Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV huko Monaco Machi 28. Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV huko Monaco Machi 28. 

Askofu Mkuu wa Monaco:Ziara ya Papa Leo XIV itatusaidia kutambua 'umaskini uliofichwa'

Askofu Mkuu Dominique-Marie David akizungumza na Vatican News alieleza udhaifu wa kiroho wa nchi hiyo ndogo ambapo utajiri mara nyingi huficha"upweke"mkubwa na"mgogoro wa maana ya maisha."

Na Edoardo Giribaldi - Vatican.

Papa Leo XIV anaanza Ziara  yake ya Kitume ya siku moja kwenda katika Ufalme wa Monaco siku ya Jumamosi, tarehe 28 Machi 2026. Mara nyingi, huonekana kama kitovu cha wasomi, utajiri wa wageni wanaotembelea nchi hiyo ndogo ya Ulaya kwenye Mto Riviera wa Ufaransa ambayo huficha upweke na wasiwasi uliofichwa, kwa mujibu wa Askofu Mkuu Dominique-Marie David, Askofu Mkuu wa Monaco. Alibainisha hayo katika mahojiano ambayo tunakuletea ya Vatican News, kabla ya ziara ya Papa, ambapo Askofu Mkuu David anatoa uelewa wake kuhusu utume wa kiroho wa Kanisa katika jiji la starehe.

Mwashamu, jambo moja la Monaco ambalo mara nyingi halisisitizwi sana ni mwelekeo wake mkubwa wa kiutamaduni. Ukweli wa Utawala wa Kifalme unaweza kuwaambia nini Kanisa la ulimwengu wote wakati wa ziara ya Papa Leo XIV?

Mojawapo ya sifa zilizonishangaza zaidi nilipofika kama Askofu Mkuu miaka sita iliyopita ni kwamba, ndani ya Jimbo dogo kama hilo, lenye kilomita mbili za mraba, hali halisi tofauti sana zinaishi pamoja. Huko Monaco, karibu mataifa 150 yanawakilishwa: kwa maana fulani, ulimwengu mpana upo katika nafasi hii ndogo. Mara nyingi mtu huwa na taswira ya Ufalme, unaoonekana tu kama jiji la starehe. Kiukweli, utajiri wake unatokana na aina mbalimbali za asili na pia kutokana na mchanganyiko fulani wa kijamii.

Kiukweli, watu wengi hufanya kazi Monaco bila lazima ya kuishi huko. Yote haya yanachangia utajiri wa nchi yetu na Kanisa. Kwa sababu hiyo, naamini kwamba, pia kwa Papa, kutembelea nchi ndogo kama hiyo kunaweza kuwa na maana muhimu, kwani atahutubia ulimwengu mzima. Dhamira yake ni kuleta Injili, kuimarisha imani, na kueneza ujumbe wa amani na heshima ya mwanadamu. Kwa hivyo kuna uwezekano kwamba mwangwi wa ziara kama hiyo utavuka mipaka ya Nchi  yetu dogo.

Mara nyingi Monaco huonekana kama ishara ya utajiri. Ni aina gani za umaskini ambazo hazionekani? Je, kuna mapungufu ambayo ni ya kiuchumi, lakini pia ya kimahusiano, ya kiroho, au ya kiutamaduni?

Umaskini ni mwingi na mara nyingi ni mkubwa sana. Mimi mwenyewe niliufahamu katika miaka ya hivi karibuni, kwa sehemu shukrani kwa wale walionisaidia kujua ukweli wa Monaco zaidi ya dhana potofu na picha zinazoenezwa na vyombo vya habari. Kwanza kabisa kuna umaskini wa kimwili, wakati mwingine umefichwa sana na ni vigumu kuona. Karibu na Ufalme wanaishi watu wengi wanaofanya kazi huko na kuchangia maisha ya nchi, lakini wakati mwingine hujikuta katika hali ngumu, hasa kuhusu nyumba au gharama ya maisha. Vyama vingi, ikiwa ni pamoja na Jimbo letu, vinazingatia hali hizi.

Pamoja na matatizo haya ya kimwili, hata hivyo, kuna aina nyingine za umaskini: upweke na mgogoro wa maana ya maisha. Mtu anapofurahia ustawi fulani na hana wasiwasi mkubwa wa kimwili, maswali mengine huibuka: mtu anapaswa kutoa maana gani kwa maisha yake? Si nadra kukutana na watu wanaoteseka kutokana na upweke. Pia tunaona wazazi ambao wamechanganyikiwa wanapokabiliana na elimu ya watoto wao, kutengana na matukio ya kifamilia ambayo yanaonekana zaidi kwa sababu maisha yanaonekana, angalau kwa mwonekano, kuwa rahisi zaidi. Kwa sababu hii, kazi yetu ni kuendelea kuwa makini na umaskini huu uliofichwa, kutunzana, na kujua jinsi ya kutambua hali za udhaifu ambazo, hata kama hazionekani kila wakati, ni halisi na wakati mwingine ni chungu sana.

Katika muktadha ambapo ustawi unaonekana kuwa kawaida, je, jinsi gani Kanisa linavyotambua na kushughulikia umaskini unaobadilika?

Kwa bahati nzuri, mshikamano upo sana. Huko Monaco, vyombo vyenye shughuli nyingi hufanya kazi kama vile Caritas Monaco, Jumuiya ya Mtakatifu Vincent wa Paulo, Shirika la Jeshi la Maria, na vyama vingi vya kikanisa au vya kiraia vinavyowatunza watoto walio katika shida, familia dhaifu, wazee, na wagonjwa. Uangalifu huu pia unaonekana katika hatua ya Kanisa. Wazo ni kwamba kutunzana na kutojiwekea mipaka ya kuishi katika nchi inayotoa maisha bora na usalama fulani. Utume wetu, hapa Monaco, ni kuwa makini zaidi kwa watu na kutokosa fursa yoyote ya kutoa ushuhuda wa Injili kwa wale wanaohitaji.

Hata hivyo, si nadra kupokea maoni yanayoonesha jinsi ujumbe fulani, baada ya muda, unavyoweza kufikia mioyo ya watu. Hili ndilo lengo letu: si kubaki juu juu, bali kumgusa mtu kwa kina. Zaidi ya majukumu na malengo tofauti ambayo kila mtu anaweza kuwa nayo huko Monaco, jambo muhimu ni kwamba mtu huyo apingwe ndani na kwamba moyo ujifungue kwa neno linaloweza kuamsha, kubadilisha, na kuelekeza maisha kwa wengine. Hatuwezi kuona matokeo mara moja kila wakati, lakini tunajua kwamba wengi husikiliza na kwamba, kidogo kidogo, njia inaweza kufunguka. Pia tunaona hili kutokana na idadi inayoongezeka ya watu wanaoomba Ubatizo au wanaotaka kuungana tena na Kanisa.

Je, imewahi kutokea kwamba unawaambia watu mambo ambayo hawatarajii kusikia kutoka kwa askofu?

Hapa, kama inavyojulikana, dini ya Katoliki ni dini ya Serikali. Kwa hivyo wengi wanatarajia kwamba Askofu na Kanisa wazungumze zaidi ya yote kuhusu uzoefu wa kiroho na kukaribishwa kwa imani. Hata hivyo, hasa wakati wa sikukuu ya kitaifa au matukio mengine muhimu, pia ninajaribu kukumbusha kwamba imani ya Katoliki si tu utambulisho wa kiutamaduni au urithi wa kihistoria. Pia ni jukumu linaloathiri njia yetu ya maisha, chaguo zetu, na utambuzi wetu. Kwa baadhi ya watu, huu unaweza kuwa mtazamo mpya. Haitoshi kujiita Mkatoliki, wala kujivunia kuwa hivyo. Mtu lazima pia aelewe matokeo yake katika jinsi tunavyoiona dunia, kwa wengine, hasa maskini zaidi, na katika mshikamano wa maisha yetu. Ikiwa mtu atabaki kushangaa, labda ni kwa sababu hii hasa: imani inahusisha matokeo na inahitaji mshikamano wa kweli wa maisha, kama Injili inavyopendekeza kwetu.

Kama ungelazimika kufupisha utume wa Kanisa huko Monaco kwa picha moja ya Injili, ungechagua ipi?

Nafikiria picha mbili za Injili. Ya kwanza ni ile ya kondoo waliopotea: kuhamasisha nguvu zetu zote kuanzia makuhani, walei, parokia, na harakati,  ili Habari Njema iwafikie pia wale wanaoonekana kuwa mbali zaidi au wasiotarajiwa. Ya pili ni tukio la Zakayo. Yesu anachagua kuingia nyumbani kwa mtu ambaye hakuwa na sifa nzuri, ingawa alikuwa tajiri na muhimu kijamii. Anafanya hivyo ili tu kumfanya agundue uzuri na furaha ya Injili. Kupitia ukaribu na urafiki, Yesu anamfunulia kwamba Ufalme wa Mungu tayari upo na unaingia katika maisha yake na moyoni mwake. Kwa hivyo, naamini kwamba ziara ya Papa itakuwa neema kubwa.

ASKOFU MKUU WA ALGERIA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

24 Machi 2026, 14:09