Nia za Baba Mtakatifu Leo XIV Kwa Mwezi Machi 2026: Kupokonya Silaha, Kudumisha Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Amani kama tunda la haki, linamtazama mwanadamu katika ujumla wake, kiroho, kimwili, kisiasa, kiuchumi na hata kiutamaduni. Na kwamba, mwanadamu anapaswa kupata haki yake ya msingi katika hayo, ile haki ya kuzaliwa nayo, kinyume cha hapo tayari mwanadamu anakosa haki yake ya msingi, na ndio chanzo cha vurugu na kukosekana kwa amani katika jamii. Ni wazi kwamba, binadamu anapokosa haki yake, na utu wake unaposhindwa kuheshimiwa hupandwa na jazba na kuchanganyikiwa na hata kuwa chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani. Kunakuwa na tishio la amani mtu anapopewa baadhi tu ya yale anayopaswa kuyapata kama binadamu, pale hadhi yake inaposhindwa kuheshimiwa na kuthaminiwa; na pale maisha yake ya kiraia yasipoelekezwa kwenye: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, siasa inawajibu na inapaswa kuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa haki na amani jamii. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: “Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na Inayopokonya Silaha.” Takwimu zinaonesha kwamba, gharama za manunuzi ya silaha yameongezeka kwa asilimia 9.4%, ikilinganishwa na kipindi cha Mwaka 2024. Kiwango hiki ni sawa na Dola za Kimarekani bilioni 2, 718 sawa na Aslimia 2.5% ya Pato Ghafi la Ulimwengu. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kuelekea kwenye amani isiyo na silaha, na inayopokonya silaha. Hii ni amani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu Mfufuka, changamoto kwa wafuasi wa Kristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano. Amani ni mchakato, ni safari na mwanga wa mapito katika maisha. Amani ni zawadi kutoka kwa Kristo Yesu: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.” Yn 14:27. Hata katika hali ya kutisha, Kristo Yesu alimwambia Mtume Petro: “Rudisha upanga alani mwake.” Yn 18:11.
Amani ni ukweli unaopaswa kumwilishwa katika maisha. Mabilioni ya Dola za Kimarekani yanayotumika kununulia silaha yangeweza kusaidia kuboresha maisha ya watu wengi duniani, kumbe kuna haja ya kuzuia ukatili wa vita kwa sababu maendeleo ya silaha za kisayansi yameongeza sana ubaya na ukatili wa vita. Rej. Gauium et spes, 80. Baba Mtakatifu Leo XIV anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza katika amani inayopokonya Silaha; amani inayosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili: Kuthamininiana pamoja na kuheshimiana. Huu ni mwaliko wa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi na kwamba, amani si swala la kufikirika tu, bali ni jambo linalo simikwa katika: maelewano na utekelezaji wa majukumu yanayofikiwa. Ni amani inayosimikwa katika diplomasia, majadiliano, kanuni na sheria za Kimataifa kwa kuimarisha taasisi za Kimataifa katika utekelezaji wa majukumu yake. Haki, Amani, Utu na heshima ya binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee, ili kurejesha tena Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; binadamu wajifunze kusaidiana! Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake kwa Mwezi Machi 2026 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Mawasiliano Jamii, anaawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujiunga pamoja naye kusali kwa ajili ya kupokonya silaha, ili kudumisha amani, kwani binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wameumbwa ili kujenga na kudumisha umoja na ushirika na wala si vita; wameumbwa ili kujenga udugu wa kibinadamu na wala si uharibifu. Kristo Mfufuka aliwaachia wafuasi wake zawadi ya amani: “Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi.” Yn 20:21.
Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote mapenzi mema kuhakikisha kwamba, amani inasimikwa katika ukweli wa kihistoria, kwa Mataifa kuachana na utamaduni wa kifo na hivyo kujikita katika mchakato wa majadiliano na diplomasia ya Kimataifa. Hii ni changamoto kwa waamini kuondokana na chuki, uhasama na hali ya kutojali, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upatanisho, kwani usalama wa kweli si matunda ya hofu bali ni chimbuko la: kuaminiana, haki na mshikamano kati ya Mataifa. Mwenyezi Mungu apende kuwaangazia viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, wawe na ujasiri wa kuachana na miradi inayopandikiza utamaduni wa kifo pamoja na mashindano ya kutengeneza silaha za maangamizi. Rasilimali fedha inayotumika kwa ajili ya kutengeneza, kuboresha na kuhifadhi na hatimaye, kuuza silaha za maangamizi, nyuma yake kuna kilio cha watoto na familia nyingi duniani. Watu wanatamani amani ya kudumu ili kuondokana na vitisho vya silaha za maangamizi na kwamba, hii ni changamoto inayowahusisha watu wote; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuaminiana na wala si katika tabia ya kupimana nguvu. Kuna haja ya kudhibiti biashara ya silaha kimataifa na maendeleo makubwa ya teknolojia kuhusu masuala ya kijeshi. Hii ni dharura inayohitaji kushughulikiwa na viongozi wote wa Jumuiya ya Kimataifa.
Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuhimiza umuhimu wa watu wa Mataifa kudumisha amani. Kanisa linaunga mkono Kanuni ya Sheria ya Kimataifa kuhusu Silaha za Nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu!Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Machi 2026 anakaza kusema, binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, tishio la silaha za nyuklia lisiwe tena kipimo cha mustakabali wa mwanadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anamwomba Roho Mtakatifu awafanye waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa wajenzi waaminifu na wabunifu wa amani kila siku, katika mioyo yao, ndani ya familia, jamii na miji yao. Anasali ili kila neno jema, kila ishara ya upatanisho na kila chaguo la majadiliano liwe ni mbegu za ujenzi wa Ulimwengu mpya.
