Papa Leo XIV Kampeni ya Kwaresima Nchini Brazi 2026: Udugu na Makazi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB., Jumatano ya Majivu, tarehe 18 Februari 2026 limezindua Kampeni ya 63 ya Udugu wakati wa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2026. Tema ya mwaka huu ni: “Fraternidade e Moradia” Yaani: “Udugu na Makazi: Alikuja akaa kwetu.” (Rej. Yn 1:14). Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwenye Kampeni hii, analialika Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil kufungua macho yake hasa kwa watu wasiokuwa na makazi ya kuishi. Kuna uhusiano kati ya karama ya Neno la Mungu, Nafasi ya Ukarimu na mabadiliko ambayo Neno hili linaleta. Kwa sababu hiyo, safari ya Kwaresima inakuwa ni fursa muafaka ya kusikiliza sauti ya Mungu na hivyo kupyaisha tena maamuzi ya kumfuasa Kristo Yesu, kwa kutembea katika njia ile iendayo Yerusalemu ambako Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko vinapata utimilifu wake.
Kipindi cha Kwaresima kimsingi kinasimikwa katika nguzo kuu nne: Sala na Kufunga; Tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hiki ni kipipndi cha kuutisha mwili kwa sala, kufunga, toba na wongofu wa ndani, tayari kuyaelekeza maisha kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya kusali na kufunga kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu aliyefunga na kusali jangwani kwa muda wa Siku Arobaini. Huu ni mwaliko wa kumwilisha Sala na Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama Yeye mwenyewe anavyojitambulisha akisema, kadiri walivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zake walio wadogo walimtendea Yeye. Rej. Mt 25: 35-40. Roho Mtakatifu, chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini awaongoze katika safari hii.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB linaadhimisha Kampeni ya 63 ya Udugu wakati wa Kipindi cha Kwaresima, Jumuiya ya waamini nchini Brazil inaelekeza sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji na matendo ya huruma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani kuna uhusiano wa pekee kati ya imani na maskini, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, wanapambana kufa na kupona na miundombinu yote inayozalisha umaskini kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Akakaa kwetu.” Yn 1:14. Huu ni mwaliko kwa Kanisa nchini Brazil kufungua macho yake ili kuwatambua watu wanaoteseka kwa kukosa makazi bora ya kuishi na wengine kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II, hawana makazi kabisa. Hiki ni kipindi muafaka cha kuamsha dhamiri nyofu ili kupata suluhu itakayowawezesha watu wa Mungu nchini Brazil kupata suluhu ya tatizo na changamoto hii, yenye athari kubwa kwa mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake na kwamba, kimsingi hili ni tatizo kubwa lenye athari zake katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kitamaduni na kiutu.
Hii ni Kampeni anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV inayopaswa kudumu kwa mwaka mzima, inayowasukuma waamini kumwendea Kristo Yesu kwa njia ya watu wasiokuwa na makazi nchini Brazil. Kampeni hii ya Udugu wakati wa Kipindi cha Kwaresima, ilete changamoto kwa viongozi wa Serikali ili waweze kusaidia kuibua na kuendesha sera na mikakati itakayo waasukuma kufanya kazi kwa njia ya umoja na ushirikiano, ili kuleta mabadiliko katika makazi ya watu wa Mungu nchini Brazil. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, anayaweka matamanio haya yote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia na Mama wa Aparecida, Msimamizi na Mwombezi wa Brazil, ambaye hakupata nafasi kwenye nyumba ya wageni kule Bethlehemu wakati alipokuwa anakaribia kumzaa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, ili awaombee neema na baraka wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza nia hii njema, ili watu wote wa Mungu nchini Brazil waweze kupata makazi bora ya kuishi.
