Papa akutana na Washiriki wa Mkutano IV wa Ukuu wa Ukarimu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana tarehe 12 Machi 2026 na Washiriki wa Mkutano wa IV kuhusu Ukuu wa Makaribisho. Alifurahi kushirikishana nao tafakari juu ya mada ambayo walijikita nayo ya "Ukuu wa Ukarimu" iliyozaliwa na uzoefu wa kiroho wa Chama cha Nyumba ya Udugu kwa usaidizi hai wa mashirika mengine ya kikanisa na kijamii. Siku zao zimechochewa na ufahamu kwamba wito wa Kikristo unalenga kuzalisha ushirika miongoni mwa watu, na ushirika unatokana na uwezo wa kuwakaribisha wengine, kutoa sikio la kusikiliza, ukarimu, na usaidizi. Papa alisema kuwa asili inayowezekana ya neno "karibu" - kitovu cha shughuli zao zote - hufuatilia kutoka kwa Kilatini accipere, ikimaanisha "kupokea," "kuchukua mwenyewe." Siku zao kwa njia hiyo zimeuhishwa na utambuzi ambao wito wa kikristo umeelekezwa na kutoa muungano kati ya watu, na muungano unaozaliwa na uwezo wa kupokea watu wengine kwa kutoa usikivu.
Uhusiano unaotokana na neema ya kukutana
Katika moyo wa kila ukaribisho wa kweli, kiukweli, kuna uhusiano unaotokana na neema ya kukutana. Tunapitia aina nyingi za kukutana na, kwa hivyo, kukaribisha: Kukutana na watu wanaotupenda, na familia, na wafanyakazi wenza, na hata na wageni, wakati mwingine wenye uadui. Wakati kukutana ni kweli, kunaweza kubadilika kutokana na uzoefu wa kibinafsi na, polepole, kuwa na uwezo wa kuwashirikisha wengine, na kusababisha uzoefu wa kijamii. Ni ndani ya mabadiliko haya ya kukutana ambapo uamuzi wao wa kujitolea toleo la nne la "Ukuu kwa vijana umejikita,” Papa amesisitiza. Katika wakati unaooneshwa na mabadiliko makubwa ya kiutamaduni na kijamii, vijana, ambao kwa kawaida ni mustakabali wa jamii na Kanisa, kiukweli tayari wanaunda uhai sasa na wenye kuzaa matunda. Maswali na wasiwasi wao, kiukweli, yanatualika kusasisha mtindo wa mahusiano yetu.
Kuwakaribisha vijana
Papa Leo XIV alisisitiza kwamba kuwakaribisha vijana kunamaanisha, kwanza kabisa, kusikiliza sauti zao, kukutana na macho yao, na kutambua kwamba, katika maisha yao na lugha zao, Roho anaendelea kufanya kazi na kupendekeza njia mpya za uwepo na utunzaji.” Baba Mtakatifu baada ya kuzungumza hayo alipenda kujikita hasa na mambo mawili “uwepo na ulinzi, mambo yanayohusiana na kuakisi maana ya ukristo ya ukarimu. Kila mmoja wetu, kuanzia wakati wa kwanza wa maisha, hukua ndani ya muktadha wa kijamii. Familia, parokia, shule, chuo kikuu, na mahali pa kazi vinawakilisha mifano ya jamii ambapo vipimo tofauti vinaingiliana: kisaikolojia, kisheria, kimaadili, kielimu, na kitamaduni. Ni nafasi za ujenzi wa utambulisho ambazo kazi yake kuu hufafanuliwa haswa na uwepo. Kuwepo katika maisha ya wengine kunamaanisha kushiriki wakati, uzoefu, na maana, kutoa uthabiti wa marejeo ambayo wengine wanaweza kujitambua na kukua.
Kutazama familia Takatifu ya Nazareth
Kutazama Familia Takatifu ya Nazareti, mfano ambao Fraterna Domus hupata msukumo, kila jumuiya inayokaribisha inaweza kugundua upya wito wake na kujifunza kujielekeza kwenye njia ya huduma. Papa Leo XIV, alisema kuwa Injili ya Maria na Yosefu waliompoteza Yesu na, wakiwa na uchungu, wakampata baada ya siku tatu Hekaluni ( Lk 2:39-52), inatufundisha kwamba uwepo wa wengine si wa moja kwa moja, bali ni matokeo ya utafutaji wa mara kwa mara. Kila mmoja wetu amepoteza mtu au kitu ambacho alikuwa amekipenda sana. Wakati huo, tulitambua jinsi uwepo huo ulivyokuwa wa thamani.
Hili pia hutokea katika maisha ya imani: tunachukulia uwepo wa Yesu maishani mwetu kirahisi, hadi ghafla inaonekana Yeye hayupo tena pale tulipomwacha. Tunahisi hisia ya kupotea. Kiukweli, si Yeye aliyepotea, bali sisi ambao tumejitenga. Hili linapotokea, tunaitwa kumtafuta kwa uaminifu, kwa ujasiri wa kusafiri njia ambazo hazijachunguzwa, tukiutazama ulimwengu kwa macho mapya, tukiwa na matumaini. Kwa njia hii, tutaacha kumtafuta Mungu aliyeumbwa kwa ajili yetu na badala yake tutakutana naye pale anapoishi. Kwa hivyo, kumtafuta Yesu kunamaanisha kuhama kutoka kwa usalama wa imani zetu hadi jukumu la kukutana Naye, kujifunza kuona na kukaribisha uwepo wa Mungu ambaye daima yuko "mbele."
Mtakatifu Yosefu mlinzi wa familia aliyokabidhiwa na Bwana
Papa Leo alisisitiza kwamba hili ndilo hasa alilofanya Mtakatifu Yosefu, akiilinda familia aliyokabidhiwa na Bwana. Ndani yake, tunatambua kwamba kuwakaribisha, pamoja na kuwapo, pia ni kulinda. Kulinda kunamaanisha kuwa karibu na wengine kwa makini, kuheshimu chaguo zao, na kuwajali. Mtazamo huu ni wa kwanza kabisa kwa Mungu, ambaye Biblia inamwonyesha kama mlinzi wa watu wake. Tukumbuke zaburi inayosema: "Hatasinzia wala kulala/ mlinzi wa Israeli/ Bwana ndiye mlinzi wako" (Zab 121:4-5). Kwa mtazamo huu, tunaelewa kwamba familia ya wanadamu pia inaitwa kuhifadhi kile kilichokabidhiwa kwake: mahusiano, uumbaji, maisha ya dada na kaka zetu, hasa wale wanaoteseka na walio katika mazingira magumu zaidi. Kwa hivyo, Yosefu anatuonyesha kwamba uwepo na ulinzi ni vipimo visivyoweza kutenganishwa: mtu hawezi kulinda bila kuwepo, na mtu hawezi kuwepo bila kuchukua jukumu kwa wengine.
Maneno haya yanawakilisha taa mbili za mchakato wa ukarimu
Maneno haya mawili Papa Leo alikazia kusema, yanaweza kuwa taa mbili katika safari yao kuelekea roho ya ukaribishaji inayoweza kufungua njia za utakatifu, katika mtazamo ambao kamwe si wa kujirejea, wa uhusiano na udugu kila wakati, kama vile Waraka wa Kitume wa Fratelli Tutti yaani Ndugu Wote, inavyotukumbusha, kwamba: "Ni utamaduni wa kijamii na kisiasa tu unaokumbatia ukaribishaji wa bure unaoweza kuwa na mustakabali" (Ft 141) kwa vizazi vipya. Kwa kuhitimisha Papa aliwashukuru kwa kujitolea kwwao kimya na kwa busara. Aliwahimiza kuwa waelimishaji wa ukaribishaji. Kukuza karama ya ukaribishaji kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu, ambaye tunda lake, Mtakatifu Paulo anatuambia kwamba: "ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, ukarimu, uaminifu, upole, na kujidhibiti" (Gal 5:22). Kwa njia hii, wataendelea kuunda mazingira yanayoweza kukuza wema na udugu katika jumuiya ya Kikristo na katika jamii. Maria Mtakatifu Zaidi na Mtakatifu Yosefu awalinde na kuwaombea. Aliwabariki kwa moyo wote.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.
