Hija ya Papa Leo XIV barani Afrika:Programu ya Ziara ya Kitume imechapishwa
Salvatore Cernuzio na Angella Rwezaula - Vatican.
Siku kumi, nchi nne, miji kumi na mmoja, takriban hotuba 25, salamu, na mahubiri, safari za ndege za ndani za kila siku, na wakati mwingine hata mbili kwa siku moja. Ziara ya Kitume ambayo Papa Leo XIV anajiandaa kufanya barani Afrika kuanzia tarehe 13 hadi 23 Aprili 2026, inaahidi kuwa tajiri, yenye nguvu, na ya kuvutia sana. Algeria, Camerun, Angola, na Guinea ya Ikweta ndivyo vituo vya safari hii, ambavyo Papa Leo mwenyewe alikuwa amevitabiri kwa kiasi fulani katika safari ya kurudi kutoka Beirut aliposema alitaka kutembelea bara la Afrika hivi karibuni, akianza na Algeria, nchi ya Mtakatifu Agostino, Baba yake wa Shirika.
Nchini Algeria, katika nyayo za Mtakatifu Agostino
Na kutoka mji mkuu, Algiers, hija ndefu ya kimataifa ya Papa itaanza ambayo itakuwa hija yake ya tatu baada ya Uturuki na Lebanon (Novemba 27–Desemba 2,2025) na Ufalme wa Monaco (Machi 28). Programu rasmi ya hija ilichapishwa Jumatatu tarehe 16 Machi 2026. Papa ataondoka kutoka Uwanja wa Ndege wa Rome-Fiumicino saa 2:00 asubuhi kuelekea jiji la Afrika Kaskazini. Amepangwa kutua saa moja baadaye katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Houari Boumédiène wa Algiers, ambapo sherehe ya kuwakaribisha itafanyika.
Saa 3:45 asubuhi, Papa Leo XIV atatembelea Mnara wa Mashahidi wa Maqam Echahid, ukumbusho uliozinduliwa mwaka 1982 katika maadhimisho ya miaka 20 ya uhuru wa Algeria kutoka Ufaransa na kuheshimu waliokuwa kwa vita vya ukombozi. Papa Leo XIV atatoa heshima zake hapo. Mikutano yote ya kitaasisi itafuata, ikifuatiwa na ziara ya faragha kwa Rais wa Jamhuri, Abdelmadjid Tebboune, katika Ikulu ya Rais, na mkutano katika Kituo cha Mikutano cha "Djamaa el Djazair" na mamlaka, asasi za kiraia, na kikundi cha kidiplomasia, ambacho atatoa hotuba ya kwanza ya safari hiyo.
Mara tu baada ya hapo, atasafiri hadi kwa Masista Wamisionari wa Mtakatifu Agostino huko Bab El Oued kutembelea kituo cha urafiki ambacho wameendesha kwa miaka mingi. Ziara hiyo itakuwa ya faragha, huku mkutano na jumuiya ya Algeria katika Kanisa Kuu la Mama Yetu wa Afrika ukifanyika hadharani saa 10:40 jioni. Hotuba pia imepangwa kwa ajili ya tukio hili
Kutoka Algiers, siku inayofuata, tarehe 14 Aprili, Papa Leo XIV atasafiri hadi Annaba, jiji la kale la Hippo, ambapo Mtakatifu Agostino alikuwa Askofu. Papa atatembelea eneo la akiolojia na nyumba ya wazee inayoendeshwa na Dada Wadogo wa Maskini. Kufuatia utamaduni ulioanzishwa na Papa Francisko wakati wa ziara zake za Kitume, ambapo kila mara alitenga muda wa mkutano kwa ajili ya ndugu zake wa Kijesuit, Papa Leo XIV pia atakutana faraghani na wanashirika wa Shirika la Mtakatifu Agostino katika nyumba ya jumuiya saa 6:10 mchana. Programu itaanza tena alasiri saa 9:30 na Misa katika Kanisa Kuu lililopewa jina la Baba wa shirika lake la Kitawa. Baada ya Misa, Papa atarudi Algiers. Kuondoka saa 12:00 jioni, kuwasili saa 1:10 usiku.
![]()
Nembo ya Ziara ya Kitume ya Papa nchini Algeria(13-14 Aprili 2026)
Vituo Vitatu Nchini Camerun
Kutoka mji mkuu wa Algeria, Papa Leo XIV ataondoka asubuhi inayofuata, tarehe 15 Aprili 2026, na sherehe itafanyika katika uwanja wa ndege saa 3:40 asubuhi na kuondoka saa 4:10 asubuhi. Mahali ataelekea: Yaoundé, Camerun. Papa atawasili saa 9:20 alasiri hivyo kuanza ziara yake ya Afrika nyeusi, kama waitavyo. Huko Yaoundé, Papa Leo XIV atamtembelea Rais Paul Biya katika Ikulu ya Rais, kukutana na mamlaka na wanadiplomasia katika Jengo la Mikutano (hotuba imepangwa), na, saa 11:45 jioni, atatembelea Kituo cha Yatima cha Ngul Zamba, ambapo atawasalimu wageni na wafanyakazi. Siku hiyo itaisha saa 12:25 jioni kwa mkutano wa faragha na maaskofu wa Camerun katika makao makuu ya Baraza la Maaskofu.
Ratiba ya Camerun inaendelea huko Bamenda, jiji lililoko magharibi mwa nchi, mji mkuu wa idara ya Mezam. Kuwasili kwa Papa kumepangwa kufanyika saa 4:05 asubuhi Alhamisi, 16 Aprili 2026; mara tu baada ya hapo, saa 5:30 asubuhi, Papa atashiriki katika Mkutano wa Amani na jamii ya wenyeji katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yoseph na kutoa hotuba.
Alasiri, saa 9:15, ataadhimisha Misa katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa, ambapo ataondoka kwa safari ya ndege ya saa moja kurudi Yaoundé. Na kutoka Yaoundé, Papa Leo XIV atasafiri, tarehe 17 Aprili 2026 hadi mji wa tatu kwa ukubwa nchini Camerun: Douala, mji mkuu wa mkoa wa Littoral kwenye Ghuba ya Guinea, moja ya vituo vikubwa vya mijini nchini na vinavyochukuliwa kuwa mji mkuu wa kibiashara wa nchi hiyo. Safari hiyo ni fupi ya ndege kwa dakika 55. Kituo kama hicho huko Douala pia ni kifupi, ambapo Misa imepangwa kufanyika saa 5 asubuhi katika Uwanja wa Japoma, na ziara ya kibinafsi katika Hospitali Katoliki ya Mtakatifu Paulo imepangwa kufanyika saa 7:20 mchana, na saa 8:10 machana, kikundi hicho kitandoka kuelekea Yaoundé, ambapo alasiri watakutana na jumuiya ya Chuo Kikuu Kakatoliki cha Afrika ya Kati.
![]()
Nembo ya Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV nchini Camerun(15-18 Aprili 2026).
Ziara ya kwenda Angola
Kisha Papa Leo XIV ataaga Camerun Jumamosi, tarehe 18 Aprili 2026 , akisherehekea Misa saa 3:30 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Yaoundé-Ville. Hafla ya kuaga itafuata, lakini wakati huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Yaoundé-Nsimalen. Papa ataondoka saa 6:30 mchana na kufika Angola baada ya saa mbili na nusu baadaye, awamu ya tatu ya ziara yake ya kitume. Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa "4 de Fevereiro" wa Luanda, Papa Leo XIV atakaribishwa na wawakilishi wa nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika. Kama ilivyopangwa, atafanya mikutano mbalimbali ya kitaasisi, ikifuatiwa na ziara ya heshima kwa Rais João Manuel Gonçalves Lourenço katika Ikulu ya Rais na mkutano na mamlaka, ambao atatoa hotuba mbele yao. Hii imepangwa kufanyika katikati ya mchana; mkutano wa faragha na Maaskofu wa Angola utafuata jioni.
Kama ilivyo nchini Camerun, nchini Angola, Papa Leo XIV hatakuwa katika mji mkuu pekee, bali pia atatembelea miji mingine. Kisha, Dominika , Aprili 19, atasafiri hadi Muxima, katika Mkoa wa Bengo, unaojulikana kwa uzuri wake wa asili na makao yake katika kaburi la Marian "Mama Muxima." Kabla ya kuondoka kwake, Papa Leo XIV ambaye bado atakuwa Luanda, ataadhimisha Ibada ya Misa katika kitongoji cha Kilamba saa 4:00 asubuhi. Hili litakuwa tukio pekee la asubuhi. Alasiri, saa 9:40, Papa atasafiri kwa helikopta hadi Muxima. Atafika huko baada ya mwendo wa nusu saa kwa gari na mara moja atahamia kwenye uwanja ulio mbele ya madhabahu, ili kusali Rozari na waamini na kutoa hotuba. Safari ya kurudi, tena kwa helikopta, hadi Luanda imepangwa kufanyika saa 11:45 jioni.
Kituo cha tatu na cha mwisho cha Waangola kitakuwa Saurimo, huko Lunda Kusini, jiji ambalo limeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu huku wahamiaji wengi wakikimbia maeneo ya vita. Papa Leo XIV atawasili Saurimo tarehe 20 Aprili saa 3:20 asubuhi kwa ndege na kama mipango yake ya kwanza, atakuwa katika Nyumba ya Wazee, dakika kumi kutoka Uwanja wa Ndege wa Deolinda Rodrigues. Baada ya dakika chache za kupumzika, Papa Leo ataadhimisha Misa katika Uwanja wa Saurimo.
Mara tu baada ya chakula cha mchana, saa 7:45 mchana ataondoka jijini kurudi Luanda. Huko, katika mji mkuu, ambapo atafika saa 9:15 alasiri, atakutana na Maaskofu, Mapadre, wanaume na wanawake waliowekwa wakfu, na wahudumu wa kichungaji kutoka Parokia ya Mama Yetu wa Fatima. Hotuba imepangwa kwa ajili ya tukio hilo. Hili litakuwa tukio la mwisho la ziara yake nchini Angola, ambapo Papa Leo ataondoka Jumanne, tarehe 21 Aprili 2026, kuelekea huko Guinea ya Ikweta.
![]()
Nembo ya Ziara ya Kutume ya Papa Leo XIV nchini Angola(18-21 Aprili 2026).
Ziara ya kitume Nchini Guinea ya Ikweta
Safari ya ndege kutoka Luanda hadi Malabo, mji mkuu wa zamani wa nchi hiyo ulioko pwani mwa kaskazini ya Kisiwa cha Bioko, inachukua takriban saa mbili na nusu. Ziara ya heshima kwa Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo na mkutano na mamlaka (wote katika Ikulu ya Rais) utafanyika asubuhi. Mkutano na ulimwengu wa utamaduni utafanyika alasiri, saa 10:00, katika Kampasi ya "León XIV", kampasi ya Chuo kikuu iliyopewa jina lake la Chuo Kikuu cha Kitaifa. Baada ya kukamilisha mipango yake rasmi, Papa atasafiri tena, saa 11:15 jioni, hadi mahali pa mateso na utunzaji: Hospitali ya Akili ya "Jean Pierre Olie", iliyopewa jina la daktari maarufu wa magonjwa ya akili wa Ufaransa anayechukuliwa kuwa "rafiki" wa Guinea ya Ikweta. Katika kituo hicho, kilichozinduliwa Desemba 2025, baada ya karibu miaka kumi, kituo cha huduma ya magonjwa ya akili chenye umuhimu wa kitaifa na kimataifa, Papa Leo XIV atawasalimu wafanyakazi na wagonjwa na kuwakaribisha kwa uchangamfu. Mkutano na Maaskofu wa Guinea, uliopangwa kufanyika saa 1:00 jioni hiyo utakuwa wa faragha.
Siku yenye shughuli nyingi zaidi katika ziara ya Papa Leo XIV barani Afrika itakuwa Jumatano, tarehe 22 Aprili 2026 ikiwa na safari mbili siku hiyo hiyo. Saa 2:10 asubuhi, Papa atasafiri kutoka Malabo hadi Mongomo, ambapo atatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa "Rais Obiang Nguema" Mengomeyén na kuadhimisha Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Asiye na Dhambi. Saa 6 :30 mchana atatembelea "Shule ya Teknolojia ya Papa Francisko," mpango uliopewa jina la Baba Mtakatifu wa Argentina. Saa 9:10 alasiri Papa Leo XIV atapanda ndege tena kuelekea Bata, mji mkuu wa kisiasa wa taifa hilo. Huko, Papa Leo atapitia nyakati tatu zenye kugusa sana: Kwanza, ziara ya kutembelea gereza, ambapo pia kuaga kumepangwa; Kisha kutakuwa na wakati wa maombi katika Ukumbusho wa Waathiriwa wa Mlipuko wa Silaha mnamo tarehe 7 Machi 2021, ambao ulisababisha vifo vya watu 20 na takriban 500 kujeruhiwa. Hatimaye, atakutana na vijana na familia Uwanjani, ambao atahutubia hotuba. Baada ya programu, Papa ataondoka Bata saa 7:40 mchana kurudi Malabo.
Malabo itakuwa mahali pa tukio la mwisho la Ziara ya Papa barani Afrika
Misa katika Uwanja, wa Malabo tarehe 23 Aprili 2026, saa 4:00 asubuhi, itakuwa ndiyo inakamilisha ziara yake ya kitume. Na saa 6:45 mchana Papa ataaga nchi na kupanda ndege itakayomrudisha jijini Roma. Kuwasili kumepangwa saa 1:55 jioni.
![]()
Nembo ya Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV nchini Guinea ya Ikweta(21-23 Aprili 2026).
Kauli Mbiu na Nembo
Mbali na programu hiyo, Ofisi ya Habari yaVatican, pia imetoa nembo na kauli mbiu kwa ajili ya hatua nne za safari ya Ziara Baba Mtakatifu Leo XIV barani Afrika
Nembo na kauli mbiu Algeria
Nembo ya Algeria, iliyoongozwa na sanamu ya kale inaonesha njiwa wawili wakinywa kutoka katika kikombe kimoja, ishara ya amani na ushirika, na Chi Rho, nembo ya Kikristo, pamoja na ramani ya Algeria. Rangi za kijani, nyekundu, na nyeupe zinakumbusha bendera ya Algeria, huku njano ikimaanisha Vatican. Katikati na chini kuna kauli mbiu kwa Kiarabu, Amazigh, na Kifaransa: "La paix soit avec vous," iliyoandikwa kwa Kiarabu na salamu "Assalamu Alaykom." Inawakilisha mazungumzo na mkutano kati ya Wakristo na Waislamu na ni mwaliko wa ulimwengu wote wa kupata amani, udugu, na kuishi pamoja kwa amani.
Nembo na kauli mbiu ya Camerun
Nembo ya Ziara ya Camerun ina Biblia iliyo wazi, msingi wa maisha ya Kikristo, ambayo msingi wa maisha ya Kikristo unategemea muhtasari wa nchi, iliyopakwa rangi ya kijani, nyekundu, na njano ya bendera ya taifa. Kutoka upande wa kushoto kunainuka Msalaba, ishara ya kutangazwa kwa Injili, huku, chini yake, ikionekana monogramu ya Maria. Katikati, njiwa wa dhahabu anang'aa miale ya mwanga, akiwakilisha kitendo cha Roho Mtakatifu na kuenea kwa Habari Njema kote nchini.
Kulia, Papa Leo XIV anaoneshwa katika sala, ishara ya ushirika na usindikizaji wa kichungaji wa Watu wa Mungu. Kurasa za Biblia zina kauli mbiu: "Que tous soient un/ yaani, "Na ili wote wawe wamoja" (Yh 17:21), ambayo inakumbusha mada ya umoja katika Kristo na inahusishwa na kauli mbiu ya Papa ya kiaskofu, "In Illo uno unum."
Nembo na kauli mbiu ya Angola
Katika vivuli vya rangi nyekundu, ikikumbusha damu iliyomwagika katika historia ya nchi hii, nembo ya Angola ina ramani iliyofunikwa na mstari mweusi wenye umbo la wimbi, ambayo inakumbusha baraka na utambulisho wa Mwafrika, ikikumbusha ulinzi wa kimungu unaoambatana na taifa. Katikati, nusu duara ya manjano iliyozungukwa na petali inaashiria gurudumu la kogi, mfano wa kazi, kwenye bendera ya taifa, huku, pamoja na msalaba, ikiwakilisha Ekaristi. Petali hizo zinaashiria mulemba, mti wa mfano wa nchi, na mistari ya bluu inawakilisha mito ya nchi. Kwa ujumla, nembo hiyo inawakilisha Angola iliyobarikiwa na Mungu na kuongozwa na Papa, ikitembea kuelekea mustakabali wa amani, utu, na tumaini jipya, kama kauli mbiu, chini kulia, inavyosema: "Papa Leo XIV, mhujaji wa matumaini, upatanisho, na amani, anaibariki Angola."
Nembo na kauli mbiu ya Guinea ya Ikweta
Msalaba wa dhahabu, ishara ya Kristo Aliyefufuka na imani ya Kikristo, ni maelezo ya kwanza ya kuvutia katika nembo ya Guinea ya Ikweta. Katikati inaonyesha ramani na bendera ya nchi upande mmoja, na familia, ikiwakilishwa na maumbo ya mwanamume, mwanamke, na mtoto, kwa upande mwingine.
Hapa chini, mwanaume ndani ya mtumbwi akiwa ameshika kitabu anakumbusha kuwasili kwa wainjilishaji wa kwanza baharini miaka 170 iliyopita. Rangi za dhahabu, kijani, nyeupe, na nyekundu zinakumbusha mwanga wa Kristo, dunia, amani, na mapambano ya uhuru. Kauli mbiu "Kristo, mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea mustakabali wa matumaini" inaelezea kumbukumbu ya yaliyopita na ujasiri katika safari ya imani na matumaini kuelekea mustakabali.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.
