuatiliaji wa waliohusika na migogoro hii, wa wale ambao waliuwezesha kifedha ukatili huo, pamoja na waliohusika kwa namna yoyote na mipango hiyo, na kuhakikisha jinsi walivyohusika. Wahanga wana haki ya kujua ukweli na kupata haki. Ni muhimu kwa sasa na kwa wakati ujao kusafisha kumbukumbu, ili kuijenga jamii bora zaidi pale ambapo matukio hayo ya kutisha hayarudiwi tena. Rej. Africae munus, 19-22.

Upatanisho baada ya vita unaweza kurejesha tena amani
Upatanisho baada ya vita unaweza kurejesha tena amani   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huu anakazia umuhimu wa sala inayoweza kuleta ukombozi dhidi ya vita na kwamba, hili ni jambo linalowezekana, ikiwa kama utashi wa kisiasa. Katika Ulimwengu uliojeruhiwa kwa vita, kinzani na migawanyiko, juhudi za ujenzi wa haki, amani na upatanisho ni mambo msingi sana. Itakumbukwa kwamba, amani ya kweli ni zawadi kutoka kwa Mungu, hii ni amani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu. “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi.” Yn 14: 27-28. Wakristo katika Ulimwengu mamboleo wanaitwa na kutumwa kuwa ni washiriki wa ujenzi wa amani na Kristo Yesu, anayetamani hata katika ulimwengu huu kushirikisha zawadi ya ubinadamu. Kristo Yesu anatembea pamoja na waja wake, ili kuwawezesha kujenga amani na utulivu. Kumbe, katika ngazi ya Ulimwengu, kuna haja ya kujenga na kudumisha amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, amani inayovuka mipaka ya imani na tamaduni na hivyo kuwahusisha watu mbalimbali na kwamba, mbinu na mkakati wa mkutano huu ni mfano bora wa kuigwa na kwamba, ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, utaweza kuzaa matunda kwa wakati wake.

Upatanisho unasimikwa katika Injili ya Upendo
Upatanisho unasimikwa katika Injili ya Upendo   (AFP or licensors)

Amani na utulivu havina budi kukita mizizi yake katika Upatanisho na Mwenyezi Mungu; amani ambayo imeletwa na Kristo Yesu kwa njia ya: mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele.Amani ni safari ya upatanisho endelevu na Mwenyezi Mungu, kati ya watu wenyewe, na wengine pamoja na kazi ya uumbaji, kwa kuendeleza utamaduni wa upatanisho, ili kushinda kishawishi cha utandawazi usiguswa na mahangaiko ya wengine. Waamini wanakumbushwa kwamba, sala ni nguzo muhimu sana ya upatanisho. Pale watu wa Mungu wanapounganika kwa njia ya Sala, hapo nguvu ya sala inaweza kuwa ni chachu ya mabadiliko ya historia. Baba Mtakatifu amewatia shime wote walioshiriki katika tukio hili na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.

Papa Leo XIV Upatanisho
11 Machi 2026, 15:12